Prime
NYUMA YA PAZIA: Ten Hag anavyojua kununua mshale wa sekunde
Muktasari:
- Wakapotea muda mrefu kiasi kwamba ingekuwa ndoto kwao kuingia Top Four. Ni kweli walikosa. Katika pambano la mwisho la msimu ambalo walitegemewa kupoteza dhidi ya Manchester City fainali ya FA, wakaibuka na kutwaa taji.
“….KILA dakika inayokuweka hai jaribu kuinunua kwa gharama yoyote ile..”. Aliandika mwandishi anayeitwa Ben Mtobwa katika kitabu chake alichokiita Tutarudi na roho zetu?. Unahitaji mfano halisi? Mtazame kocha mmoja ana kipara anakaa katika benchi la Manchester United. Hatujui filamu hii itaisha lini. Maisha ya Erik Ten Hag na Manchester United yanasisimua, hasa kama hauipendi Manchester United. Anasisimua namna anavyowayumbisha akili Manchester United. Hawajui washike lipi dhidi yake. Picha linaendelea. Unapohisi Ten Hag anakaribia ‘kupoteza pumzi’ ghafla anaibuka na kunyanyuka. United hawamuelewi. Hatujui wataenda naye mpaka lini. Msimu uliopita United walionekana hoi huku wakikosa pumzi.
Wakapotea muda mrefu kiasi kwamba ingekuwa ndoto kwao kuingia Top Four. Ni kweli walikosa. Katika pambano la mwisho la msimu ambalo walitegemewa kupoteza dhidi ya Manchester City fainali ya FA, wakaibuka na kutwaa taji.
United wakapoteza nguvu za kumfukuza Ten Hag. Mpaka leo hii huenda Ten Hag angekuwa hana kazi au angekuwa anafundisha timu nyingine huko kwao Uholanzi kama angepoteza pambano lile. Kulikuwa na sababu lukuki za kumfukuza. Lakini ghafla akawa na silaha moja nzito mkononi. Kombe la FA.
Wanahitajika matajiri wachache kama Roman Abramovich kumfukuza kocha mwenye taji mkononi. Taji ambalo amelitwaa juzi au jana. Matajiri wa Marekani wa United wakakosa nguvu ambazo Mrusi alikuwa nazo. Ten Hag akabaki huku akizungumza maneno ya nyodo.
Msimu huu ulipoanza yeye ndiye aliyefungua dimba siku ya Ijumaa. Pambano la kwanza la Ligi Kuu England. Peke yao, Manchester United dhidi ya Fulham. Timu haikuonekana kubadilika. Dakika za jioni wakafunga bao la ushindi.
Ushindi huo uliwapeleka kileleni. Wakahisi baridi na wakaanza kutangaza maneno ya nyodo. Jumamosi ilipofika na timu nyingine kucheza, United wakajikuta nafasi ya nne. Hawajawahi kurudi tena pale juu. Sasa hivi ni wa 11.
Mechi mbili zilizofuata United akanyukwa na Brighton na Liverpool. Mashabiki wakabana meno kwa hasira. Mechi iliyofuata Ten Hag akatetea roho yake. Akainunua dakika ambayo ilitishia uhai wake. Akamchapa Southampton mabao 3-0 ugenini.
Nawajua baadhi ya mashabiki wa Manchester United ambao walitamani kuiona timu yao ikifungwa ili Ten Hag afukuzwe. Hata hivyo ni katika dakika kama hizi ndipo Ten Hag huwa anawaudhi mashabiki wake. Akaibuka na ushindi.
Mechi iliyofuata akaleta tena maudhi. Dhidi ya Crystal Palace ugenini. Akatoka suluhu. Wakati City na Arsenal zikipunguzana pale Etihad kwa kutoka sare ya mabao 2-2, United ingeweza kutumia nafasi hiyo kupata pointi tatu, lakini wakati wenzake wakitoka sare katika mechi ngumu, yeye ndio kwanza akatoka sare.
Jumatano usiku ametoka sare tena na klabu ndogo ya Twente pale Old Trafford katika michuano ya Europa. Mashabiki wa United wamepandwa tena na hasira. Nadhani wapo ambao wanatamani kuiona United ikipoteza katika pambano la wikiendi hii dhidi ya Tottenham Hotspurs pale Old Trafford. Zinabakia hisia tu kwamba labda wakipoteza ndio utakuwa mwisho wa Ten Hag.
Hata hivyo ni katika mechi kama hizi ndipo Ten Hag anajua kuitetea roho yake. Utasikia ameshinda dhidi ya Tottenham kwa mshangao wa wengi. Ni hapo ambapo mabosi wanapoteza nguvu ya kumfukuza. Ukitaka kumfukuza Ten Hag inabidi uangalie mwelekeo wa ujumla wa timu. Ukitaka kumfukuza kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya unaweza usimfukuze.
Na sasa kitu cha kupima kutoka kwa mabosi wa Manchester United ni kama Ten Hag ni mtu sahihi kwa ujumla wake. Wanaamini kwamba anaweza kuwapeleka katika nchi ya ahadi bila kujali sana milima na mabonde ambayo anapitia katika matokeo.
Binafsi naona Manchester United wanapoteza muda tu. Sioni mwelekeo sahihi wa United chini ya Ten Hag. Mpaka leo sijui United ni bora katika kitu gani. Kushambulia, kukaba, kukaa na mpira? Sijaona pia United wanaelekea wapi kwa aina ya wachezaji ambao wanawanunua. Wanacheza aina tofauti ya mpira, lakini zaidi sijajua kama ana mpango wa kupunguza umri klabuni au vinginevyo.
Swali la msingi ambalo lipo ni kama United ikiamua kuachana na Ten Hag wanaweza kwenda kwa kocha gani wa kisasa ambaye atawarudishia ufalme wa Sir Alex Ferguson? Huu ni mwaka wa 11 hawajachukua taji la Ligi Kuu England na kila wanapobadili makocha bado hali inakuwa mbaya.
Walimchukua David Moyes kwa ajili ya kumkabidhi mpango wa muda mrefu klabuni, lakini safari haikufika mbali. Wakaenda kwa makocha wenye uzoefu kina Louis Van Gaal na Jose Mourinho, lakini bado haikusaidia kutengeneza ‘project’ ya uhakika klabuni.
Walirudi kwa kocha kijana Ole Gunnar Solskjaer, lakini haikusaidia. Wamerudi kwa kijana mwingine Ten Hag ambaye ilionekana angefanya kitu kama ambacho Jurgen Klopp aliifanyia Liverpool au Mikel Arteta anajaribu kuifanyia Arsenal kwa sasa. Walau hawa walishindana na Pep Guardiola.
Na sasa hatujajua Ten Hag ataendelea kununua muda mpaka lini. Anachonifurahisha ni kiburi chake cha kwamba yeye ndiye kocha pekee mwenye uwezo wa kuifikisha United katika nchi ya ahadi. Ukimuona katika televisheni anafurahisha namna anavyojiamini pindi akilisema hili.
Mechi mbili zinazofuata ni dhidi ya Tottenham kisha Aston Villa ugenini. Labda tunaweza kupata mwanga wa hatima yake lakini kwa sasa hatuoni mwanga katika hatima yake. Unaweza kukuta tunakula naye Krismasi mwishoni mwa mwaka akiwa katika benchi la United. Sijaona kocha anayejua kununua mshale wa sekunde kama yeye. Tusubiri.