PUMZI YA MOTO: Stewards husaidia mashabiki wanaovamia mchezo

Muktasari:

  • Mbaya zaidi shabiki huyo alivamia eneo hilo mara mbili huku akisaidia na watu wa usalama wanaoitwa STEWARDS.

Kwenye mchezo wa Simba dhidi ya Mashujaa, Ijumaa ya Machi 15 mwaka huu uwanjani Azam Complex, shabiki mmoja anayedhaniwa kuwa wa Simba alivamia mchezo na kuonekana akifukua vitu kwenye nguzo ya goli la Mashujaa.

Mbaya zaidi shabiki huyo alivamia eneo hilo mara mbili huku akisaidia na watu wa usalama wanaoitwa STEWARDS.

Hawa ni askari maalumu wa kwenye viwanja vya mpira ambao kazi zao kuu ni kusaidia mambo yafuatayo:

i. Kusimamia mizunguko ya watazamaji uwanjani.

ii. Kuzuia mikusanyiko mikubwa katika maeneo madogo viwanjani.

iii. Kuepusha matukio ya hatari yasiyo ya lazima.

iv. Kutoa taarifa za dalili za matukio yanayoweza kuhatarisha usalama.

Uwepo wa STEWARDS kwenye viwanja vya mpira ni maagizo ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) katika kuongeza ufanisi wa usalama viwanjani.

Zamani majukumu yote haya yalikuwa chini ya polisi wa kawaida. Mojawapo ya sababu za Fifa kusisitiza matumizi ya STEWARDS viwanjani badala ya polisi wa kawaida ni kuepuka matumizi ya nguvu iliyopitiliza.

Mpira ni mchezo wa hisia inayoweza kugeuka na kuwa jazba, pale mambo yanapoelekea Kusini.

Kukabiliana na watu wenye hisia za namna hii kunahitaji ustahimilivu mkubwa unaoendana na mafunzo ambayo kimsingi polisi hawana. STEWADS hupewa mafunzo haya kwa miongozo ya Fifa na wanatarajiwa kusaidia kukabiliana na hali ya namna hiyo bila kuleta madhara.

Tanzania ni moja ya nchi ambazo vyama vyao vya soka vinakwenda kısasa sana. TFF haipo nyuma kwenye jambo lolote linalotokea duniani. Yakija mamboleo na yenyewe inayapokea kwa haraka.

Kwa hiyo Fifa walipoleta hili la STEWARDS, TFF nayo ikalileta Tanzania haraka sana na kuendesha mafunzo yaliyosimamiwa na wataalamu wa usalama wa Fifa.

Klabu zikapeleka watu wao watakaopata mafunzo ili wawe STEWARDS kwenye mechi zao. Hapo ndipo mambo yalipoharibika. Badala ya kupeleka watu wenye weledi wa kutosha vikapeleka mashabiki kindakindaki. Matokeo yake badala ya kuisaidia kusimamia usalama viwanjani, watu hawa wanakuwa sehemu ya wanaohatarisha usalama.

Kwenye mchezo wa Simba na Mashujaa, eneo ambalo yule mvamizi wa uwanjani alilitumia kuruka na kuingia uwanjani lilikuwa likilindwa na mmoja wa STEWARDS wa Simba waliokuwepo.

Sasa badala ya kumzuia, yeye ndiye alimsaidia kuingia ili akatoe vitu ambavyo waliamini vinawafanya wakose mabao. Huyu STEWARD angekuwa mweledi asingeruhusu ile kitu itokee maana ni moja ya majukumu yake, lakini kwa kuwa alikuwa shabiki akasahau majukumu yake ya msingi.

Kwa hiyo kama tunataka hawa watu wa kuitwa STEWARDS wafanye kazi yao kitaalamu, kwanza klabu zetu zibadilike. Ziachane na watu watakaofanya kazi kishabiki na badala yake wafanye kazi kiweledi.

Ipo siku yule mvamizi atamdhuru mmoja uwanjani na watu wote wanaosimamia mpira kuonekana hawana maana. Kwa sasa inaonekana kama jambo jepesi lakini ni zito na baya sana kwa ligi yetu ambayo inajipapatua kuwa moja ya ligi bora na za mfano baranı Afrika. Uhuru uliotolewa na TFF kwa klabu kuwa na STEWARDS wao kwa mechi zao za nyumbani unatumiwa vibaya. Nadhani sasa ianze kufikiriwa kwamba badala ya vilabu kuwa na STEWARDS wao, hiyo ibaki kwa uwanja husika.

Yaani kama ambavyo timu haziendi na nyavu zao viwanjani, au magoli yao, basi pia wasiende na STEWARDS, wawakute hukohuko kama ambavyo wanazikuta nyavu na mabao.

Kuwa na STEWARDS ambao ni mashabiki kutatuharibia taswira ya ligi yetu na kuonekana ya kihuni isiyofaa kuhusishwa na ustaarabu hata kidogo.