Prime
Prince Dube namba zinambeba

Muktasari:
- Nyota huyo amejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu ili kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji linaloundwa na Clement Mzize na Kennedy Musonda.
PRINCE Dube ni jina linalotajwa zaidi kwa nyota wanaocheza eneo la ushambuliaji na utajwaji wake sio kwa uzuri liicha ya namba yake kumbeba.
Nyota huyo amejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu ili kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji linaloundwa na Clement Mzize na Kennedy Musonda.
Ujio wake ndani ya kikosi hicho ulitajwa kuwa utaondoa changamoto ya kukosa mbadala wa Fiston Mayele ambaye aliondoka kikosini humo baada ya kupata dili la kwenda kuitumikia Pyramids FC.
Nyota huyo alijiunga naYanga akitokea Azam FC ukiwa ni usajili ulioteka hisia za mashabiki wengi kutokana na vuta nikuvute iliyokuwepo baina ya mchezaji huyo na waajiri wake wa zamani.
Licha ya mshambuliaji huyo kuto kutajwa kwa ubora tangu amejiunga na Yanga tayari amefanya mambo mazuri na kumfanya akaandika rekodi mpya tofauti na misimu yake mingine nne nyuma akiwa na Azam FC.
Ubora wake msimu huu akiwa na Yanga, tayari amehusika katika mabao 16 kati ya 50 yaliyofungwa na kikosi hicho kizima kwenye Ligi Kuu Bara ambapo amefunga tisa na kutoa ‘asisti’ saba huku akipitwa bao moja tu na Clement Mzize wa timu hiyo mwenye mabao 10.

Kwenye kikosi cha Yanga, Dube anashika nafasi ya pili akiongozwa na Mzize katika ufungaji wa mabao yeye amefunga mabao tisa huku kinara akiwa na mabao 10, akiwaacha Jean Ahoua, Lionel Ateba na Elvis Rupia wote wakiingia kambani mara saba.
Msimu huu umekuwa bora zaidi kwa Dube tofauti na alivyokuwa Azam FC ambapo msimu wake wa kwanza ndani ya kikosi hicho 2020/21 alifunga mabao 14 amebakiza mabao saba kufikia rekodi yake lakini tayari amevuka rekodi hiyo kwa kuisaiodia Yanga kuhusika kwenye mabao 15 hadi sasa.
Akiwa na Azam amecheza misimu mitatu na nusu amefunga mabao 34 kwenye mechi 54, Msimu wa 2020-2021 alifunga mabao 14, 2021-21 aliingia kambani mara moja kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyokuwa yamemuweka nje kwa muda, 2022-23 alifunga mabao 12 na msimu wake wa mwisho kuitumikia Azam FC 2023-24 alicheza miezi sita na kufanikiwa kufunga mabao saba.
HAT-TRICK 1
Katika mabao nane aliyofunga nyota huyo akiwa na Yanga tayari ana ‘hat-trick’ moja ambayo ndio ilikuwa ya kwanza kwa msimu huu ambao hadi sasa una 'hat-trick' mbili zote kutoka ndani ya kikosi hicho Dube amefunga mabao hayo matatu kwenye ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mashujaa mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.
Kwenye mchezo huo Dube alifunga mabo Magoli yote matatu dakika ya nane baada ya pasi safi kutoka kwa Pacome Zouzoua, dakika ya 22 alikwamisha mpira kwa kichwa baada ya piga nikupige langoni mwa Mashujaa na bao la tatu lilifungwa dakika ya 53 huku mabao ya Mashujaa jakifungwa na Idrisa Stambuli na David Ulomi.
Hat-trick nyingine ambayo ni ya pili ligi kuu imefungwa na Aziz Ki ambaye alifunga kwenye mchezo dhidi ya KMC kwenye uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 6-1.

KIMATAIFA
Dube akiwa na Yanga kwenye mechi za kimataifa amecheza sita akitumika kwa dakika 396 amefunga bao moja na kutoa pasi moja iliyozaa bao.
Mechi alizocheza ni dhidi ya Al Hilal nyumbani alitumika kwa dakika 90 timu yake ikikubali kichapo cha mabao 2-0, MC Alger ugenini alicheza dakika saba Yanga ililala kwa mabao 2-0, TP Mazembe ugenini walipata sare ya bao 1-1 ambalo alifunga yeye akitumika kwa dakika 29.
Mechi nyingine ni dhidi ya TP Mazembe nyumbani timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 akitoa asisti moja alicheza dakika zote 90, Al Hilal ugenini alicheza dakika 90 Yanga ilishinda bao 1-0 na alitumika kwa dakika 90 dhidi ya MC Alger wakitoka suluhu.
MECHI ZA LIGI ZILIZOBAKI
Mashujaa vs Yanga
Pamba vs Yanga
Yanga vs Simba
Tabora United vs Yanga
Yanga vs Coastal Union
Azam FC vs Yanga
Fountain Gate vs Yanga
Yanga vs Namungo
Tanzania Prisons vs Yanga
Yanga vs Dodoma Jiji

WASIFU
Jina: Prince Dube
Kuzaliwa: Feb 17, 1997
Mahali: Harare
Nchi: Zimbabwe
Urefu: 1.83 mita
Nafasi: Mshambuliaji
Klabu: Yanga
Jezi: Namba 29
Alikopita: Highlanders, SuperSport Utd, Black Leopards, Azam FC
14 Mabao aliyofunga Dube msimu wake wa kwanza kucheza Ligi Kuu Bara 2020-2021
42 Jumla ya mabao yote aliyofunga mshambuliaji huyo katika misimu mitano aliyocheza Ligi Kuu Bara
16 Idadi ya mabao aliyohusika nayo Dube msimu huu akiwa na Yanga akifunga 9 na kuasisti saba.