Pasua kichwa ya Kim Poulsen iko hapa

NILIKUWA mmoja wa mashabiki wa soka wa Tanzania waliotaka sana kuona kocha Kim Poulsen akirejea kufundisha Timu ya Taifa ya Soka (Taifa Stars). Nilivutiwa sana na aina ya uchezaji wa timu yetu wakati yeye akiwa kocha.

Katika mambo haya ya ukocha, mara nyingi mara ya pili huwa haifanani na mara ya kwanza. Tazama Jose Mourinho na Chelsea yake. Tazama Luiz Felipe Scolari na Brazil. Kuna mifano mingi sana ya kueleza kuhusu hofu hii lakini mara zote nikiamini kwamba yeye hakuwa amemaliza kazi yake.

Nilitiwa nguvu pia na mazungumzo niliyokuwa nimefanya na mmoja wa wachezaji waandamizi wa Taifa Stars aliyenieleza kinaga ubaga kwamba miongoni mwa makocha wa kigeni waliokuja Tanzania katika miaka ya karibuni, hakuna aliyekuwa na uwezo wa kumfikia raia huyo wa Denmark.

Nakumbuka kwamba tamaa yangu hiyo haikuishia moyoni mwangu pekee. Kuna siku nilipata bahati ya kukutana na mmoja wa viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na nilitumia fursa hiyo kuuliza kuhusu Kim. Wakati huo tayari taarifa za aliyekuwa mwalimu wa Stars, Emmanuel Amunike, kuondoka zilikuwa zimetapakaa.

Kila nikitazama soka la Tanzania kwa sasa, kuna nyakati napata matumaini na kuna nyakati fadhaa inaniingia. Mimi ni mtu mzima na nimeona mengi katika soka hapa kwetu. Nimeishi, huko nyuma, katika nyakati ambazo mechi ya Ligi Daraja la Tatu ilikuwa inajaza watu uwanjani na vipaji vilikuwa vinatosha.

Nimekulia katika nyakati ambazo waliokuja kuwa nyota wakubwa wa baadaye katika soka tulikuwa tunasoma nao au kuwaona katika mashindano kama ya UMISETA.

Nakumbuka wakati nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Forodhani hapa Dar es Salaam, nilikuwa naondoka shuleni kwenda kuwahi kuona mechi za timu ya sekondari ya Al Harramain iliyokuwa imesheheni viungo kama vile Waziri ‘Mendieta’ Mahadhi na Shekhan Rashid.

Nimemuona pia Salvatory ‘Dokta’ Edward akicheza kandanda la kiwango cha juu sana akiwa mwanafunzi wa sekondari ya Kibasila hapa Dar es Salaam. Nimeona masupastaa wengi wakiwa wanafunzi au mitaani.

Nilimjua Kally Ongalla wakati akiwa Abajalo ya Sinza na niliwajua wengi wengine wakiwa wachezaji wa timu za mitaani walikoishi. Bado ninaishi mtaani na kila nikienda kutazama mpira mtaani kwangu, sioni tena mchezaji anayenisisimua.

Labda nakaa kusiko na vipaji.

Nikienda kwenye mashindano ya shule, na nimehudhuria mashindano mengi tu, naona kuna vipaji lakini kuna jambo moja silioni njaa ya mchezaji husika kutaka kwenda mbali na mchezo huo na kufikia mafanikio ya kiwango cha juu.

Katika Ligi Kuu ya Tanzania, timu kubwa zimeruhusiwa kusajili zaidi kutoka nje ya nchi na kwa sababu ya fedha zinazozidi kuingia katika mchezo kupitia wadhamini kama Azam Media, nina wasiwasi kwamba timu zitazidi kutazama nje kutazama vipaji kuliko kuangalia ndani.

Ni rahisi kusajili nje kuliko ndani kwa sababu nje ni kukubwa zaidi. Soko la kusajili liko katika mataifa mengine ambayo kwa sababu za kihistoria na kitamaduni, zina wachezaji wazuri na walio tayari kutoka walipo kwenda kokote wanakohitajika.

Natazama timu kama Simba. Kama John Bocco asipocheza, washambuliaji waliobakia wote watatoka nje ya Tanzania. Wamejaribiwa vijana kadhaa kuchukua nafasi yake hata kwa miaka michache lakini naona wanachemsha mapema. Wanaondoka.

Yanga nako hali ni ileile. Mtanzania pekee anayeweza kushindania namba na wageni ni Ditram Nchimbi pekee. Deus Kaseke anapambana lakini kwangu yeye si mshambuliaji bali ni kiungo.

Labda tuna walinda milango wa kutosha. Hilo ndilo eneo pekee ambalo nalitazama na kusema angalau hakuna tatizo. Katika maeneo mengine tofauti, nadhani ziko changamoto za wachezaji ambazo Poulsen anatakiwa kuziangalia vizuri.

Tunapataje viungo wa ulinzi wa kushindania namba na akina Mukoko Tonombe na Taddeo Lwanga? Tunapataje washambuliaji wa kushindana na kina Benard Morrison, Prince Dube, Yacouba Sogne na Meddie Kagere?

Tunatengeneza vipi walinzi wa kushindana na kina Lamine Moro, Pascal Wawa na Onyango? Tunatengeneza vipi kina Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Nadir Cannavaro na wengine wa aina hiyo katika miaka hii michache?

Mpira uchezwe wapi? Wavu wetu wa kuvua wachezaji wapya na wazuri utegwe wapi au upelekwe kuvua sehemu gani? Kama mpira si muhimu tena shuleni, ni wapi hasa tutawaona na kuwatambua nyota wetu wa baadaye?

Nataka kuamini kwamba Poulsen atatusaidia kwenye kutafuta majibu ya maswali haya. Na ni imani yangu kubwa kwamba hii ndiyo itakuwa kazi yake kubwa kuliko kufundisha mpira uwanjani. Uwezo wake wa kufundisha wachezaji utaonekana vizuri endapo atapata wachezaji anaowahitaji.

Jose Mourinho alipata kutamka kwamba ili mtu ale yai zuri la kukaanga, ni muhimu sana kwamba akapewa mayai mazuri, mafuta mazuri na kikaangio kizuri. Kama mpishi ni mzuri, chungu kizuri lakini mayai yameoza, upishi wake utatiliwa shaka.

Kim Poulsen ana kazi kubwa ya kutufanya tupende tena Taifa Stars kama ilivyokuwa mara yake ya kwanza lakini pia tutengeneze mtambo wa kuibua vipaji kila uchao.

Najua hii haitakuwa kazi yake pekee. Lakini, walau yeye ana tochi inayoweza kutuelekeza wapi pa kwenda na lipi la kufanya.


IMEANDIKWA NA EZEKIEL KAMWAGA