Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: Pesa imeongea sauti kubwa, tukutane Riyadh 2034

Saudia Pict

Muktasari:

  • Majuzi tulikuwa Qatar tukiungua jua na kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwishoni mwa 2022. Si kawaida. Kombe la Dunia mara nyingi imekuwa ikichezwa Juni-Julai. Pesa ziliongea. Waarabu wakamwaga pesa kwa wajumbe Kombe la Dunia likachezwa Desemba.

ALIWAHI kujisemea bosi mmoja wa benki wa Marekani, Herbert Prochnow. “Wakati pesa inaongea, kuna vitu vichache sana vinaweza kuingilia kati.” Ni kweli. Tumepeleka Kombe la Dunia pale Riyadh, Saudi Arabia. Lilikuwa suala la muda tu.

Majuzi tulikuwa Qatar tukiungua jua na kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwishoni mwa 2022. Si kawaida. Kombe la Dunia mara nyingi imekuwa ikichezwa Juni-Julai. Pesa ziliongea. Waarabu wakamwaga pesa kwa wajumbe Kombe la Dunia likachezwa Desemba.

Zamani mzunguko ungeweza kuchukua muda mrefu kabla ya Kombe la Dunia halijarudi kwa Waarabu. Hata hivyo, sasa hivi Mwarabu anautaka mpira. Anaupenda zaidi. Anatumia pesa zake kuhakikisha jambo kubwa linakuwa dogo.

Majuzi wakubwa wenye mpira, hapana shaka baada ya kupokea bahasha nzuri, wamerudisha tena Kombe la Dunia pale Saudi Arabia. Ina maana ndani ya miaka 12 tu michuano hiyo litakuwa limechezwa Qatar na Saudi Arabia. Zamani tusingetegemea hivyo.

Kuna akili imetumika kuturudisha tena kwa Waarabu. Kwanza kabisa ni kuhakikisha hakuna malalamiko kutoka kwa mabara mengine. Kwa mfano, Kombe la Dunia lijalo litafanyika Marekani, Canada na Mexico. Ina maana hakutakuwa na malalamiko kutoka kwa watu wa Amerika Kaskazini. Wameshapewa kuandaa Kombe la Dunia.

Halafu mwaka 2030 ambapo Kombe la Dunia litakuwa linatimiza miaka 100 wakubwa wamepeleka liandaliwe na nchi tatu kwa pamoja. Morocco, Hispania na Ureno. Hapa ina maana kuna Afrika na Ulaya kwa pamoja.

Lakini kuna nchi tatu nyingine ambazo zitaandaa mechi maalumu za maadhimisho ya miaka 100 ya fainali hizo.  Argentina, Paraguay na Uruguay. Hii ina maana Amerika Kusini watakuwa pia wameandaa Kombe la Dunia kimtindo. Ina maana katika michuano miwili ijayo tayari Ulaya, Afrika, Amerika Kaskazini na Amerika Kusini watakuwa wameandaa michuano hii. Kwanini lisirudi Asia?

Bahati mbaya Asia yenyewe sio ile ya Korea Kusini na Japan. Sio ile ya Singapore, Malaysia au Hongkong. Ni Asia ile ya watu walioamua kuwekeza noti nyingi zaidi katika soka. Wakati mwingine unaamini kwamba wanaweka noti kwa kujifurahisha.

Wanapenda tu mpira unavyochezwa sebuleni kwao. Walianzia kwa kupenda tu kuona kina Cristiano Ronaldo, Neymar na wengineo wenye majina makubwa wakicheza katika viwanja vyao. Wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na sasa wanapenda tu dunia yote ihamie kwao.

Ilianzia kwa Qatar na sasa Saudi Arabia. Kitu ambacho kimewahi kuniumiza kichwa baada ya kulitazama Kombe la Dunia pale Qatar ni namna gani wameweza kurudisha pesa za uwekezaji wao. Nchi ndogo ambayo iliandaa michuano mizuri.

Baada ya ile michuano sijui tungeweza kurudi Qatar kufanya nini. Kufanya utalii? Hapana. Kufanya manunuzi (shopping) hapana. Waliamua tu kuionyesha dunia jeuri ya pesa. Kwa kiasi kikubwa walifanikiwa katika hili.

Waliweka viwanja ambavyo vina vipoza hewa (air conditioners). Wakaweka viwanja ambavyo vilikuwa na vyumba hadi vya hoteli za nyota tano. Lengo ilikuwa ni kuionyesha dunia jeuri ya pesa. Ni kweli walifanikiwa.

Nadhani hata Saudi nao watafanya hivyo hivyo. Watafanya mambo mengi ya kufuru kuionyesha dunia kwamba wana pesa. Nadhani kwa sababu nchi za kule zina ushindani bwana ifikapo mwaka 2034 watataka kuionyesha dunia namna ambavyo mwanadamu anapaswa kuishi.

Zamani Kombe la Dunia lilikuwa zaidi kwa zile nchi ambazo zilikuwa na nguvu ya kimpira. Nchi za Ulaya na zile za Amerika Kusini. Mara moja walitoka kwenda Afrika pale Afrika Kusini halafu wakawahi kwenda Korea Kusini na Japan.

Lakini sasa Mwarabu analiita Kombe la Dunia kwa lazima. Usidhani kuna hiyari sana. Nyuma ya Pazia kuna bahasha nzito zinatembea kwa watoa uamuzi. Pesa inaongelea na ikiongea basi kuna vitu vichache sana vinaweza kuingilia kati. Huu ni ukweli unaouma.

Kuna mambo machache ambayo tunasubiri kuona ifikapo wakati huo. Pombe zitaruhusiwa? Kumshika mpenzi wako kiungo hadharani itaruhusiwa? Kulala chumba kimoja na mwanamke ambaye haujamuoa itaruhusiwa?

Rafiki zetu wanaishi katika tamaduni zao. Halafu Kombe la Dunia lina tamaduni zake. Pale Qatar rafiki zetu walileta hadithi ya mbuni kufunika kichwa katika mchanga akiamini amejificha. Kuna eneo maalumu ambalo lilitengwa kwa ajili ya sisi walevi. Tukanywa pombe zetu kwa raha zetu.

Isingewezekana kukwepa hili kwa sababu kuna kampuni moja ya bia ni wadhamini wakubwa wa FIFA. Kila siku wanaweka pesa zao FIFA. Isingewezekana katika michuano mikubwa kama hii wasiuze chupa zao za pombe.

Kule Saudia hatujui itakuwaje. Nasikia katika kuhakikisha ligi yao inakwenda vizuri na inavutia wachezaji kutoka nje wametengua baadhi ya vipengele vya dini. Kwa mfano, Ronaldo ameruhusiwa kulala na mpenzi wake, Georgina ingawa hawajaoana. Wangefanya nini wakati walihitaji huduma za Ronaldo? Walihitaji jina la Ronaldo katika Ligi yao na Ronaldo asingeweza kwenda bila ya hawara yake.

Nasikia kuna wachezaji ambao wanapelekewa pombe zao kimya kimya na kufanya ‘party’ za ndani kwa ndani. Neymar ana kundi lake la watu hamsini ambao kila siku wanajirusha katika jumba lake la kifahari. Pombe nasikia zinakuwapo. Nadhani hadi kufika mwaka huo kwa wale ambao watakuwa na pumzi watashuhudia mengi.

Lazima waombaji na wale wakubwa waliotoa ruhusa ya michuano hii kufanyika kule Riyadh wameshaambiana masharti ya maisha ya Kombe la Dunia.

Sidhani wale waliopokea bahasha watakuwa wajinga kiasi gani kuruhusu tufike Saudia bila ya kunywa. Kwanza wenyewe ni wanywaji wakubwa.