PUMZI YA MOTO: King Kikii aliinua kitambaa cheupe, sisi tunainua cheusi

Muktasari:
- Na rangi nyeusi imekuwa ikihusishwa na huzuni, kukataa tamaa na kukosa matumaini.
Sijui asili yake ni nini lakini rangi nyeupe imekuwa ikihusishwa na amani na upendo kwa miaka na mikaka.
Na rangi nyeusi imekuwa ikihusishwa na huzuni, kukataa tamaa na kukosa matumaini.
Ni lazima tu kuna sehemu ilianzia lakini siyo muhimu sana kuijua, kilicho muhimu ni tunachokifahamu sasa kuhusu rangi hizo.
Kupitia wimbo wake wa Kitambaa Cheupe, Boniface Kikumbi Mwanza Mpango maarufu kama Maestro King Kikii aka Bwana Mkubwa, alikuwa msanii aliyeziweka nafsi zetu katika furaha, upendo na amani katika maisha yake yote aliyoyaishi hapa nchini.
Wimbo huo ndiyo mfano halisi wa ninayoyasema.
Nainua mkono mama, kitambaa cheupeee
Ishara ya mapenzi mama, oh Zibollaa
King Kikii alikuwa anatufundisha hapa kwamba kitambaa cheupe alichokiinua na mkono wake ni ishara ya mapenzi/ upendo!
Huu ndiyo wimbo maarufu zaidi wa King Kikii, kama Michael Jackson na Thriller.
King Kiki aliutunga na kuuimba wimbo huu akiwa na bendi yake ya La Capitale maarufu kama Wazee Sugu.
Wimbo huu ndiyo alama ya msanii huyu mkongwe aliyeingia nchini miaka ya 1970 akitokea Zaire, nchi ambayo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Alizaliwa Januari Mosi, 1947 katika mji wa Lubumbashi, inakotoka TP Mazembe.
Kwa mara ya kwanza alikuja nchini Tanzania na bendi Orchestra Fouvette, akiwa na mwenzake Supreme Fred Ndala Kasheba, mwaka 1972.
Akafanya muziki, kisha akaondoka kwenda Zambia na mwaka 1977 alirudi jumla baada ya kufuatwa na mzee Paul (Chibangu Katayi) aliyekuwa akiifadhili bendi ya Orchestra Marquis du Zaire iliyokuwa ikifanya shughuli zake za muziki hapa nchini.
Akabaki hapa nchini hadi mauti yalipomkuta, Novemba 15, 2024. Amefariki akiwa raia wa Tanzania tangu mwaka 1997.
Zaidi ya bendi hiyo, King Kikii amefanya muziki na bendi nyingi sana hapa nchini, ikiwemo Orchestra Marquis Original.
Wimbo wake wa ‘Mimi Msafiri’ alioimba na bendi yake ya Orchestra Safari Sound aka Masantula, ni moja ya nyimbo zilizoleta mapinduzi ya Bongo Flava.
Wimbo huu ulirudiwa na Kwanza Unit, moja ya makundi ya kwanza kabisa hapa nchini kufanya muziki wa kizazi kipya.
Kupitia albamu yao ya Mkwanzania, Kwanza Unit waliutumia wimbo huu kuwafanya Watanzania waanze kuona muziki wa kizazi kipya siyo uhuni.
“Mimi msafiri bado niko njiani, sijui lini nitafika eeeh
Naulizia watu kule ninakokwenda, naambiwa bado ni mbali, sijui lini nitafika eeeh.”
Tukizungumzia Bongo Flava, Watanzania watakuwa wanalikumbuka vizuri sana lile tukio la kusaka vipaji la Bongo Star Search (BSS).
Ule wimbo wake wa utangulizi wa Katoto Kaanza Tambaa, ni kazi ya gwiji huyu.
King Kikii aliuimba wimbo huu akiwa na bendi ya Double O.
Ukipita pale Sinza kuna kituo cha daladala kinaitwa Kamanyola. Jina hili lilitokana na mtindo wa dansi alioubuni King Kikii, uliofahamika kama Kamanyola Bila Jasho, akiwa na Marquis.
Royo yake imeacha mwili lakini jina lake litabaki kwenye nyoyo za Watanzania kutokana urithi aliotuachia.
Kitambaa Cheupe ni jina maarufu sana kwenye mitaa ya Dar es Salaam, kutokana na biashara ya binti yake, Jessica.
Kuanzia Tabata, Sinza hadi Chamazi, kote huko kuna sehemu za starehe zenye jina hilo zikiendeshwa na binti huyo na kaka yake, Joseph Kikumbi.
Mwenzake Supreme Ndala Kasheba aliyekuja naye nchini kwa mara ya kwanza, alishafariki tangu mwaka 2003.
Kuja kwao pamoja na kuendelea kuishi pamoja kuliwafanya waanzishe bendi yao ya Zaita Muzika, iliyokuwa maarufu sana kwa nyimbo za Kesi ya Khanga na Dezo Dezo.
Baada ya Ndala Kasheba kufariki, King Kikii akabaki na bendi yake ya Wazee Sugu hadi alipoanza kuugua.
Aliugua kwa muda mrefu sana, kama alivyothibitisha binti yake, Jessica.
Kwamba hadi serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikampeleka India kwa matibabu, lakini haikuwa rizki, maradhi yalishafika mbali sana.
Kifo chake kimewatia simanzi Watanzania wa kizazi chake hadi hawa wa kizazi cha 2000, Gen Z.
Haihitaji maneno mengi kumfanya mtoto wa 2000 amfahamu, hata kama hakuwahi kumsikia kabla.
Mstari mmoja tu wa Kitambaa Cheupe, utamfanya mtoto huyo aseme, ‘Ah kumbe ndo huyu’ -- tayari keshamfahamu.
Sasa King Kikii ameshusha mikono yake yenye kitambaa cheupe -- ishara ya mapenzi, na kutuacha sisi tukiinua mikono yetu na kitambaa cheusi -- ishara ya msiba!
Kwaheri Bwana Mkubwa!