Msuva: Niligoma mazoezi ili niuzwe Wydad

MOROCCO. NIKIWA kwenye kambi ya Yanga iliyokuwa Marrakech, naamua kufunga safari kwa muda wa saa mbili na nusu nikitumia treni ya mwendokasi kutoka jijini hapo (Marrakech) hadi Casablanca, jiji lenye pilipilika nyingi na watu wengi na linatambulika kama mji wenye vurugu zaidi.

Ndani ya treni maisha ni matamu. Tiketi yako inaonyesha siti ya abiria na hakuna kusimamisha abiria. Kuna utulivu. Safari inaanza. Treni inaondoka kwa kasi.

Najiuliza ile ya kwetu inayojengwa na Serikali, itakuwa na burudani kama hii.

Safari yangu ni hadi Oasisi (wenyeji wanapatamka Osiz). Ni eneo aliloko staa mkubwa wa Tanzania, si mwingine ni mshambuliaji Simon Msuva.

Ndiko yaliko maisha yake kwa sasa akiwa na klabu ya Waydad Casablanca. Ni katika ghorofa moja lililoko kwenye eneo hilo lenye nyumba za kupanga. Hapo utampata kirahisi shujaa huyo wa taifa na nyota wa mabingwa wa Morocco, Wydad Casablanca iliyomnunua akitokea Difaaa Eljadid ya nchini humo.

Nashuka kwenye treni na moja kwa moja naenda kwenye eneo hilo. Nafika na kujitambulisha. Nawaambia nakwenda kwa Msuva (wenyewe wakitamka ‘Musuva’).

Mmoja ananiuliza ‘Wewe ni Mtanzania’ na kabla sijajibu naambiwa ‘Twende, twende’. Ni wazi walishaelewa mimi ni Mtanzania hasa kutokana na kumuulizia mwenyeji wangu ‘Msuva’.

Mwendo wa dakika nane tu tunafika nyumbani kwa Msuva. Tunamkuta nje akinisubiri. Ananiona na kutabasamu kwa furaha. Anashangaa kwa nilivyofika kirahisi nyumbani kwake.

Baada ya salamu ananikaribisha ndani na kisha tunaanza kupiga stori mbili tatu kufahamu maisha Morocco akiwa nyumbani na uwanjani.


MAISHA YA MOROCCO

Kwa sasa ana miaka minne nchini huko tangu alipotuakuitumikia Difaa. Anasema maisha ni mazuri na anaendelea kuzoea mazingira ya nchini huko lakini changamoto kubwa kwake ni lugha.

“Maisha hapa ni mazuri nashukuru Mungu. Kuna mambo ambayo naanza kuyazoea taratibu. Nimeishi hapa kwa miaka minne sasa na bado naendelea kupambana. Nina amani sana moyoni. Hata hivyo, kikubwa ni kujitambua tu uwapo mbali na nyumbani. Ujue unafanya nini,” anaeleza Msuva ambaye mbali na kufunga ana kasi ya ajabu.

Anaendelea kusimulia; “Changamoto kubwa ninayokutana nayo hapa ni lugha. Hapa wanatumia Kiarabu na wakati mwingine Kifaransa. Ni lugha ambazo sizifahamu ingawa kuna baadhi ya maneno naweza kuyatamka na nayatumia karibu kila siku. Mtu akiongea namwelewa ila kujibu ndio shida kidogo. Hakijanyooka (anacheka kidogo kama kawaida yake).


KUTOKA DIFAA HADI WYDAD

Difaa ndiyo klabu iliyomnunua akitokea Yanga ya Tanzania na anaelezea safari yake ya milima na mabonde hadi baadaye kujiunga na Waydad.

“Unajua ishu ya kuhama haikuwa rahisi. Baada ya kucheza msimu mmoja Difaa na kufanya vizuri, mmiliki wa timu aliniita na kunieleza anatamani aniuze, lakini iwe faida kwa wote, kwake na kwangu.”

“Wakati huo tunataka kwenda katika Fainali za Mataifa Afrika kule Misri, tukakubaliana nikienda kule nikafanye vizuri na kama nikifanikiwa kuonyesha uwezo mambo yatakwenda vizuri.

“Bahati mbaya hazikuwa fainali nzuri kwetu, tukaishia hatua ya makundi na hivyo kuzorotesha dili zangu nyingi na kulikuwa na ofa nyingine mbalimbali hasa za kwenda Uturuki.


UVIKO-19 YATIBUA ZAIDI

“Tatizo lingine ni mmiliki huyo alikuwa anataka pesa nyingi kutoka kwenye hizo ofa. Bila kujali matokeo ya Taifa Stars Afcon, bado kuna klabu zilikuwa zinanitaka ila akawa anaweka ngumu na alitaka pesa nyingi. Wakati anakataa pesa hizo , ghafla likazuka janga la Uviko-19 na kuharibu kila kitu,” anasema kwa masikitiko na kuendelea, katika kuzifuata zile timu ili kuzungumza nao, walimwambia kwa hali ya uchumi ilivyokuwa kipindi kile, haikuwa rahisi tena kukubali kiwango chochote labda nusu ya zile walizotaka kutoa awali.

“Niliumia sana na mmiliki alijua wazi ameniumiza kwani nilishaanza kujiandaa kuondoka.”


RAIS WA KLABU AFUNGUKA UKWELI

Msuva anasimulia baada ya kushindikana kwa madioli hayo hasa kutokana na janga la Uviko-19, rais wa klabu hiyo alimwita tena na kufunguka ukweli wa madili hayo.

“Alikataa pesa zao kwani aliona mimi ndiye mchezaji pekee nitakayeweza kumwingizia pesa nzuri baada ya kuniuza, kutokana na ubora wangu na malengo yake yalikuwa kupata pesa nyinngi ili aweze kuwalipa wachezaji wengine. Nilimwelewa kwa kuwa wakati huo nikweli klabu ilikuwa inapitia nyakati ngumu kifedha.


WYDAD WAMFUATA

Baada ya muda nilitulia na kuendelea na majukumu yangu. Nakumbuka nikiwa nchini Uturuki kwenye kambi ya Taifa Stars, Kocha Ettiene Ndayiragije (unajua ni rafiki yangu sana), alinituliza sana akinihakikishia nitapata timu na akaniambia yeye sio wakala lakini atanisaidia kupata timu nzuri.

“Niliporudi klabuni, Rais akaniita na kuniambia kuna ofa nyingine mbili zimekuja . Moja ni ya timu iliyopanda daraja hadi ligi kuu na wana pesa sana. Hapo nikaamini akili yake ilitaka niende huko.

“Niliona hiyo sio timu sahihi kwangu kwa kuwa ndio inakuja ligi kuu kikubwa nitakachofuata kule labda ni pesa. Ilinivunja moyo. Nakumbuka kuna wakati nikawa hata raha ya kwenda mazoezini sina tena nabaki nyumbani. Kuna wakati akili ikikaa sawa narudi kazini maisha yakawa hivyo.

“Baada ya kuona hayo, rais akaniambia, kuna ofa nyingine kutoka Wydad. Sikusubiri, baada ya kuipima klabu na kugundua ni kubwa hapa inashiriki mara kwa mara mashindano makubwa na mastaa wakubwa wanaichezea, nikamwambia niko tayari.”

“Nilimwambia ongea nao niende huko. Wakati huo sikuwa na meneja. Nikamwomba Kocha Ettiene, akaniambia atanitafutia mtu mzuri. Nilimtafuta pia rafiki yangu Himid Mao. Yeye ana meneja mzuri na akaniambia ataniunganisha naye.”

“Ni muhimu kuwa na meneja huku kwa sababu klabu zao ni wajanja sana na wanaweza kukupa mkataba mbovu utakaokuumiza hasa ukiwa mtu mweusi.

“Walinipa mkataba, lakini yalikuwa yale yale. Himid aliniunganisha na meneja wake. Nikamtumia ule mkataba. Akaniambia kama ningeukubali, ungeniumiza kweli. akanisaidia kubadili baadhi ya vipengele na ulipokuwa sawa nikasaini Wydad.”

“Kama mtambuka kuna wakati ilivuma sana naondoka Difaa basi pale mimi nilikuwa tayari nimeshasaini muda mrefu ila maisha yangu huwa sipendi kuyaweka wazi sana katika jamii na sasa nashukuru Mungu nipo hapa Wydad naendelea kupiga kazi.


MAISHA WYDAD YAKOJE?

Msuva baada ya kueleze alivyohamia Wydad, sasa anaelezea maisha ya ndani ya klabu hiyo akisema ni klabu ambayo wachezaji wanaishi maisha kama ya klabu za Ulaya, wakiwa wanajitambua.

“Tangu nifike hapa nashukuru nilipokelewa vizuri. Nakumbuka kocha niliyemkuta awali hakuwa ananipa sana nafasi alikuwa kama amekariri nikicheza sana dakika 20 inawezekana. Nikianza au nikitokea benchi yaani ikifika dakika 20, atanitoa. Inawezekana alitaka nizoee taratibu na mimi nikajipanga na ndani ya muda huo huo lazima nifanye kitu kikuwa ili nizidi kumshawishi anipe muda Zaidi.

“Nakumbuka mwanzoni ilikuwa inaniumiza. Niliwahi kumfuata nahodha wa timu akaniambia, Simon tulia. Wewe ni mchezaji mzuri usiumie utacheza sana Wydad. Maneno yale yalinifariji kwa kuwa niliona kama wazawa walikuwa wanapewa nafasi zaidi kuliko mimi. Hata hivyo, baadaye yule kocha aliondoka na sasa tuna kocha mwingine.

“Hapa klabu inakupa kila kitu kinachotakiwa. Nyumba ya peke yako. gari ya kutembelea na kila kitu kinafanyika kwa kujali muda wao. Wanajua mchezaji wanayemsajili tayari ameshakuwa mchezaji mkubwa na haihitaji tena kufuatiliwa wanachotaka ni kuona unajituma.

“Mashabiki nao wananikubali sana, hilo nashukuru Mungu kuna wakati nikicheza vizuri nikitolewa unaona wanakasirika lakini hata nikiwa benchi wakiona natakiwa kuingia utasikia wanaimba jina langu niingie. Unajua ukijituma mpira haukufichi utakuweka mbele, na wao ndio maana wanataka sana kuniona nacheza na sijawahi kukumbana na hatua ya wao kunichukia zaidi ya kupenda kazi yangu.


MAISHA NA KOCHA MPYA

Msuva anasema sasa wako na kocha mpya ambaye alipofika tu amemwelezea kila kitu anachotaka kutoka kwake na akimhakikishia nafasi pia katika kikosi chake kama atafanya vizuri.

“Nimekwambia sasa tuna kocha mpya ambaye nashukuru Mungu naona kama nitakuwa naye vizuri. Nikiwa nyumbani hivi karibuni, alinipigia simu na kuniambia ananihitaji haraka Morocco. Unajua kuna mshambuliaji wetu wa kwanza ameondoka na nilipofika akaniambia ananihitaji hapa na sasa natarajia nitamfanyia kazi kwa kiwango kikubwa. Bahati nzuri huyu ni Mmorocco, lakini anajua Kiingereza na naona kama hili litanisaidia, kwani kocha aliyeondoka alikuwa hajui Kiingereza.


Unajua maisha ya Morocco yamemjenga vipi Msuva? Anamiliki nini na nini malengo yake akiwa na klabu hiyo? Usikose mwendelezo wa makala haya kujua undani wa maisha ya Msuva.