Prime
Sakilu afungua mjadala mpya kuhusu ‘Doping’ Tanzania
Picha kwa msaada wa AI
Muktasari:
- Programu za kusaidia wanamichezo zinapaswa kuwa na vipengele vitatu muhimu ambavyo ni ushauri wa kisaikolojia, tiba ya mwili na lishe bora.
Wakati Tanzania ikiendelea kujijengea sifa katika mashindano ya kimataifa kupitia mafanikio ya wanariadha na wanamichezo wake, wadau wa michezo wanaonya kuwa maendeleo hayo yanaweza kuathiriwa na uelewa mdogo wa sheria na kanuni za matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni (doping).
Mbali na tamaa ya kupata matokeo ya haraka, ushawishi kutoka kwa marafiki, makocha na mitandao ya kijamii umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazowasukuma baadhi ya wanamichezo na vijana wanaofanya mazoezi ya kujenga mwili kutumia dawa hizo bila kuelewa madhara yake kiafya na kisheria.
KILICHOMSIBU SAKILU
Mfano wa karibuni ni wa mwanariadha wa Tanzania, Jackline Sakilu, aliyefungiwa na Kitengo cha Kusimamia Uadilifu katika Riadha (AIU) kwa miaka 10 baada ya kukutwa na matumizi ya dawa zilizokatazwa michezoni, hatua iliyomfanya kupoteza haki ya kushiriki mashindano ya kimataifa hadi mwaka 2035 na kufutiwa matokeo yake kuanzia Juni 2024.
Taarifa ya AIU ilieleza adhabu hiyo imeanza rasmi Septemba 17, 2025 na kwamba, Sakilu alikutwa na viambato vinavyohusiana na homoni ya testosterone, mojawapo ya dawa zilizopigwa marufuku chini ya Kanuni za dunia za kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.
Akizungumza na Mwananchi Septemba, 2025 baada ya tukio hilo, Rogart Akhwari, Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) alibainisha kwamba kilichomponza Sakilu ni kanuni za AIU na si kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.
"Kanuni za AIU zipo wazi kwamba ukitumia dawa za hospitali ambazo zina element (chembe chembe) ya zile zilizopigwa marufuku michezoni basi utoe taarifa, Jack (Sakilu) wakati huo alikuwa na injury (majeraha) hivyo alikuwa kwenye matibabu," alisema.
Alisema ambacho alikosea ni kutotoa taarifa AIU na katika utetezi wake mwanariadha huyo alipeleka cheti cha daktari, akibainisha: “Kilichomponza ni kutotoa taarifa na ameadhibiwa kutokana na kanuni."
Akhwari alisema dawa zikiwamo za pumu, mzio na baadhi ya zile za maumivu zinaweza kuwa na viambato vinavyohitaji mwanamichezo kupata kibali maalumu kabla ya kushiriki mashindano kwani huwa na chembechembe za dawa zilizopigwa marufuku michezoni.
Alisisitiza kuwa, Tanzania ni moja ya nchi bora duniani ambayo haipo kwenye kashfa ya matumizi ya dawa zilizokataliwa na AIU na mwaka 2025 ilipata Cheti cha Shirikisho la Dunia (WA).
Sakilu alikuwa miongoni mwa nyota wa timu ya taifa walioiwakilisha nchi kwenye michezo ya Olimpiki 2024 iliyofanyika, Paris Ufaransa.
Kocha na nyota wa zamani wa timu ya taifa, Suleiman Nyambui, alisema tukio hilo ni funzo kwa wanamichezo wote.
"Hii si mara ya kwanza kutokea. Wapo waliowahi kufungiwa, lakini kwa Sakilu adhabu imekuwa kubwa zaidi,” alisema akisisitiza elimu kwa wanamichezo kuhusu dawa zilizopigwa marufuku inapaswa kuimarishwa.
Mwanariadha ambaye hakutaka kutajwa jina anasema aliwahi kushawishiwa kutumia dawa hizo kuelekea mashindano ya kimataifa.
“Nakumbuka nilishawishiwa na kocha wangu. Nilidhani kujaribu hakutakuwa na madhara lakini badala yake nilijikuta nikiingia kwenye matatizo makubwa zaidi. Sikufanya vizuri na hatimaye nilikamatwa na kufungiwa. Ilikuwa aibu kwangu, kwa familia yangu na taifa langu. Ni tukio ambalo siwezi kusahau," anasema alipozungumza na Mwananchi.
SIYO RIADHA PEKEE
Mbali na wanariadha, matumizi ya dawa hizo yanaonekana pia katika vituo vya mazoezi (gym) huku baadhi ya wanaofanya mazoezi wakikiri kuwahi kushawishiwa kuzitumia.
"Kila mtu anataka mwili unaovutia. Wengine wanashawishiwa na marafiki zao, wengine wanachochewa na ushindani. Nilijaribu pia, niliona mwili wangu unakua haraka lakini sikuwa najua madhara ya muda mrefu," anasema Rashid Juma, ambaye amekuwa akifanya mazoezi ya gym kwa zaidi ya miaka mitano eneo la Kinondoni Studio.
Msimamizi wa Gym iliyoko Tabata Segerea, mkoani Dar es Salaam anayefahamika kama Masta Jay, anasema aliwahi kutumia dawa hizo akiamini zingemsaidia kupata misuli kwa haraka.
"Nilianza kutumia dawa za kusisimua misuli nikiamini zitaniwezesha kupata misuli kwa haraka lakini sikufahamu madhara yake. Mwanzoni niliona nakuwa na nguvu na mwili mzuri, baada ya mzunguko wa miezi kadhaa, nilianza kuhisi mabadiliko makubwa," anasema na kuongeza:
"Sikuwa na hamu ya kufanya shughuli za kawaida, nilikuwa nikipata usingizi kwa tabu, nilihangaika hospitalini kupata usaidizi. Ilinichukua muda hadi kurudi katika hali yangu ya kawaida."
USHAWISHI MITANDAONI
Mbali na ushawishi wa watu wa karibu, inaelezwa kuwa mitandao ya kijamii imeongeza shinikizo la matumizi ya dawa hizo.
Wataalamu wanasema mitandao ya kijamii imekuwa miongoni mwa vyanzo vinavyochochea vijana kutamani kupata miili yenye misuli au mwonekano unaofanana na wanaouona mtandaoni, hali inayoweza kuwafanya baadhi yao kujaribu dawa za kuongeza utendaji bila ushauri wa wataalamu wa afya.
Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii yanaweza kuathiri mtazamo wa vijana kuhusu mwonekano wa mwili, ingawa kiwango cha ushawishi hutofautiana kati ya tafiti.
Mchezaji wa ligi ya wanawake nchini ambaye hakutaka kutajwa jina anasema: "Nimekuwa nikiona video hivyo naweza kupungua mwili kwa kutumia dawa na siyo kufanya mazoezi."
NINI KINAFANYIKA
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Tanzania hutekeleza mfumo wa kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku kupitia Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa, kanuni za mashirikisho ya michezo na miongozo ya Shirika la Dunia la Kupambana na Matumizi ya Dawa Michezoni (WADA).
Mfumo huo unasimamiwa na Shirika la Taifa la Kupambana na Matumizi ya Dawa Michezoni (NADO Tanzania), lenye jukumu la kutoa elimu, kuratibu upimaji wa sampuli, kufuatilia ukiukwaji wa kanuni na kusimamia mashauri yanayohusiana na doping.
Tanzania pia ni miongoni mwa nchi zilizoridhia Mkataba wa UNESCO wa Kupambana na Matumizi ya Dawa Michezoni wa mwaka 2005, unaozitaka nchi wanachama kuimarisha elimu, kuzuia matumizi ya dawa hizo na kushirikiana na WADA katika utekelezaji wa viwango vya kimataifa.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, anasema changamoto kubwa si ukosefu wa sheria bali utekelezaji na kuwafikia wanamichezo wengi zaidi.
"Sheria zipo wazi na zimeundwa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. Tunayo idara ya maendeleo ya michezo kwenye wizara, kitengo cha tiba na kinga na kamati ya kitaifa inayotoa elimu kwa wanamichezo. Hata hivyo, changamoto kubwa ni utekelezaji wake katika vitendo, hasa kufikia wachezaji wa ngazi ya chini na michezo isiyopewa kipaumbele kikubwa, anasema na kuongeza:
"Tuna mhimili wa uchambuzi wa sampuli na kuchukua vipimo, kisha tunapeleka Afrika Kusini kwa msaada wa kitaalamu. Tunajitahidi kuhakikisha usahihi kabla ya kutoa zawadi au kuidhinisha matokeo. Pia, tunatoa mafunzo na mwongozo wa 'antidoping' hata kwa wachezaji wa mpira wa miguu."
Msitha anasema: "Tuna mipango mingi kuhakikisha tunawafikia wanamichezo zaidi kwa kushirikiana na vyama ili kuondokana na changamoto ya matumizi ya dawa ambazo zimekatazwa michezoni, matumizi ya dawa za kusisimua misuli hayakubaliki."
Mwanasheria Everlin Simtowe, anasema jambo la msingi si kuwapo kwa sheria maalumu ya kupambana na doping pekee, bali ni kuhakikisha mfumo uliopo unatekeleza viwango vya kimataifa, huku ukilinda haki za wanamichezo.
Anasema wanamichezo wanapaswa kuelewa kuwa sheria za doping zinatumia kanuni ya uwajibikaji binafsi, hivyo hawawezi kujitetea kwa msingi wa kutokujua walichotumia.
"Ni muhimu wanamichezo wafahamu wanawajibika kwa kila kitu kinachopatikana mwilini mwao. Hata kama dawa au kirutubisho wamepewa na kocha, daktari au mtu mwingine, bado mwanamichezo ndiye mwenye wajibu wa kuhakikisha hakiuki kanuni za WADA," anasema na kuongeza:
"Kutokujua sheria au kutokujua dawa uliyotumia imepigwa marufuku si kinga ya kuondoa uwajibikaji. Ndiyo maana elimu kwa wanamichezo ni jambo lisiloepukika."
Simtowe anasema: "Kesi nyingi zinaweza kuzuilika kama kutakuwa na elimu ya kutosha kuhusu dawa, virutubisho na taratibu za kupata kibali cha matumizi ya dawa kwa sababu za matibabu pale inapohitajika. Kinga bora dhidi ya doping ni elimu."
ATHARI ZA KIAFYA
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, matumizi ya dawa za kusisimua misuli yanaweza kusababisha shinikizo la damu, matatizo ya moyo, ini na figo, kuvurugika kwa homoni, ukosefu wa usingizi, msongo wa mawazo na kupungua kwa uwezo wa mwili kwa muda mrefu.
Dk Robert Kamau, mtaalamu wa tiba ya wachezaji anasema wanamichezo wengi hutumia dawa hizo wakivutiwa na matokeo ya haraka bila kujua athari zake.
“Wengi wanatumia dawa hizi bila ushauri wa daktari. Wanajua matokeo ya haraka ambayo yanapatikana lakini hawajui madhara, hasa kwa muda mrefu,” anasema.
Anasema programu za kusaidia wanamichezo zinapaswa kuwa na vipengele vitatu muhimu akivitaja kuwa ni ushauri wa kisaikolojia, tiba ya mwili na lishe bora.
Ushauri wa kisaikolojia anasema unasaidia mchezaji kuacha dawa hatari, kudhibiti msongo wa mawazo na kujenga nidhamu ya muda mrefu.
"Lishe ni msingi wa kurekebisha matatizo ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli. Programu zinapaswa kuhakikisha wanamichezo wanapata lishe bora, ikijumuisha virutubisho, protini na maji ili kuondoa nguvu ya dawa hizo," anasema.
Dk Kamau anasema huduma hizo zinapaswa kuwa endelevu, ikiwamo vipimo vya ufuatiliaji wa muda mrefu na matibabu ya kurekebisha afya.
Kwa wadau wa michezo, kulinda maendeleo ya Tanzania katika mashindano ya kimataifa hakutategemea vipaji pekee, bali pia kiwango cha uelewa wa wanamichezo kuhusu sheria za doping, matumizi sahihi ya dawa na uwezo wa kupinga ushawishi wa kutafuta mafanikio ya haraka kupitia njia zisizoruhusiwa.
Hamisi Tesha, daktari bingwa wa tiba ya michezo na majeraha ya wanamichezo, aliyewahi kufanya kazi na klabu ya Toto Africans ya Mwanza anasema:
"Dawa nyingi zinazotumiwa kuongeza nguvu au kasi ya kupona majeraha huathiri mfumo wa mwili kwa namna ambayo mchezaji hawezi kuiona mara moja, wapo wanaopata matatizo ya moyo, shinikizo la damu, figo, ini pamoja na kuvurugika kwa homoni za mwili jambo ambalo linaweza kuathiri hata maisha yao baada ya kuachana na michezo."
Anasema baadhi ya wanamichezo huamini kuwa wanaweza kupata mafanikio kwa kutumia njia za mkato badala ya kuwekeza kwenye mazoezi, lishe bora na nidhamu.
Anasema elimu inapaswa kuanzia katika akademi za vijana, shuleni na mitaani ili kuwajengea uelewa mapema kuhusu hatari za dawa hizo.
"Ukimfundisha mchezaji akiwa na miaka 12, 13 au 14 kuhusu madhara ya dawa za kusisimua misuli unakuwa umejenga msingi mzuri wa kumlinda katika maisha yake yote ya soka, hii ndiyo sababu akademi, makocha, wazazi na viongozi wa michezo wanapaswa kushirikiana katika vita hii," anasema.
MTAZAMO WA WADAU
Kocha wa Yanga Soccer School, Mohamed Badru, anasema matumizi ya dawa za kusisimua misuli kwa wanamichezo ni tatizo ambalo halijapewa uzito unaostahili katika nchi nyingi za Afrika Mashariki tofauti na mataifa yaliyoendelea ambako sheria na mifumo ya ufuatiliaji imeimarishwa kwa kiwango kikubwa.
Anasema uzoefu wake wa kufundisha soka ndani na nje ya Tanzania umemfanya kushuhudia namna baadhi ya wachezaji wanavyoingia kwenye matumizi ya dawa hizo wakiamini zitawasaidia kuongeza uwezo wao uwanjani, huku wengi hawafahamu madhara ya kiafya na athari zinazoweza kuharibu taaluma zao.
Kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambina anaeleza alipofanya kazi nchini Uingereza kwa zaidi ya miaka 10, alijifunza jinsi mifumo ya kudhibiti matumizi ya dawa hizo ilivyo madhubuti kiasi cha kufanya iwe vigumu kwa mchezaji yeyote kukwepa sheria.
Anasema ushawishi wa marafiki na mazingira yanayowazunguka vijana wengi ni changamoto kwao, baadhi yao wakiamini kuwa kutumia dawa hizo kunaweza kuwasaidia kupata mafanikio kwa haraka.
"Vijana wengi wanahitaji elimu zaidi, wengine wanaingia kwenye matumizi ya dawa hizi kwa kushawishiwa na wenzao bila kujua kuwa wanaweza kupoteza kabisa taaluma zao, tunawaambia kila siku kuwa kipaji, nidhamu, mazoezi na lishe bora ndiyo siri ya mafanikio ya muda mrefu," anasema.
Mchezaji wa kimataifa wa Tanzania, Emily Mugeta, anayecheza soka la kulipwa Ujerumani akiwa na FC Waldkirch, anasema: "Lazima tuwe na mfumo endelevu unaoshughulikia elimu, sheria na afya kwa pamoja huku (Ujerumani), wamefanikiwa katika hilo kwa sababu ya ufuatiliaji ambao wamekuwa nao mara kwa mara."