Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RIPOTI MAALUM -2: Klabu 16 Bara mtihani soka la vijana

Ripoti Pict

Muktasari:

  • Kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara au Mashindano ya Kimataifa inatakiwa iwe na angalau, timu mbili za vijana ya kwanza kuanzia miaka 15-21 na 10-14.

JANA tulianza mfululizo wa makala maalumu juu ya ukiukwaji wa Kanuni ya Leseni za Klabu kuhusiana na timu za vijana tukaona chanzo kikuu cha kukiukwa kwake katika utekelezaji huo.

Tuliona pia wasiwasi uliopo kwa kukiukwa kwa utekelezaji huo unaoenda sambamba na Kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kifungu cha 26 ambacho kimeweka wazi kwamba: “Kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara au Mashindano ya Kimataifa inatakiwa iwe na angalau, timu mbili za vijana ya kwanza kuanzia miaka 15-21 na 10-14.”

Leo tunaendelea na mfululizo wa makala hizo, kuonyesha namna gani klabu hizo zinapata timu hiyo za vijana kwa mujibu wa kanuni hiyo ya CAF na jinsi klabu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zimefanikiwa kutekeleza kanuni hiyo.


1. AZAM FC

Azam FC ni timu pekee inayotimiza kanuni za CAF kwa kuwa na timu za vijana kuanzia miaka 10-14 na 15-21. Ina timu za U17 na U20, na ina programu maalumu ya vijana chini ya makocha wenye uzoefu. Kiongozi mmoja wa timu anasema; “Tunawapata vijana hawa kupitia vituo mbalimbali vya soka na wengine tunawakuza wenyewe.”


2. COASTAL UNION

Klabu hii kutoka Tanga ina timu mbili za vijana, U20 na U17 zote zikishiriki michuano ya Ligi ya vijana. Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Omary Ayoub anasema timu yao katika kuwapata wachezaji hao wanaokwenda kuunda timu zao za vijana wanawapata  kupitia mashindano na vituo vya michezo mbalimbali vilivyopo mkoani humo na baadhi ya wachezaji wengine huja wenyewe kujaribu bahati yao kupitia mchujo maalum wa vijana.

RIP 01

“Sisi Coastal Union kama nilivyosema awali tuna timu mbili za vijana na tunachofanya katika kuwapata wachezaji hawa, huwa tunazialika timu mbalimbali za vijana hapa mkoani Tanga, watacheza mashindano mafupi na hapo makocha wetu wenye uzoefu na waliokidhi vigezo vyote vinavyohitajika na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanachagua wale wanaowaona wanatufaa, tukiona huyu anatufaa tutamuita na kumtaka atuletee nyaraka zake zinazothibitisha umri wake,” alisema Ayoub.

“Tukimaliza mashindano hayo tunakuwa na kliniki nyingine ambayo hii sasa inasimamiwa na makocha wetu pia, kuna wale vijana ambao hawako kwenye timu wanajua soka na wametoka sehemu mbalimbali za jiji na hata nje na hawa wote ni wanafunzi wa shuleni, wanawapa mazoezi na kuangalia nani ana akili kubwa ya mpira na wao ni vilevile tukiona wanaotufaa tutawataka kufuata utaratibu uleule wa kuthibitisha umri wao kabla ya kuamua waende timu ipi.”


3. DODOMA JIJI

Kwa upande wa Klabu ya Dodoma Jiji wameweka wazi kwamba inamiliki timu moja pekee ya vijana wa chini ya miaka 20 ambayo ndio imeamua kuiendesha ikikwepa kuwa na timu nyingine za umri wa chini kwa miaka 17, 14, na 10 kutokana na ukosefu wa fedha.

Afisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo Fortunatus Johnson anasema kwamba, mchakato wa kuwapata wachezaji hao huwa wanaokwenda kuunda timu ya U20 wametoa ajira ya muda maalum kwa maskauti wao ambao wanazunguka ndani ya mkoa huo kusaka vipaji shuleni na mitaani kisha kuwaleta kwenye timu yao.

“Ukisema uandae kliniki kuna gharama kiasi kwahiyo sisi Dodoma tumewapa kazi maalumu maskauti ambao wanapita shuleni kuangalia vipaji kwenye mashindano ya shule na wakimuona mchezaji fulani watatuletea na baada ya hapo makocha wetu watamuangalia akiwa hapa kwetu na wakiridhika naye tunaanza kazi ya kujiridhisha juu ya umri wake.

“Tukasema timu yetu hii iwe na wachezaji kutoka ndani ya mkoa huu wetu ili tuweze kupunguza gharama za malezi, lakini pia kama unavyojua wengi wao ni wanafunzi ambao watakuwa na muda wa kuendelea na masomo yao na baadaye kuja mazoezini.

“Tunatamani kuwa na timu za umri wa chini kidogo lakini kama nilivyosema shida kubwa ni rasilimali fedha ambayo imetulazimu kuwa na timu moja tu ya umri huo. Huko mbele hali ikiwa sawa tutatanua wigo zaidi.

“Changamoto kubwa tunayoipata ni udanganyifu wa umri kama unavyojua wachezaji hawa wanakuja na cheti cha kuzaliwa pekee kama kitu ambacho kinathibitisha umri wake na kuna wengine wanakuja bila hivyo vyeti mnaaza kusumbuana lakini kubwa na gumu ni namna ya kujua umri sahihi wa mchezaji.”

Aidha, Johnson anaweka wazi kuhusu suala la makocha na anasema: ”Tuna makocha waliokidhi vigezo. Awali tulikuwa na kocha Mohamed Muya ambaye sasa ndio huyu anayeifundisha timu ya Fountain Gate baada ya kuondoka timu yetu ya vijana utaona ni kocha wa viwango gani, tulimpa hili jukumu, lakini alipoondoka bado nafasi yake haijajazwa ila msaidizi wake kocha Omari Mohammed maarufu kwa jina la Omaroo ndiye anayekaimu nafasi hiyo na huyu ana leseni daraja B ambayo inakidhi kabisa viwango vya kufundisha vijana wetu kulingana na matakwa ya TFF.”


RIP 02

4. JKT TANZANIA

JKT Tanzania ambayo iko jijini Dar es Salaam kupitia Afisa Habari wake Jemedari Said anaweka wazi kuwa, kwa upande wa klabu hiyo wana vikosi viwili U17 na U20, huku wachezaji hao wakipatikana kwa njia ya mashindano ya kusaka vipaji kutoka maeneo mbali mbali.

Kama ilivyo kwa timu nyingine JKT pia inapata wachezaji wanaounda timu ya vijana kwa kuwafanyia majaribio kutoka katika vituo vya soka na maeneo mbalimbali huku wakiwa na vyeti vya kuzaliwa ili kuweza kufahamu umri kamili.

“Wachezaji kutoka maeneo tofauti wanakutana na kuchujwa kwa mashindano ambapo mwisho tunapata idadi kamili ya wachezaji ambao tutaona wanafaa kujiunga nasi, na tunaanza safari kuwajenga kama wachezaji wa JKT.

Suala la umri kwa wachezaji ni gumu kidogo ila kupata usahihi huwa wanakuja na vyeti vya kuzaliwa ambapo hapo tunafahamu umri wa kijana lakini pia wanakuja na wazazi hivyo ni rahisi pia kupata uhakika ingawa ni changamoto.”


5. KAGERA SUGAR

Hali ya Dodoma Jiji iko pia kwa Kagera Sugar ambako Katibu Mkuu wa timu hiyo Thabit Kandoro anasema, timu hiyo inamiliki kikosi kimoja tu ambacho ni U20 hali ambayo inatokana na ukosefu wa fedha.

Kandoro anasema njia wanayotumia kuwapata wachezaji hao ni kupitia timu mbalimbali za vijana kutoka mkoa huo na wengine kuletwa na watu binafsi wakiamini kwamba wanaweza kuwa sehemu ya timu hiyo kisha makocha wao wa vijana kuwafanyia mchujo.

“Tunafahamu umuhimu wa kuwa na timu za chini zaidi za vijana kama hizo za kuanzia miaka 10, lakini ukweli tuuseme kwamba shida ni fedha. Hizi timu kuzilea ni gharama kubwa ingawa manufaa yake ni makubwa.

“Timu yetu hii wachezaji wake tunawapata kupitia shuleni wanapokuwa na mashindano yao. Makocha wetu wanakwenda kuangalia vipaji sahihi, lakini wapo wengine wanaletwa na watu binafsi wakiona kama wanafaa na baada ya hapo makocha wetu watawaangalia kama wanafaa,” alisema kandoro.

“Tukishaona huyu mchezaji anafaa tutajiridhisha juu ya umri wake na akikidhi na hapo anakuwa mchezaji wetu akija kwa program ya vijana na ikimalizika anarudi kwao na hawa vijana wanafundishwa na makocha wenye vigezo sahihi kabisa kulingana na miongozo ya wakubwa TFF.


6. KMC

KMC ina timu mbili za vijana zile za U17 na U20, lakini haina timu za vijana kuanzia miaka 10-14. Ofisa Mtendaji Mkuu, Daniel Mwakasungula anasema kukosa uwezo wa kifedha umewalazimu timu yao kuwa na timu hizo tu.

Mwakasungula anasema kuwa, wachezaji wao wanaounda timu hizo wanatoka ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam hususan kwenye shule za wilaya yao ya Kinondoni kupitia mashindano mbalimbali ya soka ya shule.

RIP 03

“Vijana wanaokwenda kuzitumikia hizi timu wanatoka kwenye shule za Kinondoni makocha wetu huwa wanakwenda kwenye mashindano hayo na kutafuta vipaji na bahati nzuri kwetu kocha wa hizi timu ni mwalimu wa Shule ya Makumbusho ambaye ni Imani Mwalupetelo ambaye anaendelea kusoma kuchukua leseni daraja A ambayo inakidhi vigezo kabisa,” alisema Mwakasungula.


7. MASHUJAA

Mashujaa inamiliki timu tatu za vijana zile za U20, U17 na 10-14 lakini zikiwa kwenye vituo viwili tofauti.

Ofisa Habari wa timu hiyo Khamis Malyango anasema, U20 pekee ndio inayokaa mkoani Kigoma ambako ndio timu hiyo inatumia kama eneo lao la nyumbani huku timu zilizobaki zinakaa mkoani Dar es Salaam ambako hupata nafasi ya kupata mechi nyingi za kujifua za mashindano.

“Tuna timu tatu lakini hii ya chini ya miaka 20 inakaa Kigoma ambako ndio uwanja wetu wa nyumbani ulipo lakini hizi za chini kuanzia miaka 17 na nyingine za chini hadi kufika U10 ambazo hizi tumezianzisha mwaka jana hizi zipo Dar es Salaam kwenye kituo chetu cha Twalipo,” alisema Malyango.

“Kituo hiki ni kikubwa sana naweza kusema tunashindana na Azam, tumeona tuziache Dar es Salaam ili zipate nafasi kubwa ya kutumia kituo hicho na pia kupata mechi nyingi za vijana ambazo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni rahisi kuzipata.

“Wachezaji wote hawa wanapatikana kupitia kliniki maalumu tunazoendesha zinazosimamiwa na jeshi lakini wapo ambao wanatoka shuleni na wengine wanaletwa na wazazi wao ambao wanasikia sifa za kituo chetu na kuwaleta watoto wao.

RIP 04
RIP 04

“Timu zote hizi zinasimamiwa na makocha wenye uzoefu na vigezo zaidi ya vile ambavyo TFF imevielekeza. Makocha hawa ni Mohammed Seif ‘King’ anayesimamia timu ya U20 kule Kigoma na ana leseni daraja B na timu za hapa Twalipo zipo chini ya kocha Seif Hamza mwenye leseni C.

“Tuna mafanikio makubwa kwenye soka la vijana tumetoa wachezaji wengi wanaocheza timu za taifa na hata klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, lakini tunatengeneza hata waamuzi kuanzia chini mfano mzuri ni huyu Ramadhan Kayoko anayecheza mpaka mechi za kimataifa ametoka Twalipo tangu akiwa chini mdogo kabisa.


8. NAMUNGO

Namungo ya Lindi ina timu moja tu ya vijana ya U20 ambapo kupitia aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Omar Kaaya anasema wamelazimika kuwa na timu hiyo kutokana na gharama kubwa za uendeshaji.

Kaaya anasema katika kuwapata wachezaji hao wamekuwa wakialika wachezaji wanaojiona wana sifa ya kuitumikia timu hiyo kisha kuwafanyia mchujo unaoendeshwa na makocha wa timu hiyo.


9. PAMBA JIJI

Pamba Jiji ambayo msimu huu imerejea Ligi Kuu Bara baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja 2001, hadi sasa ina timu moja tu ya U20 lakini inaendelea na mchakato wa kuunda timu ya pili ya U17 ikikusanya wachezaji vijana 50 wakiendelea na mchujo wa kupata kikosi kimoja.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Pamba, Mohammed Bitegeko anasema timu hiyo ipo chini ya kocha mwenye sifa akiwa kuzifundisha timu kubwa zinazoshiriki Ligi Kuu Mathias Wandiba.

“Tulifanya kliniki ya siku tano kutafuta wachezaji wa U17 na U20 wakajitokeza vijana 374 lakini wamechaguliwa 25,” alisema Bitegeko.

“Kliniki hii iliongozwa na kocha mzoefu na mtaalamu wa vijana, Mathias Wandiba,” alisema.

“Wachezaji hawa tunawatoa kwenye shule na vituo mbalimbali, kama tunavyojua Mwanza ni mkoa mkubwa wenye vipaji kwahiyo kwakuwa ndio tumepanda tulianza na hii U20 lakini sasa tunajitanua kuwa na U17 na baada ya hapo tutazidi kufika huko chini kulingana na bajeti kwa kuwa soka la vijana kuliendesha linahitaji fedha nyingi.”


10. SIMBA

Kati ya timu kubwa katika ligi ni Simba ambayo kupitia meneja wake, Patrick Rweymamu anathibitisha kuwa, klabu hiyo ina timu mbili za vijana zinazoingia katika kundi moja la kanuni ya Leseni za Klabu ambazo ni U17 na U20.

Rweymamu anaweka wazi kuwa kila timu ina namna yake ya kuunda timu za vijana lakini kwa upande wa Simba yenyewe inakusanya vijana walio shuleni kupitia mashindano mbali mbali ili kuweza kupata vipaji vinavyojenga timu hizo.

“Huwa tunakuwa na mchujo baada ya kuwakusanya katika mikoa mbalimbali na baadaye tunapata vijana kadhaa kutokana na idadi tunayoitaka na hao ndio wanaoanza safari ya kuwa timu ya vijana ya Simba, ila tunafahamu umri wa halisi kutokana na vyeti vyao vya kuzaliwa.”


11. SINGIDA BLACK STARS

Singida Black Stars ambayo inashiriki Ligi Kuu Bara kupitia Ofisa Habari wake, Hussein Masanza, klabu hiyo ina timu mbili za vijana ambazo ni U17 na U20, ingawa kutokana na kanuni bado hawajatimiza kwani timu zote zinaingia katika kundi moja la vijana kuanzia miaka 15-21.

“Jinsi tunavyowapa vijana wanaounda timu hizi ni kwa kuwachukua katika vituo tofauti na kuwafanyia mchujo ili kupata vipaji halisi tutakavyo vichagua kuunda kikosi cha vijana, lakini njia tunayotumia kupata umri wa wachezaji kamili ni kupitia wazazi wanaowaleta pamoja na vyeti vya kuzaliwa.”


12. FOUNTAIN GATE

Fountain Gate ambayo nayo ipo Ligi Kuu kupitia Ofisa Habari wake, Issa Liponda anasema wao wana timu tatu za vijana za U20, U17 na U15 zilizogawanywa kwenye mikoa mitatu tofauti ya Morogoro, Dodoma na Mwanza.

Liponda anasema pia timu yao ina timu za vijana za U14 na ile U10 ambazo usimamizi wake upo sana kwenye shule zinazomilikiwa na Fountain Gate ambapo pia shule hizo ndio huzalisha wachezaji wote wanaokwenda kwenye timu zao za vijana.

“Hizo timu zote tunazo lakini tumezigawanya kwenye makundi tofauti ya usimamizi, tuna timu za U20, U17 na U15. Hizi tumezigawanya kwenye mikoa mitatu ambayo ni Dodoma,Morogoro na Mwanza lakini zote zinasimamiwa na Fountain Gate,” alisema Liponda.

“Hizi mbili za U14 na U10 kwa umri huo utaona kabisa hawa ni vijana wadogo zaidi wanaohitaji usimamizi, hizi tumeamua kuziacha shuleni ili zikae chini ya usimamizi wa walimu wao wanahitaji uangalizi zaidi.

RIP 05

“Wachezaji wote hawa wa timu za vijana tunawatoa kwenye shule zetu za Fountain Gate ambazo zipo mikoa mbalimbali na tunachofanya wakikua na na kuangalia vipaji vyao tunawasogeza juu na timu zote hizi zina makocha wenye leseni daraja B ambalo ni zaidi ya matakwa ya TFF.

“Kujiridhisha juu ya umri wao tunatumia vyeti vyao vya kuzaliwa kama ambavyo nilikueleza sisi wachezaji wengi tumewachukua kutoka shule zetu kwahiyo kwasasa tunatumia nyaraka hizo za serikali kujiridhisha juu ya umri wao.”


13. TABORA UNITED

Kwa upande wa kikosi hicho, Ofisa Habari wa Klabu hiyo,  Christina Mwagala anasema kuwa, kikosi chao kina timu moja ya vijana ingawa anaweka wazi kuwa hafahamu namna inavyoendeshwa na jinsi wanavyopatikana kwani hawako karibu.

“Siwezi kusema kuhusu changamoto moja kwa moja kwa sababu sina taarifa kuhusu timu yetu ya vijana hivyo hata makocha wao siwafahamu ila najua ipo na nimewahi kuisikia ila ipo mbali na timu kubwa ilipo.”


14. TANZANIA PRISONS

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Prisons Ajabu Kifukwe anasema mbali na kuwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara pia wana vikosi viwili vya timu za vijana zile za U20 na U17 lakini pia timu ya wanawake.

Anazungumzia mchakato wa kuwapata wachezaji wa timu za vijana Kifukwe akisema wanatumia majaribio maalumu ya kusaka vipaji ambayo huyandaa lakini pia makocha wao hupita kwenye mashindano ya shule.

“Tunatambua umuhimu wa kuwa na timu za vijana lakini pia kanuni inatutaka kuwa nazo, hapa Prisons tuna vikosi viwili vya timu za vijana ile ya U17 na U20 lakini pia tuna timu ya wasichana hizi timu zote zinasimamiwa na uongozi wa Prisons,” alisema Kifukwe.

“Namna ya kuwapata vijana tunatumia maskauti maalum ambao tumewapa kazi ya kutusakia vijana kutoka shuleni lakini pia kuna wakati tunaandaa mchujo maamlum wa vijana kwa kuwaita vijana wanaodhani wana umri stahiki ili waje wajaribu bahati yao,” alisema Kifukwe.

“Hizi timu zote zina makocha wao kila moja mfano hii U20 kocha wake ni Innocent Mwagombe, U17 iko chini ya kocha Dickson Oswald huyu alikuwa mchezaji wetu na akajiendeleza kwa ukocha na hii ya wanawake ipo chini ya Shaban Mtupa, hawa wote ni makocha wenye leseni stahiki kwa kuweza kuziendeleza hizi timu wakiwa na leseni B .”


15. YANGA

Yanga ni moja kati ya klabu inayomiliki vikosi viwili za timu za vijana chini ya miaka 17 na 20 ambapo Mkurugenzi  mpya wa Mashindano, Ibrahim Mohammed anasema, wanaleta mfumo mpya ambao utakwenda kuwapa matokeo makubwa na mazuri kwa klabu yao na taifa.

“Tumekuwa kwa muda mrefu na timu za vijana chini ya miaka 20 na 17 na mpaka sasa tunaendelea nazo lakini tunachofanya sasa ni kuziboresha zaidi ili ziweze kutuletea matunda tunayokusudia kama klabu na taifa kwa ujumla wake,” alisema Mohammed.

“Kwasasa tupo kwenye mashirikiano na klabu kubwa ya CSKA Moscow, nadhani mtakumbuka walikuja hapa nchini na wakazunguka mikoa mbalimbali kusimamia namna ya kupata vijana stahiki wanaokwenda kuunda hizi timu za vijana tunawapimaje kisasa juu ya vipaji vyao.

“Kama klabu tumeanza kuona matunda ya kuwa na timu za vijana. Tunao vijana ambao wamekuwa tegemeo kubwa kwa klabu yetu wako ambao tumewatoa nje ya nchi lakini wapo ambao wamekuwa tegemeo hata kwa timu za taifa.”

Clement Mzize ni zao la timu ya vijana ya Yanga akitamba na kikosi cha wakubwa katika Ligi Kuu Baram akiwindwa na klabu mbalimbali za ndani na nje ya Afrika, kwa dau linalotajwa kufikia Sh3 bilioni.  


16 KENGOLD

KenGold ambayo  inacheza msimu wake wa kwanza Ligi Kuu, kupitia Katibu Mkuu wake, Benson Mkocha anasema timu yao hadi sasa ina timu moja ya vijana chini ya miaka 20 ambayo walilazimika kuwa nayo kikakuni.

Mkocha anasema timu hiyo ya vijana ipo chini ya kocha Ratifu Masesa  ambaye pia yupo kwenye timu yao kubwa akihudumu kama mtunza vifaa wa timu ya Ligi Kuu na ana leseni daraja C ambapo wachezaji hao wanawapata shuleni kutoka ndani ya mkoa wao Mbeya.

“Sisi tuna timu moja tu ya U20 kama mnavyofahamu hii ipo kikanuni, hizo nyingine bado tunajikusanya ili tuangalie tunaanzia wapi ukizingatia kwamba tumepanda ligi msimu huu, nguvu yetu kubwa tunaiweka kwenye timu ya Ligi Kuu kisha hii ya vijana, na hii U20 bado hatuna kocha rasmi lakini tunamtumia mtunza vifaa wa timu kubwa Masesa akikaimu nafasi hiyo,” anasema Mkocha.

Inaendelea kesho