Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

PUMZI YA MOTO: Mastori ya Dabi ya Dar es Salaam Yanga vs Azam

Muktasari:

  • Ilikuwa mechi iliyojaa mbinu za makocha zaidi kuliko uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja, japo kulikuwa na nyakati fulani chache na majukwaa kukaanga chipsi.

MECHI namba mbili kwa ukubwa hapa nchini, Dar es Salaam Derby, imefanyika mwishoni mwa juma na wageni waliokuwa nyumbani, Azam FC, kushinda 1-0.

Ilikuwa mechi iliyojaa mbinu za makocha zaidi kuliko uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja, japo kulikuwa na nyakati fulani chache na majukwaa kukaanga chipsi.

Mechi ilionekana na matokeo yakajulikana, lakini hapa nataka kukuletea mastori makubwa nyuma ya mechi hii.


1. YANGA WALIJIDANGANYA

Awali, wenyeji wa mchezo huu, Yanga, walichagua Uwanja wa Mkapa kuchezea mechi hii.

Lakini Oktoba 25, wamiliki wa Uwanja wa Mkapa, serikali, wakaandika barua kwa wahusika wa mechi yaani bodi ya ligi, TFF, Yanga na Azam FC kuwataarifu kwamba uwanja huo hauwezi kupatikana siku ya mchezo kwa sababu hatua ambayo wakandarasi wapo hairuhusu kusimamisha ujenzi.

Azam FC inasemekana ilishauri kwamba kama ni hivyo mechi ikachezewe Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.

Bodi ya Ligi ikaliacha hilo kwa wenyeji wa mchezo ambao ni Yanga.

Itakumbukwa kuwa Yanga ilipaswa kucheza na Singida Black Stars Oktoba 30 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kwa hiyo ingekuwa rahisi kwao kubaki Zanzibar kuisubiri Azam FC.

Lakini Yanga inasemekana waliukataa ushauri wa Azam FC wa kubaki Zanzibar na kukawepo na mitazamo kwamba Azam FC ilikuwa inaogopa kuchezea Chamazi mchezo huo ili isifungiwe kwenye uwanja wake.

Rekodi zilikuwa zinaonyesha kwamba Azam FC hawakuwahi kupata angalau sare dhidi ya Yanga wakichezea Azam Complex.

Walikuwa wamekutana mara tatu na zote Yanga walishinda:


Azam FC 1-2 Yanga - 2018

Azam FC 0-1 Yanga - 2020

Azam FC 1-2 Yanga - 2022

Rekodi hizo kwa namna yoyote zingetosha kuwapa jeuri Yanga na kuamini kwamba Azam FC wako tayari kwa lolote kuhamisha mechi.

Na hii ndiyo sintofahamu ya uwanja iliyokuwapo kuelekea mechi hii. Kila siku kulikuwa na simulizi mpya.

Licha ya kuwa Uwanja wa New Amaan ni mkubwa kuliko Azam Complex na ungewapa Yanga mashabiki wengi zaidi, lakini Wananchi wakachagua mechi ichezwe Azam Complex na kilichowakuta ndiyo kama mlivyosikia.


2. DIARRA ANATESEKA SANA KWA AZAM FC

Bao la Gibril Sillah ni la 11 kwa Djigui Diarra kufungwa na Azam FC, tangu aje nchini mwaka 2021.

Diarra ambaye ni moja wa makipa bora Afrika, amekuwa akiteseka sana mbele ya Azam FC.

Amekutana na Azam FC mara 10 na kufungwa mabao hayo 11, huku Gibril Sillah akiwa mtesi wake mkuu.

Sillah amemfunga Diarra mabao matatu katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu, tangu raia huyo wa Gambia aje nchini mwaka 2023.

Alimfunga mechi zote mbili msimu uliopita na amemfunga tena mechi ya kwanza msimu huu.


Rekodi ya Diarra dhidi ya Azam FC

Mechi 10:

Ligi Kuu Bara - mabao 7

Ngao ya Jamii - mabao 2

Fainali CRDB - bao 1

3. DUBE KURUDIA YA 2021/22?

Prince Dube, mshambuliaji wa Yanga aliyetoka Azam FC, hajafunga bao hata moja na wala hajatoa pası ya bao katika mechi nane za Ligi Kuu alizocheza hadi sasa msimu huu.

Hii ni kinyume cha matarajio ya Yanga ambayo ilitumia nguvu kubwa sana kumpata raia huyo wa Zimbabwe.

Yanga wenyewe na mashabiki wengi wa soka waliamini kwamba Dube ataenda kuwa hatari zaidi akiwa Yanga, kuliko alivyokuwa Azam FC.

Lakini kitu ambacho watu wengi hawakukifikiria ni kwamba msimu wa 2021/22, ambao ulikuwa wa pili kwake hapa nchini, aliumaliza akiwa amefunga bao mmoja tu na kutoa pası mbili za mabao.

Kwa hiyo kwa mwenendo wa sasa, isije ikajirudia.


4. UDHIBITI MKALI

Moja ya sifa za Yanga na Simba ni mambo ya nje ya uwanja hasa ‘kuutibu’ uwanja watakaochezea mechi.

Mwina Kaduguda alipokuwa Mwenyekiti wa Simba alisema walipoenda Swaziland kucheza na Mbabane Swallows, yeye aliingia uwanjani usiku mmoja kabla ya mechi kwenda ‘kuutibu’ uwanja… na wakashinda kwa mabao mengi sana ile mechi.

Huo ndio utamaduni wa timu nyingi za Kiafrika.

Lakini kuelekea Dabi ya Dar es Salaam, udhibiti wa jambo hilo ulikuwa ni mkubwa.

Azam FC waliulinda uwanja wao kwa kuweka askari zaidi ya 50 kuuzunguka, huku wote wakifuatiliwa kwa kamera maalumu za usalama zilizouzunguka uwanja huo.

Na pia ndani ya eneo la kuchezea, waliwekwa mbwa (majibwa) 15 ili kuzuia mtu yeyote kuingia ndani.

Yaani endapo mtu angefanikiwa kuruka ukuta kwa ujanja wake au hata kwa msaada wa siri wa askari mmoja, basi akutane na majibwa akiingia ndani.

Hii iliwapa ugumu sana watu ambao walishinda kutwa nzima wakipitapita eneo la uwanja.

Wengine walikuwa wanaingia kwenye msikiti uliopo uwanjani pale, hata kama siyo muda wa ibada, na wengine walishinda chini ya mwembe mkubwa uliopo nje ya geti kuu la kuingilia uwanjani.

Waliondoka eneo lile jioni kabisa, na haikujulikana kama walirudi usiku au la.


5. CHAMAZI USALAMA MDOGO

Moja ya hoja za Azam FC kuhamisha mechi zao dhidi ya Simba au Yanga kutoka Chamazi, ni usalama.

Mashabiki wa Simba au Yanga wakiona timu yao inaelekea kupoteza mchezo huanza vurugu, hasa wanapokerwa na jambo fulani.

Kutokana na majukwaa ya uwanja huo kuwa karibu zaidi na sehemu ya kuchezea, imekuwa rahisi kwa mashabiki hao kutupa vitu uwanjani na kuwafikia moja kwa moja, wachezaji au waamuzi.

Kiusalama hili halijakaa sawa. Nadhani ni muda sahihi kwa mamlaka kuliona hili na kulichukulia hatua haraka.

hatua ni mbili tu

1. Wamiliki wa uwanja wafanye ukarabati wa kufunga uzio mrefu zaidi ya uliopo sasa.

2. Mechi kubwa (Azam FC dhidi ya Yanga au Simba) zihamishiwe kwenye viwanja vikubwa.


Hayo ndo mastori makubwa yaliyoizunguka Dar es Salaam Derby.