Prime
Ripoti Maalumu -3: Hii ndo dawa madaktari wasiosajiliwa Ligi Kuu

Muktasari:
- Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat), Dk Deusdedit Ndilanha anasema wataalamu ambao wanatoa huduma za afya kwa timu za soka wanatakiwa wasajiliwe MCT.
WADAU tofauti wa michezo na tiba wametoa maoni juu ya kile wanachoamini ni suluhisho la kumaliza changamoto ya uwepo wa madaktari kwa baadhi ya timu za Ligi Kuu ambao hawajasajiliwa na Baraza la Madaktari Tanzania (MCT).
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (Mat), Dk Deusdedit Ndilanha anasema wataalamu ambao wanatoa huduma za afya kwa timu za soka wanatakiwa wasajiliwe MCT.
"Hao wote wanatakiwa kama wanataka kufanya kazi ya kutoa huduma katika maeneo hayo ya tiba wawe wamesajiliwa na wawe na leseni ya kutoa huduma, ndivyo sheria inavyotaka. Kama kuna mtaalamu ambaye anatoa huduma kwa ngazi hiyo, lakini hana usajili, maana yake ni kwamba anavunja sheria," anasema Dk Ndilanha.

"Na itakapobainika kwamba anatoa huduma, lakini hana usajili maana yake sheria itafuata mkondo wake. Hadi sasa hatujapata taarifa ya uwepo wa wataalamu hao ambao hawana usajili. Lakini katika namna kwamba tutafahamu kwamba wapo watu wanafanya hizo tiba, lakini hawana usajili, utaratibu wa kawaida utafuatwa ili kuhakikisha kwamba sheria inafuata taratibu."
Dk Ndilanha anasema kuwa timu zinahitajika kupata uhakika juu ya uwezo wa wataalamu wao wa tiba.
"Sina utaalamu zaidi sana kwenye sheria za TFF, lakini ninachoweza kuzungumza ni kwamba kama kuna timu inamtumia mtu ambaye anajitanabaisha kuwa ni daktari ni vyema wajiridhishe kwamba huyo daktari ana usajili kinyume na hapo wanaweza kujikuta wanadhani wana mtaalamu kumbe sio mtaalamu.
"Sasa kama kweli kuna hiyo shida kuwa maana yake yeye mwenyewe atawajibika kwa taratibu za kisheria, lakini hasara itakuwa kwa timu kwamba wanatumia mtaalamu ambaye hana vigezo ambavyo wao wanavitegemea," anasema.
Mdau wa tiba, Dk Fredy Mpeli anasema madhara yanakuwa zaidi kwa mtaalamu husika wa tiba na sio wachezaji kwa vile madaktari hao wanachokikosa ni leseni.

“Kitaaluma hao wako vizuri, ila kinachowabana ni miongozo. Usajili huwa ni mmoja ila leseni ndio huwa zinahuwishwa kila mwaka. Kutibu ni lazima uwe umesajiliwa labda iwe hawajahuwisha leseni zao, jambo ambalo tunafanya kila mwaka,” anasema daktari huyo.
Ofisa habari wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Karim Boimanda anasema kanuni zimefafanua kuhusu masuala ya tiba, hivyo ni jukumu la klabu kuzifuata.
“Kanuni za ligi zimeelezea vizuri kuhusu mahitaji yanayohusu tiba na kuna chama cha Tasma ambacho kimekasimishwa mamlaka ya kusimamia mambo yote yahusuyo tiba. Jukumu la Bodi ya Ligi ni kusimama kanuni ambazo kwa sasa zinafuatwa vizuri bila kuvunjwa na ikitokea kinyume hatua zitachukuliwa,” anasema Boimanda.
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Dar es Salaam, Lameck Nyambaya anasema anaamini klabu zitaendelea kufuata kanuni na miongozo ya TFF na Bodi ya Ligi.
“Naipongeza TFF, Bodi ya Ligi na Tasma kwa kuziweka kanuni nzuri na zenye mashiko kuhusu tiba za wachezaji ambazo klabu zikizitekeleza vizuri, wachezaji wetu watakuwa salama na mpira utachezwa.
“Ushauri kwa klabu ni kuhakikisha zinawajibika kuzitekeleza hizo kanuni na miongozo kwa faida yao wenyewe pamoja na wachezaji. Ligi yetu imepiga hatua kubwa hivyo klabu zetu zinapaswa kuendana na kasi ya kukua kwa ligi yetu,” anasema Nyambaya.

Katibu mkuu wa Baraza la Madaktari Tanzania, David Paul anasema klabu na TFF zinapaswa kushirikiana na baraza ili zipate ushauri wa kitaalamu.
'Milango iko wazi kwa TFF na timu kututafuta baraza kwa ajili ya kusaidiana kwa maoni na ushauri ili kusitokee changamoto au wasingoje hadi kutokee jambo ndio watuone. Baraza muda wote liko wazi na tutawapa ushirikiano mkubwa na wa kutosha," anasema Paul.
Kiungo wa zamani wa Yanga, Hussein Swedy anasema kuna haja ya kuboresha kanuni ili kuzibana zaidi timu.
"Inaonekana kanuni za sasa za ligi hazizibani sana klabu hivyo lakini zikifanya hivyo nadhani kila moja itakuwa na daktari au madaktari waliosajiliwa. Kanuni ndio kila hivyo ikiwepo ambayo inazilazimisha timu kuwa na madaktari waliosajiliwa, zitakuwa nao tu.

"Mfano mwanzoni ilionekana itakuwa ngumu kwa klabu kuwa na timu za vijana lakini hii kila moja iliyopo katika ligi ina vikosi vya vijana hivyo kila kitu kinawezekana ni kuamua tu," anasema Swedy.