Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ramovic amekabidhiwa jezi na mchezo hajauelewa

Ramovic Pict
Ramovic Pict

Muktasari:

  • Kipande hicho kinapatikana katika ngoma hiyo kwenye dakika ya 1:57, huku wimbo mzima ambao amepewa shavu Ben Pol ukiwa na dakika 4:21 na ukiwa na verse tatu na ulitoka Novemba 26, 2015.

"NYUMBANI kwenu wewe ndiye mlezi na ilipaswa kulelewa, kama umekabidhiwa jezi na mchezo haujauelewa." Hiki ni kionjo kinachopatikana kwenye ngoma ya Mwanabongo Fleva, Shariff Thabit Ramadhan huku mitaani akijulikana zaidi kama Darassa inayokulikana kama 'Sikati Tamaa'.

Kipande hicho kinapatikana katika ngoma hiyo kwenye dakika ya 1:57, huku wimbo mzima ambao amepewa shavu Ben Pol ukiwa na dakika 4:21 na ukiwa na verse tatu na ulitoka Novemba 26, 2015.

Ngoma hiyo hadi leo hii ina miaka tisa kule YouTube tangu ipandishwe na ikiwa na watazamaji 827,214 hadi makala haya yanaandikwa.

Katika mkwaju huo, Darassa amegusia mambo mengi hasa yale ya mtaani juu ya shida, matatizo, njaa, umaskini na mambo mengine hasa kwenye ile mistari niliyoanza nayo pale juu.

Ram01

Kwa uchache kidogo katika maneno yale, Darassa anamzungumzia kijana ambaye licha ya umri wake mdogo lakini anajikuta yeye ndiye mwenye jukumu la kuitunza familia ambayo inamuangalia na ukweli wa mambo ni kama hali hiyo haiwezi.

Kile alichokisema kule Darassa kwa namna fulani ni kama kinamtokea Kocha mpya wa Yanga, Mjerumani Saed Ramovic kwa sasa tangu akabidhiwe mikoba ya kuinoa timu hiyo.

Ramovic ameingia Yanga wakati ambao hajui afanye kitu gani kwa ajili ya kuifanya timu hiyo irudi katika makali yake ya awali. Kwa sababu licha ya jitihada anazofanya mambo yanaonekana kuwa sivyo.

Japo ameisimamia Yanga katika mechi tatu pekee hadi sasa za mashindano rasmi lakini kwa kiasi kikubwa inaonyesha ni mwanzo mbaya tofauti na watangulizi wake wawili waliopita katika timu hiyo, Miguel Gamondi na Nasreddine Nabi.

Ram02

TANO ZA MWANZO KWA WOTE

Ramovic ndiye kocha aliyeingia na mguu mbaya zaidi kati ya makocha watatu walioingia kwenye timu hiyo. Amepoteza michezo mingi zaidi ya wenzake katika mechi tano za mwanzo.

Amefungwa mechi mbili kati ya tatu alizosimamia ikiwa ni tofauti na kile Nabi na Gamondi walichokutana nacho wakati wanaingia.

Amepoteza dhidi ya Al Hilal na MC Alger katika Ligi ya Mabingwa Afrika na ameshinda dhidi ya Namungo FC mchezo wa Ligi Kuu Bara.

Katika tano za mwanzo, Nabi alishinda nne na kupoteza moja, huku Gamondi akishinda nne na kupoteza moja ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba kwa penalti.


Ram03

KAA LA MOTO LIPO HAPA

Licha ya kuwa amekabidhiwa jezi na mchezo hauelewi lakini bado kuna ugumu zaidi kwa Ramovic aliyetangazwa kuwa kocha mkuu wa Yanga Novemba 15, mwaka huu kwa kuwa ana ratiba ngumu katika mechi zake zijazo.

Anatakiwa kupigana kwelikweli kwa kuwa ratiba ya timu hiyo imekaa vibaya na haimpi muda wa kujiandaa na hadi mwishoni mwa Desemba ataisimamia Yanga katika mechi tano ikiwemo ya Jumamosi hii dhidi TP Mazembe ya Ligi ya Mabingwa Afrika na michezo minne ya Ligi Kuu Bara.

Mbaya zaidi katika mechi hizo, kuna nafasi ya kupumzika kwa siku moja pekee kabla ya kutoka kituo kimoja kwenda kingine kwa ajili ya kusaka pointi tatu.


LAZIMA ATIBU HILI

Kocha huyo aliyetambulisha soka la 'Gusa Achia Twende Kwao' klabuni hapo ni lazima ahahakishe anairudisha timu hiyo katika kucheza soka la kuvutia ambalo walikuwa wanacheza chini ya makocha wawili waliopita.

Yanga ya Ramovic kila unapoitazama unaona wazi kabisa ipo tofauti na ile ya Nabi na Gamondi, kitu ambacho kinamlazimisha kocha huyo kuingia tena maabara yake ili aweze kutengeneza dawa ya tatizo hilo.

Uzuri ni kuwa anaweza kupata dawa hiyo katika dirisha dogo la usajili ambalo limebakisha saa chache kuanzia leo kabla ya kufunguliwa na hapo atakuwa na uwezo wa kuleta nyota watakaoingia kikosini moja kwa moja na kumsaidia kurudisha makali.


Ramovic Pict
Ramovic Pict

NABI, GAMONDI WAMEMCHONGEA NJIA NGUMU

Mafanikio waliyoyapata watangulizi wake, Nabi na Gamondi Yanga wakati wakiinoa timu hiyo ni njia ngumu sana ambayo wamemuachia kocha huyo aipite.

Kubeba mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la CRDB ni sehemu ya njia ngumu kwa kocha huo kuipita na kuifikia kwa kuwa kama atashindwa kuipa Yanga taji lolote kati ya hayo mawili lazima mashabiki watamshukia.

Pia ana kipengele kikubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuhakikisha timu hiyo inamaliza kwanza kwenye sehemu nzuri katika kundi lake kabla ya kufikia hatua ya nusu fainali ambayo viongozi wa timu hiyo wanaitaka.


MECHI ZIJAZO

Des 14 v Mazembe (A)

Des 19 v Mashujaa (H)

Des 22 v Prisons (H)

Des 25 v Dodoma (A)

Des 29 v Kagera (H)


Ram04

TANO ZA MWANZO ZA NABI

Yanga 0-1 Azam

JKT Tanzania 0-2 Yanga

Ruvu Shooting 2-3 Yanga

Yanga 3-2 Mwadui

Simba 0-1 Yanga


Ram05

TANO ZA MWANZO ZA GAMONDI

Yanga 2-0 Azam

Simba 0-0 Yanga (penalti 1-3)

Yanga 5-0 Zalan FC

Zalan FC 0-5 Yanga

Yanga 5-0 KMC