Prime
RIPOTI MAALUM -3: Kinachotakiwa kufanyika soka la vijana

Muktasari:
- Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao anasema kuna changamoto mbalimbali kwwenye utekelezaji wa leseni ya klabu hususan kwenye eneo la soka la vijana, huku akitaja kinachokwamisha na namna shirikisho hilo linavyojipanga kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko makubwa.
JANA katika mwendelezo wa ripoti maalumu juu ya ukiukwaji wa kanuni ya Leseni kwa klabu nchini, tuliona namna klabu 16 za Ligi Kuu zinavyoendesha mchakato wa kupata wachezaji wa timu za vijana. Leo tunaendelea kuona vitu gani vinavyopaswa kufanywa ili kuweka mambo sawa katika utekelezaji wa kanuni hiyo ya leseni za klabu ili kuhakikisha soka la vijana linaleta ufanisi zaidi nchini. Sasa endelea...
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa anasema kwa sasa wamejipanga kuweka mazingira wezeshi kwa akademi za soka ili kutimiza vigezo vya kukuza vijana na hilo litawavutia wawekezaji kufungua vituo vingi zaidi ili kukusanya vipaji vingi.
Msigwa anasema wizara kwa kutambua umuhimu wa soka kwa vijana wanapambana kutafuta wafadhili kutoka nje ya nchi watakaowekeza na kufanya biashara ya kukuza na kuuza wachezaji wenye vipaji nje ya nchi ili Taifa na vijana wanufaike.

“TFF ambayo ni msimamizi mkuu wa kanuni ina kazi ya ziada kuhakikisha inasimamia timu zinazoshiriki Ligi Kuu kutilia mkazo suala la soka la vijana kwani hao ndio wachezaji wa timu ya Taifa na klabu mbalimbali hapo baadaye,” anasema.
“Tumeandaa Umiseta na Umitashumta ili baadaye wawekezaji na klabu kupata wepesi wa kuchukua vipaji vya watoto waliopo shuleni, kwani kupitia mashindano kama haya wanapata nafasi ya kuonyesha uwezo wao na kuukuza kuanzia shuleni, jambo ambalo ni la msingi.”
Msigwa anaongeza, “BMT (Baraza la Michezo Taifa) watembelee akademi na wataalamu wa michezo na wasiwafungie ila wawape ushauri wa kuboresha zaidi. Lakini shuleni tumeendelea kuweka walimu wa michezo ili kuhakikisha kuwa kuna somo maalumu wale wenye vipaji waanze kupata elimu mapema.”
Naye Katibu wa BMT, Neema Msita anasema hakuna mwamko mkubwa kwa klabu, lakini serikali imeamua kuanzisha vituo maalumu vya kuzalisha vijana umri wa kuanzia miaka 10 hadi 14 watakaozisaidia zile timu za miaka 17 na 20 zilizopo kwenye klabu za Ligi Kuu Bara.

“Timu nyingi zimejikita kuendesha kwa malengo ya kutafuta fedha, lakini hata Serikali tunajua tunapata faida hapo. Lakini tumekuwa tukiwalazimisha kuhakikisha wanawekeza kwenye soka la vijana,” anasema Msita.
“Njia nzuri tunayoiona Serikali kuhakikisha tunakuwa na matokeo sahihi - tumerudi shuleni ndio maana tumeimarisha hizi shule maana yake tunataka watoto wacheze kuanzia shuleni. Wakishamaliza kushindana shuleni sasa tutazilazimisha klabu wakati hawa watoto wanashindana huku waende wakachukue vipaji kwa sababu wanakuwa wengi.
“Tumeenda mbali kama serikali kuhakikisha tunakuwa na akademi zetu kwa kuzitengeneza shule 56 za sekondari ambazo zitakuwa vituo vya michezo. Changamoto tunayoipata ni kwa shule za msingi ambazo wanafunzi wanasoma na kurudi nyumbani. Tumeendesha mafunzo ya makocha na bado tutaendelea lakini tutaimarisha pia miundombinu.

“Kwa hiyo Serikali tumeona tuchukue mkazo wa kulea kuanzia chini ili hizi klabu zijikite na hizi timu za miaka 17 na 20, lakini ndani yake tuzilamishe kuzingatia kuzilea hizo timu ipasavyo ili hawa wanaotoka kuzalishwa huku shuleni wawe na timu za kuwapokea.”
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao anasema kuna changamoto mbalimbali kwwenye utekelezaji wa leseni ya klabu hususan kwenye eneo la soka la vijana, huku akitaja kinachokwamisha na namna shirikisho hilo linavyojipanga kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko makubwa.
“Changamoto ambayo ni kubwa ni namna ambavyo watu wanatakiwa wajue kwamba hakuna njia ya mkato kwenye mafanikio ya mpira. Bila kuwekeza kuanzia chini hatuwezi kufanikiwa ni lazima kazi ifanyike na unaweza kuangalia kwenye maeneo matano ya leseni ya klabu ya kutekeleza. Kuna maeneo yanatuelekeza ni lazima yafanyike na moja ya eneo la lazima ni hili la maendeleo ya soka la vijana,” anasema Kidao na kuongeza:

“Changamoto kubwa ya utekelezaji wa leseni ya klabu sio Tanzania tu, tumekuwa na vikao vingi vya namna ya kutekeleza Afrika nzima na kila wakati tumekuwa tunakuja na maeneo ambayo tunaona ni kipaumbele na ndio maana wakati tunaanza wengi walikuwa wanafanya hii ya miaka 17 na 20, na karibu timu zetu zote na hata TFF tumekuwa na mashindano ya vijana wa miaka 17 na 20.
“Baada ya kukaa nazo kuangalia mahitaji ya mpira wa sasa tunasema hizi ni program za muda mfupi yaani leo ukizungumzia vijana wa miaka hiyo 17 na 20 ni mambo ya muda mfupi.
“Hata sisi na CAF wametambulisha sheria kwa somo la ndani kuangalia na maeneo ambayo tutayapa kipaumbele.
“Kwa hiyo kwa maana ya kuzisaidia klabu tumeona ni kukaa nao na kuwapa somo kama ambavyo mmekuwa mkiona idara ya ufundi ya TFF imekuwa inaendesha mafunzo mengi kwa makocha wa klabu za Ligi Kuu kuwaonyesha namna ambavyo wanatakiwa kwenda kutekeleza kwa kuwa na hizi timu za chini ya miaka 15 - kwa kuanzia, lakini ukweli ni kwamba tunatakiwa kuwa na timu za chini ya miaka 12 na 15 ambapo tukifika ndio tutakuwa tunaanza kuangalia mipango ya muda mrefu.
“Kwa hiyo hiyo ni changamoto- changamoto ya kwanza ni uelewa kwamba mpira mahitaji yake kwenye soka la vijana ni yapi na kama mnajua tumekuwa tunapiga hatua za hapahapa kwenye maeneo ya kutekeleza hii leseni ya klabu kwa miaka mingi mpaka pale ambapo tumeanza kuchukua hatua.”

Kidao anaongeza kuwa, “sasa kuna mabadiliko makubwa yameanza kujitokeza. Kwa hiyo kwangu kwanza klabu zinatakiwa kuanza kutambua kuwa na hizi timu za chini ya miaka 17 na 20, ni jambo kubwa kwa maana kwamba tayari wana sehemu ya kuanzia na baadaye wataendelea kuwa na hizi zingine za miaka 12 na 15 ambazo baadaye ndio zitakuwa zinakwenda kulisha hizi za juu za miaka 17 na 20.
“Tumekuja na njia hii kwanza ya kuelimisha klabu kuona umuhimu kwa mujibu wa leseni kuanzia kuwekeza chini kabisa. Tunapokea maoni kila klabu ikiongea itakuambia kuna changamoto ya fedha, lakini unawasikiliza kwa kuwa hata hizo timu za vijana zinatakiwa kuwa chini ya makocha waliokidhi vigezo.
“Lakini sio hivyo tu ni vitu ambavyo vinashirikiana ukiwa na programu ya vijana uwe na miundombinu mizuri kama ambavyo unaelewa nayo ipo kwenye hii leseni ya klabu, na ndio kama mnavyoona tumekuwa tukipambana na klabu itasaidia wao kuendesha hizo programu na zingine ambazo watakuja kuanza nazo na msimu ujao mtaona tutaweka mkazo sana.
“Hapo kati tulikuwa tunaweka sana mkazo kwa klabu zilizokuwa zinakwenda kushiriki kimataifa, lakini sasa tutatoka huko tutakuja kwenye Ligi Kuu pamoja na Ligi ya Championiship kwa sababu tunaamini huku kwenye Championiship ndio klabu za Ligi Kuu za baadaye.”
Kwa upande wake, Wane Mkisi, kocha mzoefu kuibua vipaji kwa vijana anayefanya kazi kwenye Kituo cha Magnet kinachojihusisha na kuzalisha vijana anasema changamoto kubwa kutokuwa na maendeleo stahiki ni timu zinazoshiriki Ligi Kuu kujikita kuvipa kipaumbele vikosi vinavyoshiriki ligi.
ITAENDELEA KESHO