Pablo tatizo lilianzia hapa!

MABOSI wa Simba wapo sokoni kutafuta kocha mpya atakayechukua mikoba ya Pablo Franco aliyesitishiwa kibarua chake baada ya kushindwa kufanya vizuri na timu hiyo kwenye mashindano matatu makubwa.
Simba ilifanya vizuri misimu mitatu iliyopita na msimu huu imekuwa ovyo na sasa baada ya kuondoka kwa Pablo, inahitaji kocha mpya ili kupata muda wa kufanya usajili pamoja na maandalizi ya msimu.
Makala haya yanakuletea sababu tano za Pablo kutimuliwa Simba akiwa ameichukua msimu ukiwa katikati lakini viongozi wakaona safari yake iishie hapo kutokana na mwenendo wake kwenye chama lao.
KUPOTEZA MATAJI
Simba ilijiwekea malengo ya kutetea mataji yao ya Ndani msimu huu ikiwamo lile la Ligi Kuu Bara na Yanga ndio inapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo.
Pia imepoteza Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC), baada ya kufungwa na Yanga bao 1-0 katika mechi ya nusu fainali Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza wiki moja iliyopita.
Pia lishindwa kufikia malengo yao msimu huu kwenye kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa na Orlando Pirates katika hatua ya mikwaju ya penalti baada ya mechi zote mbili kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Hata hivyo, msimu huu imeambulia taji moja pekee hadi sasa (Kombe la Mapinduzi) chini ya Kocha Pablo.
DILI ZAKE
Pablo wakati anaendelea na mashindano hayo matatu makubwa na Simba msimu huu alikuwa anakutana na ofa nyingi kutoka kwenye timu mbalimba ndani ya Afrika pamoja na Ulaya.
Miongoni mwa timu zilizoweka mezani ofa ya kumtaka Pablo zipo, Horoya ya Guinea, Orlando Pirates na Amazulu zote za Afrika Kusini pamoja na Raja Casablanca ya Morocco.
Mabosi wa Simba hawakuonekana kuvutiwa na jambo hilo kwani waliamini Pablo anakosa utulivu wa akili kukiongoza kikosi na kutokana na mawasiliano hayo kutoka kwenye hizo timu zinazomuhitaji.
MAELEWANO MAZURI
Wiki kadhaa nyuma kabla ya Pablo kuonyeshwa mlango wa kutokea kulikuwa kuna mambo yanaendelea ndani ya timu hadi kusababisha kutokuwepo na maelewano mazuri kati yake na mmoja wa kiongozi wa juu.
Kuna vitu Pablo alikuwa anahitaji kama ambavyo ilikuwa kwa kigogo huyo na kila mmoja alikuwa anavutia upande wake jambo ambalo liliwafanya kutokuwa kwenye maelewano mazuri.
Hadi Pablo anaingia kwenye mechi yake ya mwisho ya kimashindano dhidi ya Yanga kulikuwa hakuna utulivu kati yake na kigogo huyo na jambo hili lilichangia kuondoka kwake haswa mara baada ya kupoteza mchezo huo mkubwa nchini.
MAPROO
Kikosi cha Simba kilikuwa na wachezaji wengi majeruhi tena wa mara kwa mara na kushindwa kuwepo na nyota wote wenye utimamu wa mwili katika michezo mfululizo.
Jambo hilo liliwakera mabosi wa Simba kiasi kuona kuna mapungufu hadi kwenye eneo la kocha wa viungo, Daniel De Castro aliyependekezwa na Pablo, walioamua kuachana nae.
Pablo alionekana kutokuwa katika hali nzuri na baadhi ya maproo wa Simba ikiwemo, Benard Morrison aliyeondoka na aliweka wazi kuna wachezaji anawaamini lakini wanashindwa kuonyesha viwango bora.
PRESHA YA UONGOZI
Maamuzi hayo ya kuachana na Pablo yalichangiwa na kigogo mmoja mwenye nguvu ya maamuzi Simba kutokana na kile alichoeleza kushindwa kufanya vizuri msimu huu kocha huyo amechangia.
Ndio maana maamuzi hayo ya kuachana na Pablo kuna baadhi ya mabosi ndani ya Simba wamekuwa hawakubaliana nayo huku wakiamini kocha huo alistahili kupewa muda zaidi wa kuifundisha Simba.
Ushawishi na nguvu aliyokuwa nayo kigogo huyo yaligusa moja kwa moja hatma ya Pablo hadi kukutana na barua ya kusitishia mkataba wake wa miaka miwili aliyokuwa ametumikia si zaidi ya mwaka mmoja.
REKODI
Tangu Pablo alipotua nchini Novemba mwaka jana, ameiongoza Simba katika mechi 39 zikiwamo 20 za Ligi Kuu Bara na kushinda michezo 22, sare 10 na kupoteza saba kwa kufunga mabao 66 na kufungwa 24, huku akibeba Kombe la Mapinduzi na kuifikisha Simba nusu fainali ya ASFC na kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ametemwa akiwa ameshalipoteza taji la ASFC na huku timu ikiwa na dalili zote za kulitema taji la Ligi Kuu Bara.