PUMZI YA MOTO: 2024 ulikuwa mwaka wa Fei Toto

Muktasari:
- Ameshinda mataji yote makubwa, kuanzia timu ya taifa hadi ngazi ya klabu.
LIONEL Messi anatajwa mmoja wa wachezaji bora wa muda wote duniani, kama siyo mchezaji bora wa muda wote.
Ameshinda mataji yote makubwa, kuanzia timu ya taifa hadi ngazi ya klabu.
Na ameshinda tuzo zote binafsi, ikiwemo Ballon d'Or ambayo aliigeuza kuwa yake binafsi.
Na mwaka 2012 unahesabiwa kama mwaka bora zaidi kwake kama mchezajji, katika miaka yake yote ambayo amecheza soka.
Ndani ya mwaka huo, yaani kuanzia Januari mosi hadi Desemba 31, Messi alivunja kila aina ya rekodi iliyokuwapo na kuweka yake.
Alifunga mabao 91, na kuvunja rekodi ya Gerd Mueller wa Bayern Munich aliyoweka mwaka 1974 kwa mabao 85.

Mabao hayo 91 ya Messi yalipatikana kwenye mechi 69 tu… hatari sana.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Feisal Salum 'Fei Toto', ndani ya mwaka 2024.
Mchezaji huyo ambaye pia ni maarufu kwa jina la Failasufi yaani 'hariri laini', au Zanzibar Finest yaani mchezaji bora zaidi wa Zanzibar, alikuwa na mwaka bora wa 2024 kuliko miaka yake yote aliyowahi kucheza soka.
Japo hakushinda taji na klabu yake, lakini hiyo haindoi ubora aliokuwa nao yeye binafsi kama mchezaji.
Takwimu za Feitoto mwaka 2024
Mechi 59
Mabao 22
Pasi za mabao 13
1. NGAZI YA KLABU
Fei Toto aliuanza mwaka 2024 kwa mchezo wa Dabi ya Mzizima uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, uliomalizika kwa sare ya 1-1.
Bao lake la kwanza mwaka 2024 lilikuja katika mchezo wake wa nne wa mwaka, Februari 25, dhidi ya Tanzania Prisons jijini Mbeya.
Bao hilo la penalti ya dakika ya 54 lilifungua njia kwa mabao mengine 19 yaliyofuata.
Penati hii pia ikafungua njia kwa penati zingine tano zilizofuata, nne zikiwa mabao na moja ikiota mbawa, dhidi ya Simba SC.
Machi 3 akafunga mabao mawili dhidi ya Dodoma Jiji katika ushindi wa 4-1 wa timu yake.
Lakini bao la heshima zaidi katika mabao yake yote lilikuwa lile la Machi 17 dhidi ya timu yake ya zamani, Yanga.
Hili lilikuwa bao la pili na la ushindi kwa timu yake iliyotoka kifua mbele kwa mabao 2-1.
Mashabiki wa Yanga walikuwa wakimsema vibaya sana Feisal Salum tangu aihame timu yao.
Kwa hiyo Feitoto akalitumia bao hilo kuwaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa yote yaliyotokea baina yao.

Takwimu za ngazi ya klabu 2024
Mechi 41
Mabao 20
Pası za mabao 13
A. Ligi Kuu
- Mechi 32
- Mabao 15
- assist 12
B. Kombe la Shirikisho la Benki ya CRDB
- Mechi 5
- Mabao 3
- Pasi za mabao 1
C. Ligi ya Mabingwa ya CAF
- Mechi 2
- Magoli 0
- Pasi za magoli 0
D. Kombe la Muungano
- Mechi 1
- Mabao 1
- Pasi za mabao 0
E. Ngao ya Jamii
- Mechi 2
- Mabao 2
- Pasi za Mabao 0
Feisal Salum amehusika kwenye mabao 27 ndani ya mwaka 24 katika ngazi ya klabu.
Takwimu hizi zinafanya kuwa mchezaji aliyehusika na mabao mengi zaidi ndani ya mwaka huo.
Tatu bora ya waliohusika na mabao mengi kwa mwaka 2024 (mabao + pasi za mabao) kwenye ligi kuu pekee.
1. Feisal Salum 27 (15+12)
2. Aziz Ki 21 (12+9)
3. Gibril Sillah 13 (8+5)
2. NGAZI YA TIMU YA TAIFA
Feisal alicheza mechi 18 za timu ya taifa ndani ya mwaka 2024.
Mechi hizi ni kuanzia za mashindano makubwa kama fainali za AFCON kule Ivory Coast na kufuzu Kombe la Dunia 2026 na AFCON 2025.
Ndani ya mwaka huu Feitoto alifunga mabao mawili, dhidi ya Guinea na dhidi ya Ethiopia.
Mabao haya ni mengi zaidi kwake ndani ya mwaka mmoja, kwani tangu aanze kuchezea timu ya taifa amemfunga jumla ya mabao manne tu.
Mabao ya Feitoto akiwa Stars
17 Novemba 2020
Tanzania 1-1 Tunisia - kufuzu AFCON 2021
7 Septemba 2021
Tanzania 3-2 Madagascar - Kufuzu Kombe la Dunia 2022
10 Septemba 2024
Guinea 1-2 Tanzania - Kufuzu AFCON 2025
16 Novemba 2024
Ethiopia 0-2 Tanzania - Kufuzu AFCON 2025
Takwimu zilizotumika hapa ni mabao na Pasi za mabao pekee, lakini Feitoto alikuwa na vitu vingi na vikubwa zaidi ya hivyo.
Kwa mfano bao la pili dhidi ya Guinea kule ugenini lililofungwa na Mudathir Yahya, lilitokana na nafasi kubwa (Big Chance) ambayo ilitengenezwa na Feisal Salum.

Bao la Saimon Msuva dhidi ya Guinea kwenye kufuzu AFCON 2025 kule Morocco, lilitokana na nafasi kubwa iliyotengenezwa na Feisal Salum kwa Mudathir Yahya.
Zaidi tu ya mafanikio ya uwnajani, Feisal Salum amekuwa mchezaji aliyezungumzwa zaidi hapa nchini ndani ya mwaka 2024.
Habari yoyote iliyomhusu Feisal Salum ilivutia watu wengi, ikiwa kwenye redio, magazetini na hata kwenye mitandao ya jamii.
Feisal Salum amehusishwa na timu kubwa za ndani na nje ya mwaka, kuliko wachezaji wote hapa nchini, ndani ya mwaka 2024.
Kocha wa Wydad Casablanca, Rhulani Mokwena, alikiri waziwazi kwamba yeye ni shabiki mkubwa wa mchezaji huyo na anatamani sana kufanya naye kazı siku moja.
Kocha huyo wa zamani wa Mamelodi Sundowns, aliyasema hayo alipokutana na mchezaji huyo nchini Morocco wakati Azam FC ilipokuwa kwenye maandalizi ya msimu mpya.
Kocha wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi, amefanya kila kitu kumpata mchezaji huyo huku timu yake ikituma barua mara mbili ya kuomba kufungua maongezi na Azam FC kumhusu mchezaji huyo, lakini Azam FC haikujibu hata moja.
Lakini hapa ndani Feitoto amekuwa akihusishwa na Simba kila uchao.
Kila akikutana na waandishi wa habari, swali la kwanza ni hilo.
Ama kwa hakika mwaka 2024 ulikuwa bora sana kwa Feisal Salum Abdallah.