Okejepha afunguka kuhusu Osimhen, Lookman
Muktasari:
- Nyota huyo maisha yake yalianza taratibu Simba ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana ushindani wa namba japo kwa sasa ameanza kuaminiwa na benchi la ufundi, ndipo Mwanaspoti lilipomtafuta na kufunguka mambo mengi.
KIUNGO mkabaji wa Simba, Augustine Okejepha ameanza kufurahia maisha ndani ya kikosi hicho tangu asajiliwe msimu huu akitokea Rivers United ya kwao Nigeria, huku akiweka wazi amekuja nchini kupambania na kutimiza malengo.
Nyota huyo maisha yake yalianza taratibu Simba ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara kutokana ushindani wa namba japo kwa sasa ameanza kuaminiwa na benchi la ufundi, ndipo Mwanaspoti lilipomtafuta na kufunguka mambo mengi.
MTU WA USHINDANI
Okejepha anasema yeye ni mchezaji anayependa ushindani katika jambo lolote akiamini ndiyo siri ya kufanikiwa na kutimiza malengo aliyojiwekea hivyo, sio mtu wa kukata tamaa hata kama atapitia changamoto nyingi mbalimbali za kumrudisha nyuma.
“Changamoto ni sehemu ya maisha ya binadamu lakini kwangu nazichukulia kama fursa ya kunikuza kiakili, kuna muda naona kabisa hata nafasi ya kucheza sipati, ila najiangalia mwenyewe na kugundua napaswa kufanya nini cha utofauti,” anasema.
Nyota huyo anasema hata pindi anapokosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza huwa haimuumizi, kwani kitu anachokifanyia kazi ni kuangalia wenzake wamemzidi nini ili afanye jambo la utofauti litakalowapa matumaini benchi la ufundi kumtumia.
KATI KWA MOTO
Nyota huyo anasema licha ya ushindani wa namba kwa wachezaji wenyewe kwa wenyewe ila anaeleza changamoto kubwa ipo sana eneo la kiungo analocheza yeye, huku akieleza sio rahisi kucheza ikiwa utakuwa hujitumi ipasavyo wakati wa mazoezini.
“Eneo la kiungo limekamilika kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya wachezaji bora wanaocheza hapo, kwangu napenda kucheza na kila mmoja wao, iwe ni Debora Fernandes Mavambo, Yusuph Kagoma, Mzamiru Yassin na wengine wote mimi freshi tu,” anasema.
AHOUA MTU SANA
Okejepha anasema timu hiyo ina wachezaji wazuri katika kila nafasi ingawa kwa wakati huu nyota ambaye amekuwa akichangia sana matokeo mazuri ya kikosi hicho ni Jean Charles Ahoua, kwani asipofunga atatengenezea wengine waweze kufunga pia.
“Unapotaja wachezaji bora wa Simba hadi sasa hutoacha kumtaja Ahoua, jamaa anajua kufunga mabao na kusaidia upatikanaji wa mengine ‘asisti’, kiukweli ni nyota tunayejivunia uwepo wake lakini anatufanya kila mmoja wetu pia kupambana zaidi.”
Ahoua aliyejiunga na Simba pia msimu huu akitokea Stella Club Adjame ya kwao Ivory Coast na alikuwa mchezaji bora wa msimu ‘MVP, amefunga mabao matano ya Ligi Kuu Bara na kuchangia manne ‘asisti’, jambo linalomfanya Okejepha kumsifia.
Nyota huyo anasema ilikuwa rahisi kukubali ofa ya Simba wakati ilipomuhitaji licha ya klabu nyingi kutoka Bara la Afrika kuhitaji saini yake, japo ukubwa wa timu hiyo ilikuwa moja ya chachu iliyomshawishi kukubali kuja nchini kujiunga nayo.
“Rivers yenyewe ambayo nimetokea iliniwekea ofa nzuri ya kuhitaji kunibakisha ila baada ya kuona Simba pia inanihitaji niliwaomba viongozi wangu waniruhusu niondoke, kiukweli walinipa baraka zao na ndiyo maana leo hii niko hapa kikosini.”
SOKA LA BONGO LIMEKUWA
Kitu kikubwa ambacho kimemvutia pia nyota huyo kutua nchini ni kutokana na soka la Tanzania kupiga hatua kubwa katika ukanda huu wa Afrika, tofauti na Ligi ya kwao Nigeria ambayo uchumi wake sio mkubwa kiasi cha wachezaji kuamua kuondoka.
“Ukiangalia wachezaji wa Nigeria wanaocheza Tanzania ni wengi kuliko wa hapa wanaocheza kule, hii inaonyesha wazi kwamba kuna hatua kubwa zimepigwa, ukiangalia kiuchumi utaona Bongo kunalipa pia vizuri ndio maana kumekuwa kimbilio la wengi.”
Nyota huyo anasema Nigeria ni moja ya nchi iliyojaaliwa vipaji vingi vya soka tofauti na nchini, ingawa ukilinganisha kwa Ligi utaona kuna utofauti mkubwa, kwa sababu Tanzania ina viongozi na mashabiki wanaopenda kujitolea katika mpira.
OSIMHEN, LOOKMAN WAMPA MZUKA
Moja ya wachezaji Okejepha anajivunia kwake ni washambuliaji Victor Osimhen anayecheza Galatasaray ya Uturuki na Ademola Lookman anayeichezea Atalanta ya Italia, ambao anakiri ni nembo ya Nigeria kwa sasa katika kuitangaza taifa hilo kisoka.
“Unapotaka wachezaji wakubwa na wanaowakilisha taifa vizuri la Nigeria kwa sasa hutoacha kuwataja, Osimhen na Ademola kutokana na viwango bora wanavyovionyesha nje ya Bara la Afrika, ni kioo kwetu cha kuendelea kupambania tu ndoto zetu.”
MAKOCHA WAMSHANGAZA
Kama kuna kitu ambacho nyota huyo kimemshangaza tangu atue hapa nchini ni kuona wimbi kubwa la makocha wa kigeni wakiwa ndio wakuu wa benchi la ufundi, tofauti na kwao Nigeria ambao wazawa ndio wametawala kuanzia timu kubwa hadi za kawaida.
“Kwetu Nigeria makocha wengi wanaofundisha timu za kule ni wazawa na wana uwezo mkubwa sana japo wanaangushwa na suala tu la kiuchumi kama nilivyosema hapo mwanzo, huku nimeona ni tofauti lakini ni kawaida kwa nchi zilizoendelea kisoka.”
MIKAKATI MIZITO
Nyota huyo anasema moja ya malengo yake makubwa ni kuhakikisha kikosi hicho kinatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu huu, huku akieleza jambo hilo linawezekana ikiwa wataendelea kupambana katika kila mchezo hadi pale msimu utakapoisha.
“Hadi sasa tuko katika njia sahihi za kupigania malengo yetu lakini bado ni mapema na hatupaswi kubweteka, naamini kwa umoja na ushirikiano wa kila mmoja wetu msimu huu utakuwa bora kwetu kuanzia Ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.”