NYUMA YA PAZIA: Mzee wa 'Bling' Lingard alipoamua kujali akaunti yake

NYUMA YA PAZIA: Mzee wa 'Bling' Lingard alipoamua kujali akaunti yake

NIKUSIMULIE kitu? Achana na majina makubwa sana katika soka. Sahau mabao mawili ya Erling Haaland dhidi ya West Ham. Sahau Kylian Mbappe anafanya nini. Usijali sana kuhusu kilichoikuta Manchester United wikiendi. Kuna kitu nataka kukusimulia kidogo kuhusu mchezaji anayeitwa Jesse Lingard.

Sijui kama amenifurahisha au hapana. Alimaliza mkataba wake na Manchester United mwishoni mwa msimu uliopita. Kabla ya hapo Lingard alikwenda zake kwa mkopo West Ham. Aling’ara haswa. United ikapata hamu ya kumrudisha kwa kuamini kwamba angehamishia kile alichofanya West Ham akiwa Old Trafford kwa mara nyingine.

Hata hivyo, mambo hayakwenda sawa. Sijui tatizo lilikuwa yeye au kocha Ralf Rangnick. Sijui. Ninachojua ni kwamba aliporudi alianza kusugua benchi tena. Kuna wakati nilikuwa nawaza ni kipi hasa ambacho United iliamua kumrudisha. Kwamba kwanini wamrudishe halafu wamuweke benchi?

Sijui kama alijali sana. Mwisho wa msimu mkataba wake ukamalizika. Ulipomalizika alitakiwa na klabu ambayo aling’ara kwa mkopo, West Ham. Watu wengi walipenda arudi zake West Ham ambayo kwanza aling’ara nayo, lakini pili inaonekana kuwa klabu ambayo inaleta upinzani kwa wakubwa.

West Ham wanachachafya katika siku za karibuni. Wanashindana haswa. Watakuwepo Europa msimu ujao lakini pia kocha wao, David Moyes amewaweka kuwa katika ushindani. West Ham walipambana vilivyo kuinasa saini ya bwana Lingard.

Mwishowe nini kimetokea? Lingard ameamua kusaini zake Nottingham Forest. Timu ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu baada ya kupotea kwa miaka 23 iliyopita. Amewaacha mdomo wazi wachambuzi na watu wa soka ambao wanaamini kwamba West Ham ingekuwa sehemu sahihi zaidi kwake.

Sio West Ham tu, kuna timu tatu zaidi za Ligi Kuu ya England ambazo zilikuwa zinasaka saini yake. Bwana Lingard ameamua kwenda zake Nottingham Forest bila kinyongo wala wasiwasi. Ameenda katika timu ambayo imepewa uwezekano mkubwa wa kushuka msimu ujao.

Kisa? Amepewa mkataba ambao kwake ni mnono. Ni mkataba ambao unaweza kufikia Pauni 200,000 kwa wiki. Rafiki yangu Lingard hajataka kuangalia mambo mengi zaidi ya akaunti yake. Amesaini mkataba wa mwaka mmoja tu na jambo hilo linamaanisha mambo mengi.

Kwanza anamaanisha kwamba hata timu ikishuka daraja yeye ana uhakika wa kubaki Ligi Kuu wakati huo akiwa tayari ameshapokea pauni zake kwa msimu mzima. Kifupi ni kwamba anawaacha nyinyi mmezama halafu yeye anaibuka na timu nyingine huku akaunti yake ikicheka.

Na mkataba wake hauruhusu Forest kuongeza mkataba mwingine. Labda kama wakibaki na yeye wakaendelea kumpa pauni zake. Hii ina maana amekwenda Forest kusaka noti tu wakati huu akiwa na umri wa miaka 29 huku akiwa hana mpango wa kushinda taji lolote. Tangu lini Forest ikakuhakikishia taji baada ya kupanda Ligi Kuu.

Rafiki zangu wachambuzi wa Ulaya wamenuna kwelikweli. Wameongozwa na Jamie Carragher. Alisikika akisema: “Amekwenda Forest kwa sababu ya pesa. Nafurahi kwamba Nottingham Forest wamerudi Ligi Kuu, lakini kama mtu anaichagua Forest mbele ya West Ham kwa sasa ni kwa sababu amefuata pesa.”

Gary Neville naye alirudia maneno hayo hayo ambayo rafiki yake Carragher alikuwa ameyasema. Kumalizia hasira hizi, kesho Jumapili linapigwa pambano la Nottingham Forest dhidi ya West Ham ambayo inaaminika alipaswa kwenda. Mashabiki wa West Ham ambao wote walimpenda Lingard wakati akiwa kwa mkopo klabuni kwao wamepanga kutengeneza noti bandia na kumtupia ili kumuonyesha kwamba ana tamaa ya pesa.

Haya yakiendelea, binafsi najisikia kucheka tu. Namjua vyema mshkaji wangu Lingard. James Hardley aliwahi kuuliza ‘Kitu gani ni bora kuliko pesa?’ Lingard anaonekana kuwa bize kufunga hesabu zake za pesa katika kazi ya soka. Lakini pia hawezi kuacha pesa ndefu wakati yeye ni mtu wa kula starehe kila kukicha.

Lingard anapenda maisha ya starehe. Huwa anaishi kama staa wa Hollywood. Mara nyingi nimekuwa nikifuatilia maisha yake binafsi. Anapenda kungaa. Cheni nyingi shingoni na mavazi ya thamani. Anaweza asiwe Cristiano Ronaldo lakini anataka kuishi kama yeye.

Ukitazama picha zake za starehe huwa yupo na kina Chris Brown, Neymar, Ronaldinho na wengineo. Nenda Google tafuta picha zake za starehe unaweza kudhani Lingard ni mwamuziki maarufu wa Kimarekani. Anaonekana kama wao. Anaishi kama wao.

Linapokuja dili kama la West Ham, mchezaji wa aina hii hawezi kutazama mambo mengi zaidi ya pesa. Kama Forest wapo mbele ya West Ham kipesa yeye anatazama pesa zaidi. Anaangalia kile ambacho kipo mbele yake. Acha kina Carragher na Neville waongee. Acha mashabiki wa West Ham wamkejeli.

Anachojali yeye ni kuendelea kusuguana mabega na kina Neymar katika sehemu za starehe. Anachoangalia yeye ni uwezekano wa kulipa bili bila ya manyanyaso katika meza ileile ambayo Neymar, Lil Wayne, Chris Brown wamekaa. Hajali kama anachezea Manchester United au West Ham.

Lakini hapohapo kumbuka kwamba Lingard sio mjinga. Anataka kuendelea kula bata hata msimu huu ukiisha. Amesaini mkataba wa mwaka mmoja tu. Ina maana mwisho wa msimu huu atakuwa mchezaji huru. Kuna mambo mawili yanaweza kutokea.

Kama akifunga mabao zaidi ya kumi halafu Forest ikabaki Ligi Kuu ni wazi kwamba atakuwa mfungaji wao bora. Na kama watabaki Ligi Kuu watataka abaki nao na ni wazi watampa mkataba mwingine ambao utasababisha aendelee kutumia meza moja na kina Chris Brown.

Lakini kama pia akifunga mabao zaidi ya kumi na kisha Forest ikashuka bado atakuwa na uhakika wa kubaki Ligi Kuu. Katika nyakati kama hizi wachezaji huwa wanajali hatima zao binafsi kuliko hatima za timu. Ni nyakati hizo ndipo atakaporudi katika timu za katikati.

Kwa sasa Lingard hana mpango na timu yenye hadhi yoyote ile. Anaangalia namna gani ataendelea kuishi maisha yake ya kula bata na washkaji. Ameshinda mataji kadhaa kama FA, Europa na Carabao lakini sidhani kama ana tamaa kubwa kama mchezaji.

Angekuwa na tamaa kubwa kiasi angeweza kwenda West Ham kuliko Forest. Mara nyingi timu zinazopanda huwa zinatabiriwa kushuka lakini usidhani kama Lingard hajui hilo. Ndio maana amesaini mkataba wa mwaka mmoja kwa sababu ana maana yake kaka.