SEHEMU YA PILI - Msuva: Wydad si pa mchezo

BAADA ya kuangalia sehemu ya kwanza na maisha ya mshambuliaji Saimon Msuva akielezea hatua ya uhamisho wake kutoka Difaa kuja Wydad tunaendelea naye na sasa anazungumzia malengo yake katika mkataba wake ndani ya klabu hiyo bingwa wa Morocco.



HATA ASIA FRESHI

Msuva anasema bado ana deni kubwa la kufikia malengo yake ambayo ni kupaa zaidi ya Wydad huku akidhamiria kwamba akifika nusu tu ya mkataba wake awe ameondoka.

“Hakuna kitu unakifanya bila malengo, hapa nilisaini mkataba wa miaka mine na Wydad na nimepanga ndani ya miaka miwili tu niwe nimefanya makubwa ili nipate timu ya kwenda kuichezea Ulaya, ndio maana mnaona napambana sana, ndoto hii haitaweza kufikia kama nitalala. Natakiwa kupambana.

“Mpira bado unanidai sana nina kazi kubwa ya kufanya wakati huu nikiwa na nguvu, nashukuru katika mwaka wangu wa kwanza hapa nimefanikiwa kuchukua ubingwa. Sasa nilichopanga msimu ujao nataka nipate mafanikio zaidi nikiwa hapa ili msimu huohuo ukiisha tu jina langu lipae katika soko la mpira.

“Sio lazima iwe Ulaya nitaangalia nafasi iliyokuja, hata bara la Asia nikipata ofa nzuri wakati huo nitaiangalia. Unajua mwisho wa siku watu watakuja kuangalia Saimon amecheza nje amevuna nini katika maisha yake. Huwa nikiwaza kitu kama hicho, hata kama nimelala, usingizi unaondoka na napata kiu ya kufanya mazoezi zaidi.


UWEKEZAJI WAKE

Msuva ni wazi alivuna pesa nzuri wakati akihamia Wydad na hapa anaeleza juu ya kitu anachofanya katika matumizi ya fedha zake anazovuna nchini Morocco.

“Sisi wachezaji wengi sio wafanyabiashara asikudanganye mtu, ni wachache sana, sisi biashara zetu asilimia kubwa ni kujenga nyumba za kutosha kama ni za biashara basi tutatengeneza ‘apartment’ kingine zaidi labda tutanunua Bajaj zitakuwa nyingi na pikipiki za kawaida hiyo ndio miradi midogo ambayo tunafanya na mimi niko humohumo, nikikwambia nitauza unga wa chakula au mchele nitakudanganya labda lije wazo kutoka kwenye familia uwawezeshe wao waendeleze, lakini binafsi siko sana huko.

“Kusema ukweli wakati nakuja huku nilianza kujenga nyumba ya kawaida tu na nilipopata fedha za Difaa nikahakikisha inamalizika na ilimalizika ambayo ni kama niliwajengea wazazi wangu baadaye nikaongeza tena nyumba nyingine hapohapo kwa kuwa eneo lilikuwa kubwa nikajenga ghorofa flani hivi nashukuru Mungu wazazi wangu wanaishi sehemu nzuri hakuna shida.

“Mimi kama mimi bado nisidanganye nimeshajenga nyumba za biashara lakini sasa nataka kujenga nyumba yangu mwenyewe ambayo nitakuwa ndiyo nyumba yangu na familia yangu na mchakato huo nimeshaanza.


LUGHA NA MISOSI ZINAZINGUA

Msuva anaeleza kuna mambo mawili yanampasua kichwa sana akiwa Morocco na kitu cha kwanza ni lugha kama ambavyo awali alieleza lakini kingine ni chakuka, hajazoea vyakula vya kule na anapata wakati mgumu katika maisha yake ya chakula huku akimtaja mtu ambaye anamsaidia sana.

“Chakula kinanipa shida sana, nimeshindwa kuzoea vyakula vyao, inanilazimu kutafuta njia ya kula chakula ambacho nimezoea, nina kaka yangu hapa anaitwa Midrad ambaye ni raia wa Burundi ambaye anaishi hapa kama daktari huyu ndio msaada mkubwa kwangu.

“Nisiseme uongo sijui kupika sana, kuna vyakula vichache sana ninavyojua kuviandaa kama vitu vya chai au wali lakini kaka yangu huyu anajua kupika. Sio kwamba namfanya kama mpishi wangu hapana huwa namuita tunakaa wote anaandaa chakula na mimi naandaa kitu kingine baso mwisho wa siku najikuta nimekula chakula ninachokifahamu.

“Mimi najua kutengeneza pia tambi, ubwabwa kama nilivyokwambia najua kupika ingawa kuna wakati kama chakula cha watu wawili huwa naogopa kutoa boko ila nikiwa peke yangu huwa napambana hivyohivyo, hivyo vyakula vingine kama pilau na vingine nisiseme uongo sina ujuzi navyo. Nikikosa kabisa basi nitakula chapati au mikate, unajua maisha yetu ya mpira yanatulemaza ukiwa kambini ukitioka mazoezini unakuta chakula kipo tayari ni ngumu sana kujua kupika vizuri.

“Kuhusu lugha kuna wakati nahitaji kutoka ndio kwenda kutafuta vitu mbalimbali sasa nikiwa natoka namwambia kabisa kaka yangu Midrad kwamba ebwana. ‘natoka kaa na simu yako karibu ili nikifika pale dukani nampa anaongea nao. Yeye ndugu yangu bahati nzuri anajua Kifaransa, unajua Warundi kwao wanajua Kifaransa lakini pia amekaa sana huku anajua hata lugha yao.

“Shida nyingine ya watu wa hapa Kiingereza hawakipendi na ni kama wanaona wakiongea Kiingereza wanajidhalilisha, wana dharau hizo, kwahiyo unaweza kwenda sehemu hata kama anajua Kiingereza lakini bado atajifanya hajui ili tu akukomoe ukizingatia na rangi zetu hizi ndio kabisa tena unaweza ukakutana na mtu akajifanya kama hakuelewi. ila nashukuru Mungu mimi hapa nafahamika, wakiniona wananipa ushirikiano wa haraka.


WAMEMPA BENZ LA KISASA

Msuva anaeleza vitu ambavyo amevipata akiwa na Wydad na hapa anaeleza kwasasa anatumia gari moja ya kisasa aina ya Merecedes Benz aliyopewa na bosi mkubwa wa klabu yake lakini pia akisimulia changamoto za barabarani anazokutana nazo.

“Hapa pia nilivyofika mbali na kunipa nyumba walinipa gari moja ndogo niliitumia kwa muda flani baadaye ikaleta shida, kuna siku nikawa natoa taarifa kwamba gari yangu imepata tatizo sasa bosi mmoja wa klabu akasikia na kwa wakati huo hakukuwa na gari nyingine ndogo ya kunipa nilienda nyumbani nikashtuka naitwa chini na kupewa gari ya kisasa Marcedes Benz. Wiki hiyo nilifunga sana. Naona bosi alifurahi, sasa sijajua ndio nitakuwa naitumia moja kwa moja au wataniletea lingine na hili wachukue.

“Mimi sio mzururaji sana, mara nyingi kama unavyoiona hapo nje imepaki tu. Mimi napenda sana kupumzika muda mwingi. Kutoka ni mara moja moja sana. Wakati naanza kuendesha gari huku nilipata wakati mgumu, unajua huku barabara zao ni kubwa na wanakimbia sana, halafu huku kwao magari mengi karibu yote usukani upo kushoto wakati kwetu Tanzania ni kulia ila sasa nimezoea kabisa hata nikirudi nyumbani nikipewa gari ya namna hii nitaendesha vizuri tu.

“Nilipofika hapa awali nilikuwa natumia leseni yangu ya Tanzania lakini baadaye wakanibadilishia wakanipa ya kwao ya hapa ingawa ya nyumbani ninayo halafu huku askari wao wa barabarani sio wasumbufu sana na pia madereva wengi wanajitambua barabarani na hakuna ajali za mara kwa mara, barabara zao ziko wazi sana kuelewa.”


BONGO UMUONDOA STRESS

Msuva sasa anazungumzia hatua ya wachezaji wengi wazawa kushindwa kumudu uvumilivu wa kucheza soka nje ya nchi na pia akifichua kwamba hata yeye kuna wakati mawazo ya namna hiyo humjia lakini baadaye anajikuta anaamua kupambana huku huku.

“Mimi sioni shida sana kama kuna mchezaji anakutana na wakati mgumu na anaamua kurudi nyumbani, sio kitu kibaya sana, inategemea unarudi ukiwa na mipango gani. Sioni sababu ya watu kuwaona waliorudui nyumbani kama wamekosea sana, sio kwamba tukiwa huku mwazo ya kuja nyumbani kwa sisi tulio huku hayatujii, yanakuja. Kuna wakati unajiuliza mbona nakutana na wakati mgumu wakati nyumbani sasa hivi klabu baadhi zinalipa vizuri na nyakati hizo unakuwa upo katika wakati mgumu hasa.

“Hiyo hali huwa inakuja kichwani lakini sijawahi kusema sasa nataka kurudi nyumbani na hakuna timu ambayo inaweza kunirudisha nyumbani kwasasa na wala sijawahi kupokea ushawishi wowote wa kutakiwa kurudi nyumbani, najua kuna klabu kama Simba,Yanga au hata Azam lakini kwa hatua ambayo nakwenda sasa watanirudisha kwa kitu gani.

“Mawazo ya kurudi yanakuja wakati ambao unaona hupati nafasi, mfano nilipokuwa Difaa nilikuwa nacheza kila mechi labda itokee mimi sitaki kucheza ila nilipokuja hapa mwanzoni nafasi nilikuwa sipati nakaa sana benchi, inakuwa kama kocha hakuamini na unaona una nafasi ya kufanya kitu kikubwa tu nyakati hizo huwa ndio ngumu kwa mchezaji.

“Unajua nikiwa Difaa hizi klabu kubwa za hapa hawa Wydad, Raja na hata Berkane mimi kila mechi hawa nilikuwa nawafunga nikiwakosa mechi hii basi inayokuja nawafunga, sasa nilipofika hapa nafasi hiyo nilikuwa naikosa ilikuwa inaniumiza kwakweli.”


STARS NA MZUKA

Msuva anafichua kwamba kila anapokosa nafasi katika klabu yake huwa anaomba sana kuitwa katika kikosi cha Taifa Stars ambako huko ndio humrudishia nafasi katika kucheza klabuni kwake.

“Nikiwa narudi Taifa Stars huwa napanga kabisa huko nakwenda kukiwasha kweli unajua hapa nilikuwa sipati nafasi lakini jambo zuri mashabiki, makocha na hata viongozi mchezaji akirudi kwenda kulitumikia taifa lake wanamfuatilia kwa karibu sana, sasa ikitokea nimeifungia Stars wanapata habari. Nilikwambia kwamba mashabiki hapa wananikubali sana. Sasa wakiona nimefunga, wanawafuata makocha na viongozi wakiwaambia kwanini hawanipi nafasi, kwahiyo mimi Stars ni kama mkombozi wangu, inanisaidia sana huku pindi ninapokuwa sipati nafasi na nikirudi Stars nikafunga na ndio maana huwa najituma sana ninapolitumikia taifa, inakuwa faida mara mbili taifa linafurahia kazi yangu lakini na mimi kuna kitu huwa najiongezea.


DAU LAKE LA SH2 BILIONI

Msuva anafichua mambo yaliyopo ndani ya mkataba wake na Wydad akisema akiwa hapo anapata karibu kila kitu mshahara kwa wakati posho za timu ikifanya vizuri lakini pia anaweka wazi kiasi ambacho kama timu yoyote ikimtaka basi inamchukua fasta.

“Mkataba wangu ni mzuri na hata klabu inauheshimu, hakuna matatizo, tunalipwa kwa wakati mishahara yetu licha ya hili janga la Covid 19. Tunaposhinda kuna posho mbalimbali tunapata za timu na sio kwamba mimi ninakuwa na zangu peke yangu ni kama timu ambavyo inajipangia na kwa wachezaji wake.

“Nashukuru Mungu kuna kipengele pia katika mkataba wangu ambacho kinaniruhusu kuondoka wakati wowote nikihitaji kufanya hivyo na tulikubaliana kimkataba kwamba kama timu itafika bei kuanzia Dola 1 milioni basi hawa jamaa wanaweza kuniachia lakini ikiwa zaidi ya hapo nayo hakuna shida, itategemea wakati huo niko kwenye kiwango bora kiasi gani.


UBINGWA WAMPA MZUKA

“Hii ni klabu kubwa sana sio klabu ya kawaida na hata nyumbani wasiizungumzie kama klabu walizozizoea, nimekuja hapa nimejifunza mengi sana jinsi mchezaji anavyotakiwa kutunzwa na mchezaji anavyotakiwa kukua kiakili, klabu hii imenibadilisha sana nimefika hapa haraka nimejikuta najitambua kwamba kumbe mimi naanza kuwa mchezaji mkubwa nikiangalia maisha ya wachezaji wa hapa na jinsi mchezaji anavyoheshimika na haraka nikajikuta najipangia malengo bora zaidi ninachoweza kusema kifupi Wydad wamenifanya nisiridhike nipambane Zaidi.

“Msimu wa ubingwa ulikuwa mzuri sana tulipambana kama timu tulikuwa na malengo ya mashindano ya Caf lakini pia tulikuwa na malengo katika ligi, tulishikamana kama timu kuanzia wachezaji mpaka makocha na mwisho juhudi zikatusaidia tukawa mabingwa.

“Hatua ya kufika tu hapa na nikawa bingwa imeniongezea ari zaidi ya kupambana lakini ubingwa huu ni wa kwanza kwangu tangu niondoke nyumbani kuja huku kuna kitu au thamani umeniongezea sasa sitakuwa tu mchezaji ambaye amecheza Morocco lakini kuna kitu kitatambulika kwamba amewahi kuchukua ubingwa.

“Nakumbuka wakati nasajiliwa tulikuwa wageni kama watatu na wote tumevuna mafanikio hayo tena tukicheza tulitambulika kama wachezaji ambao tuliongeza kitu katika timu yetu ukiacha wao wenyeji ambao wameshazoea kuchukua ubingwa wa hapa.”


USHAURI KWA FARID MUSSA

Msuva hakusita kumpa ushauri winga wa Yanga, Farid Mussa ambaye naye alikumbana na changamoto alipokuwa Hispania akimtaka kutambua yafuatayo.

“Farid Mussa sawa aliondoka Tenerrife ila bado ni mchezaji bora sana, asisumbuke na hilo, hajashuka kiwango, anachotakiwa kujua kipi anakitaka na mashabiki wanataka kipi kutoka kwake. Yanga ni klabu yangu naijua. Mimi niliishi pale. Hakuna mtu alikutana na wakati mgumu kama mimi ndani ya Yanga.”

Wajua hata mazoezini Msuva amekuwa akiwakera wachezaji wenzake, pia mkali huyo anafichua juu ya maisha yake ya mahusiano, unamjua mke wake mtarajiwa?


Itaendelea kesho.