Prime
Ripoti Maalumu... Madhara madokta wasiosajiliwa haya hapa

Muktasari:
- Kwa mujibu wa machapisho mbalimbali, yapo baadhi ya madhara yanayoweza kusababishwa na wataalamu wa afya ambao hawajasajiliwa.
KATIKA makala yaliyopita gazeti hili, yalibainisha uwepo wa timu ambazo madaktari wake hawapo katika orodha ya usajili wa Baraza la Madaktari Tanzania kama Ibara ya 37 ya kanuni za usajili na utoaji leseni za klabu za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika zinavyotaka.
Ibara hiyo inafafanua hivi, "Kila klabu inapaswa kuwa na daktari anayefanya kazi kwa kuajiriwa au kwa mkataba. Daktari huyu anapaswa kuwa na sifa zinazokubalika na kutambulika na mamlaka za afya za nchi husika. Daktari anayekubalika kwa kazi hii lazima awe ameidhinishwa na baraza la madaktari au chombo kingine cha kitaifa kinachohusiana na usimamizi wa madaktari.”
Timu hizo ambazo hazina madaktari ambao wapo kwenye orodha ya MCT ni Fountain Gate, Pamba Jiji, Tanzania Prisons, KenGold, Kagera Sugar, Coastal Union na KMC.
Hata hivyo, Chama cha Madaktari wa Michezo Tanzania (Tasma) kimesema hakuna madhara yoyote ambayo yametokea kutokana na hilo na hao wote wanakidhi vigezo vya kuzisimamia timu walizopo.

Katibu mkuu wa Tasma, Juma Sufian anasema hadi sasa hakuna changamoto yoyote ambayo imetokea kutokana na kutokuwa na daktari aliye katika orodha ya Baraza la Madaktari Tanzania.
“Hakuna shida yoyote ambayo imetokea na mara kwa mara tumekuwa tukipeana uzoefu wa kitaaluma wa masuala mbalimbali yanayohusu tiba na madaktari wa timu zote zinazoshiriki ligi nchini.
“Madaktari wote ni wanachama wa Tasma na wanakidhi vigezo na miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa sheria na wamekuwa wakifanya kazi kwa weledi ya kutoa tiba kwa waajiri wao. Kimsingi niseme tu kuwa upande wa tiba, timu zina watu sahihi wanatoa huduma stahiki za matibabu,” anasema Sufian.
Sufiani anasema wamekuwa wakifanya mafunzo ya mara kwa mara ambayo wahitimu wake hupata vyeti maalum ambavyo bila ya hivyo, mtu haruhusiwi kufanya shughuli ya utoaji tiba katika timu.
Mchezaji wa Tanzania Prisons, Samson Mbangula anasema wamekuwa wakipata matibabu mazuri katika timu yao.
"Kwa upande wetu tumekuwa tukipata matibabu mazuri kutoka kwa idara yetu ya tiba. Unajua suala la majeraha linaweza kusababishwa na mambo mengi. Unaweza kuwa na daktari mzuri lakini mchezaji ukashindwa kujitunza.

"Au unaweza ukachezewa rafu kwa bahati mbaya lakini kiukweli upande wa matibabu tuko vizuri na nawashukuru madaktari wetu," anasema Mbangula.
Ofisa habari wa Mashujaa, Salum Kimwagu anasema wana imani kubwa na idara yao ya tiba.
"Madaktari tulionao wanakidhi vigezo na usalama wa wachezaji wetu ni mkubwa na ndiyo maana katika misimu hii miwili ambayo timu yetu imeshiriki Ligi Kuu, Mashujaa ni miongoni mwa timu ambazo hazijakumbana na changamoto kubwa ya majeraha na wachezaji wetu wamekuwa fiti.
"Kuna changamoto ndogondogo za kiafya ambazo zinaweza kumfanya mchezaji akose mechi moja au mbili lakini huwa sio kukosa idadi kubwa ya mechi," anasema Kimwagu.
MADHARA HALISI HAYA HAPA
Kwa mujibu wa machapisho mbalimbali, yapo baadhi ya madhara yanayoweza kusababishwa na wataalamu wa afya ambao hawajasajiliwa.
"Madaktari wasio na leseni hawana mafunzo, ujuzi na utaalamu unaohitajika ili kutoa huduma ya matibabu iliyo salama na yenye ufanisi. Matendo yao yanaweza kupotoka kutoka kwa kanuni za kawaida za matibabu na kusababisha utambuzi mbaya, matibabu yasiyofaa au makosa ya dawa.
"Zaidi ya hayo, kutokuwepo kwa ufuatiliaji wa kutosha wa matibabu na uangalizi kunaweza kusababisha matatizo au kuzorota kwa afya," unafafanua utafiti uliofanywa na www.klandrylaw.com.

Taasisi ya Sheba Roy iliyopo Michigan Marekani ambayo inajihusisha na tafiti za afya na tiba, imetaja madhara matano ambayo yanaweza kusababishwa na uwepo wa madaktari ambao hawajasajiliwa.
Utambuzi usioendana na tatizo na tiba isiyo sahihi ni athari ya kwanza ya taasisi kuwa na daktari asiyesajiliwa kwa mujibu wa Sheba Roy. Mtu asiye na leseni anaweza kukosa utaalam wa kutambua kwa usahihi hali ya mgonjwa na kusababisha utambuzi mbaya na matibabu yasiyofaa. Hii inaweza kuchelewesha utambuzi sahihi, kuzidisha hali ya mgonjwa na kupunguza uwezekano wa kupona kwa mafanikio.
Athari ya pili ni ukosefu wa mazoea yanayotegemea ushahidi. "Madaktari" wasio na leseni wanaweza kuwa hawajui utafiti wa kisasa wa matibabu au mazoea yanayotegemea ushahidi. Kwa hiyo, wagonjwa wanaweza kukabiliwa na matibabu ambayo hayajathibitishwa kuwa salama au yanafaa, ambayo yanaweza kusababisha madhara mabaya, afya mbaya, au hata kifo.

Unyonyaji na ulaghai ni kwa baadhi ya "madaktari" wasio na leseni ambao wanaweza kufanya hivyo kwa wagonjwa walio katika mazingira magumu, wakitoa matibabu ya gharama kubwa na yasiyofaa ambayo hayatoi manufaa yoyote. Hili linaweza kudhuru kifedha na kuhuzunisha kihisia kwa wagonjwa na familia zao.
Athari nyingine ni kukosekana kwa msaada wa kisheria. Kwa kuwa watu wasio na leseni hawazingatiwi viwango sawa na vya madaktari walio na leseni, huenda wasiwajibike kwa utovu wa nidhamu, uzembe, au madhara yanayosababishwa na wagonjwa. Ikiwa kitu kitaenda vibaya, wagonjwa wanaweza kukosa msaada wowote, kwani daktari asiye na leseni anaweza kuwa hana bima ya utendakazi au uwajibikaji wa kisheria.
Tokeo lingine hasi la uwepo wa madaktari wasio na leseni ni uwezekano wa kuingiliana kwa madhara na matibabu ya kawaida. Madaktari wasio na leseni wanaweza kukuza matibabu mbadala au ambayo hayajathibitishwa ambayo yanakinzana na matibabu ya kawaida. Matibabu haya yanaweza kuingilia kati na dawa au taratibu zilizowekwa na madaktari walio na leseni na kusababisha mwingiliano hatari au kudhoofisha ufanisi wa matibabu yaliyothibitishwa.
Itaendelea kesho