Prime
ONE MAN SHOW! Hawa jamaa ni mastelingi wa msimu kwenye Ligi Kuu England

Muktasari:
- Liverpool imefunga mabao 64 kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Kwa maana ya Mo Salah kuhusika kwenye mabao 41, hiyo ina maana, wachezaji wengine waliobaki kwenye kikosi hicho cha Arne Slot, wamehusika kwenye mabao 23 tu. Ni rahisi tu kucheza, Mo Salah anaibeba Liverpool kwenye mabega yake msimu huu.
LONDON, ENGLAND: SUPASTAA, Mohamed Salah kila anachoweka mezani msimu huu kinauzika. Kwenye Ligi Kuu England, mkali huyo wa kimataifa wa Misri, amehusika kwenye mabao 41 kwa maana ya kufunga na kuasisti katika mechi ameitumikia klabu yake ya Liverpool.
Liverpool imefunga mabao 64 kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Kwa maana ya Mo Salah kuhusika kwenye mabao 41, hiyo ina maana, wachezaji wengine waliobaki kwenye kikosi hicho cha Arne Slot, wamehusika kwenye mabao 23 tu. Ni rahisi tu kucheza, Mo Salah anaibeba Liverpool kwenye mabega yake msimu huu.
Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Salah kuibeba Liverpool kwenye mabega yake, alifanya hivyo pia kwenye msimu wa 2017/18.
Straika Erling Haaland alifanya hivyo kwenye msimu wake wa kwanza Ligi Kuu England, wakati alipojiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Manchester City. Makala haya yanahusu viwango bora kabisa vya mchezaji mmoja kwa msimu mmoja kwenye Ligi Kuu England.

10) Mohamed Salah 2017/18
Mechi: 36
Mabao: 32
Asisti: 11
Mo Salah aliwahi kucheza kwenye Ligi Kuu England kabla ya kujiunga na Liverpool mwaka 2017, lakini ni watu wachache sana wanakumbuka kwamba mkali huyo alicheza dakika 530 huko Chelsea. Kiwango chake cha Stamford Bridge hakikuwa vizuri hivyo akaenda Italia ambako alikuwa moto kwenye timu za Fiorentina na AS Roma na hivyo Liverpool wakavutiwa na kumrudisha kwenye Ligi Kuu England.
Msimu wake wa kwanza tu Liverpool, alivunja rekodi ya kufunga mabao 32 kwenye msimu wa mechi 38 za Ligi Kuu. Kwa msimu huo, aliasisti mara 11 pia na hivyo kuwa amehusika kwenye mabao 43 kati ya mabao 84.

9) Gareth Bale – 2012/13
Mechi: 33
Mabao: 21
Asisti: 9
Gareth Bale alikuwa kwenye kiwango bora sana Tottenham Hotspur kabla ya kubamba dili la maana kabisa kwenda kujiunga na Real Madrid. Msimu wa 2012/13 hakuipa Spurs ubingwa wa Ligi Kuu England, lakini winga huyo alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Msimu wa ligi hiyo, alinyakua pia tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa soka la kulipwa, kinda bora na mchezaji bora wa waandishi wa habari za michezo. Bale aliibeba Spurs kwenye mabega yake msimu huu na kufanikiwa kumaliza kwenye nafasi ya tano katika msimamo, akifunga mabao 21 na kuasisti mara tisa. Spurs ilishinda mechi nyingi sana msimu huo kwa mabao ya Bale.

8) Kevin De Bruyne – 2019/20
Mechi: 35
Mabao: 13
Asisti: 20
Wachezaji wengi walikaribia kuvunja rekodi ya Thierry Henry kwenye asisti tangu ilipowekwa 2003. Mwaka huo, fowadi huyo Mfaransa, aliasisti mabao 20. Mesut Ozil alikaribia kufikia rekodi hiyo katika msimu wa 2015/16 alipoasisti mara 19; ambapo Mjerumani huyo aliasisti mara 16 kabla ya mwaka mpya, lakini alishindwa kuvunja rekodi. Manchester City ilishinda mataji matano ya Ligi Kuu England katika miaka sita, ambapo ilibeba pia kwenye msimu wa 2011/12 na 2013/14, lakini kwenye msimu matata wa Kevin De Bruyne kwenye kikosi hicho, 2019/20, miamba hiyo ya Etihad ilishindwa kubeba ubingwa wa ligi. Lakini, ni msimu huo ambao alifunga mabao 13 na kuasisti mara 20, akiibeba Man City kwenye mabega yake.

7) Dennis Bergkamp – 1997/98
Mechi: 28
Mabao: 16
Asisti: 11
Mdachi huyo mwoga wa kupanda ndege alijiunga na Arsenal mwaka 1995 chini ya kocha Bruce Rioch. Nyakati zake alizokuwa Inter Milan huko Italia hazikuwa zenye mafanikio makubwa, lakini Mdachi huyo alikuwa moto kwelikweli Arsenal. Hakuna ubishi, Bergkamp alikuwa mmoja wa wachezaji wenye vipaji vikubwa sana waliopata kutokea kwenye Ligi Kuu England na msimu wa 1997/98, aliibeba Arsenal kwenye mabega yake na kuipa taji lao la kwanza la Ligi Kuu England. Bergkamp alikuwa akiwafanya mabeki wa timu pinzani kwa kadri anavyotaka yeye, huku alikuwa staa mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na hakika miguu yake ilikuwa na uchawi fulani. Msimu huo, alifunga mabao 16 na asisti 11 katika mechi 28 alizocheza.

6) Alan Shearer – 1994/95
Mechi: 42
Mabao: 34
Asisti: 13
Alan Shearer alikuwa steringi wa Ligi Kuu England kwenye msimu wa 1994/95, wakati huo Blackburn Rovers iliposhinda ubingwa wao wa kwanza na wa mwisho wa Ligi Kuu England. Ligi ya msimu huo ilikuwa ya mechi 42 na ndipo Shearer alipoweka rekodi ya kufunga mabao 34 na kuasisti 13, hivyo akiwa amehusika kwenye mabao 47. Kwenye kikosi hicho cha Ewood Park, straika Shearer aliunda kombinesheni matata kabisa kwenye fowadi ya Rovers sambamba na Chris Sutton. Kipindi hicho ligi ilikuwa na timu 22, hivyo kwa msimu timu moja ilikuwa inacheza mechi 42. Sutton kwa msimu huo alifunga mabao 15 na asisti 10. Msimu uliofuatia, Blackburn ilimaliza ligi kwenye nafasi ya saba.

5) Thierry Henry – 2003/04
Mechi: 37
Mabao: 30
Asisti: 6
Kwenye msimu ambao Arsenal ilicheza bila ya kupoteza kwenye Ligi Kuu England, supastaa Thierry Henry alikuwa kwenye kiwango bora sana na kuibeba timu hiyo kwa mabega yake katika vita ya kubeba ubingwa. Henry alikuwa mwanasoka wa kiwango kikubwa sana na ingekuwa kwenye kipindi hiki, basi thamani ya mkali huyo sokoni ingekuwa Pauni 200 milioni. Bila ya huduma ya Henry kwa msimu huo, Arsenal ambayo ilicheza msimu wote bila ya kupoteza, isingebeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Henry ameondoka kwenye Ligi Kuu England, lakini akilicha jina lake juu na kuwa mmoja wa wachezaji mahiri kuwahi kutokea kwenye ligi hiyo.

4) Cristiano Ronaldo – 2007/08
Mechi: 37
Mabao: 31
Asisti: 7
Msimu huo, Cristiano Ronaldo alicheza kwa kiwango bora sana. Na kama vile ulikuwa mwanzo bora kabisa wa maisha yake ya soka, kwa sababu alikwenda kuwa matata zaidi alipojiunga na Real Madrid mwaka 2009. Baada ya kiwango bora kabisa katika msimu wa 2007/08, supastaa huyo wa Ureno alishinda Ballon d’Or, alichaguliwa pia mchezaji bora wa Fifa, Mchezaji bora wa PFA na mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu England kwa mwaka wa pili mfululizo na alishinfa pia Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England na kile cha Ulaya. Man United ilishinda ubingwa kwa tofauti ya pointi mbili, shukrani kwa mabao 31 ya Ronaldo na asisti saba zilizoifanya miamba hiyo ya Old Trafford chini ya Sir Alex Ferguson kunyakua taji hilo.

3) Erling Haaland – 2022/23
Mechi: 35
Mabao: 36
Asisti: 8
Straika Erling Haaland aliingia kwa kishindo kwenye Ligi Kuu England, ambapo alifunga hat-trick tatu katika mechi nane, huku kiwango chake kwenye mechi dhidi ya Manchester United, ambayo ilikuwa ya nane kwake tangu atue kwenye ligi, ilionyesha wazi jinsi mshambuliaji huyo alivyokuwa na balaa na tishio kwa makipa. Katika msimu wa 22/23 kulikuwa na timu mbili tu, ndizo ambazo Haaland alishindwa kuzifunga kwenye mechi 15 za mzunguko wa kwanza kwenye ligi. Kwa msimu huo, Haaland aliweka rekodi ya kufunga mabao 36 katika ligi ya mechi 38, huku akiasisti pia mara nane na kuisaidia timu yake ya Man City kunyakua ubingwa wa ligi. Idadi hiyo ya mabao ilitosha pia kwa Haaland kunyakua tuzo ya Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu England.

2) Thierry Henry – 2002/03
Mechi: 37
Mabao: 24
Asisti: 20
Staa matata kabisa, gwiji wa Ligi Kuu England, ambaye ametokeza kwa mara nyingine kwenye orodha hii. Msimu huo ulikuwa wa kipekee kabisa kwenye Ligi Kuu England, ambapo mchezaji mmoja alifunga mabao yanayoanzia 20 na kuasisti pia mara 20 ndani ya msimu mmoja. Katika msimu huo, Arsenal iliweka rekodi ya kuwa timu iliyofunga mabao mengi kwenye ligi, mara 85, lakini nusu ya mabao hayo, yalitokana na shughuli pevu ya mkali wa Ufaransa, Henry. Hata hivyo, kwenye tuzo ya Kiatu cha Dhahabu, Henry alishindwa mbele ya straika wa Manchester United, Ruud van Nistelrooy kwa tofauti ya bao moja tu, lakini alishinda tuzo ya PFA kutokana na kuwa na wastani mzuri wa mabao kwa dakika, ambapo alifunga bao moja kila dakika 75.

1) Luis Suarez – 2013/14
Mechi: 33
Mabao: 31
Asisti: 12
Suarez aliichezea Liverpool bora kabisa ambayo ilishindwa kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu England. Alikuwa kwenye kiwango bora sana kwa msimu huo, ambapo alifunga mara 31 katika mechi 33 alizocheza kwenye Ligi Kuu England na kuasisti pia mara 12, hivyo alihusika katika mabao 43. Fowadi huyo wa Uruguay alifanya kila kitu kuisaidia Liverpool kushinda ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu England, lakini ndoto hazikutimia.
Suarez alikosa mechi tano za mwanzo wa msimu kutokana na kufungiwa, lakini alipoanza kucheza tu, makipa wa timu pinzani walikuwa bize kuokota mipira kwenye nyavu zao, huku akigongesha nguzo mara tisa msimu huo, la mabao yangekuwa mengi zaidi. Hakupiga penalti yoyote, hiyo ilikuwa kazi ya Steven Gerrard.