NYUMA YA PAZIA: MOURINHO, MSHALE WA SEKUNDE UNAKATA ROHO
Muktasari:
ALIWAHI kujisemea mwandishi maarufu wa Marekani, Elizabeth Forsythe Hailey kuwa ‘muda ni kitu cha kikatili ambacho kinatufanya tuwe watu wa zamani’. Ni kweli. Wakati mwingine muda unakuwa kitu katili sana.
ALIWAHI kujisemea mwandishi maarufu wa Marekani, Elizabeth Forsythe Hailey kuwa ‘muda ni kitu cha kikatili ambacho kinatufanya tuwe watu wa zamani’. Ni kweli. Wakati mwingine muda unakuwa kitu katili sana.
Nilishtuka usingizini juzi usiku na kukuta mtu anayeitwa Mislav Orsic akiwa amemtupa nje Jose Mourinho katika michuano ya Europa. Ina maana Dinamo Zagreb walikuwa wameitupa nje Tottenham Hotspur katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Kwa tunavyomfahamu Jose tangu zamani ilikuwa rahisi kutotazama mechi na kusubiri kuangalia asubuhi jinsi alivyopita katika hatua husika hasa baada ya ushindi wa mabao 2-0 katika pambano la kwanza. Ndivyo alivyotuzoesha.
Zamani Jose angekufunga 2-0 katika pambano la awali basi hatua hiyo ilikuwa imeisha. Mechi ya pili angefunga milango yake ya chuma, kisha akasogeza basi kando yake, halafu angehamishia Mlima Kilimanjaro mbele ya basi hilo. Hakuna ambaye angeziona nyavu zake.
Iwe dhidi ya Barcelona, Manchester United (ya Sir Ferguson), Arsenal (ya Arsene Wenger), Real Madrid, AC Milan (ya Ricardo Kaka) au timu nyingine yoyote ile.
Jose alijua kufunga milango yake ya chuma. Leo Jose anashindwa kufanya hivyo dhidi ya timu ya kawaida kutoka Croatia. Nyakati zimekwenda wapi?
Mambo mawili kuhusu wakati yanakufanya ukumbuke kauli ya Elizabeth kuhusu Jose Mourinho. Kwanza kabisa msimu huu unaanza kumtupa mkono. Amebakiza dakika 90 tu za pambano dhidi ya Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi.
Akishinda mechi hii anaweza kuwa ametubadilisha mawazo kiasi. Anaweza kuwa amewabadilisha mawazo mashabiki wa Tottenham ambao hawajachukua taji lolote tangu mwaka 2008. Lakini jikumbushe tena. Anacheza na nani? Manchester City.
Hasira za Pep Guardiola zote zitashuka katika mgongo wake. Na sio kwa kubahatisha. City wana timu bora. Jose anahitaji maajabu yatokee ili aweze kushinda taji hili. Hatujui atafanyaje lakini ukweli ni kwamba ana kazi nzito ya kufanya.
Katika Ligi, Jose anashika nafasi ya nane. Ana kazi nzito ya kuingia Top Four. Huu ni msimu wake wa pili kamili akiwa na kikosi cha Tottenham. Katika msimu wake wa kwanza ungeweza kumsamehe na kusema kwamba anakisuka kikosi chake. Katika msimu wake huu wa pili tulipaswa kujua mwelekeo wa Tottenham.
Hata hivyo Tottenham haipati matokeo yoyote ya maana na Jose ameendelea kuwa yuleyule. Mlalamishi kwa waamuzi, mlalamishi kwa makocha wa timu pinzani, mlalamishi kwa wachezaji wa timu pinzani na pia mgomvi dhidi ya wachezaji wake. Hana uhusiano mzuri na Dele Ali na baadhi ya wachezaji.
Ni katika msimu huu wa pili Jose anapaswa kuhukumiwa kwa kukosa mwelekeo. Alinunua wachezaji aliowataka mwenyewe. Alianza Ligi vema na ilionekana kama vile alikuwa ana jambo jipya katika Ligi. Kumbe tulikosea.
Kumbe Jose ameendelea kuwa yule yule wa miaka ya karibuni. Yule aliyefukuzwa na Ed Woodward pale Manchester United. Hana maajabu. Na hapa ndipo tunapoikumbuka kauli ya Elizabeth kwa mara ya pili. Jose amepitwa na wakati kwa ujumla?
Inawezekana Jose amepitwa na wakati. Si tu kwa msimu huu, lakini pia ukichunguza maisha yake ya soka katika miaka ya karibuni. Soka la kisasa linamtupa. Hana maarifa tena. Zamani alikuwa na maarifa mazuri katika kusuka timu inayojihami vema. Walau alijipambanua ni kocha wa namna gani.
Siku hizi Jose hatumuoni popote. Timu zake hatujui zinataka nini uwanjani. Hatujui kama ni mzuri katika kushambulia au katika kujihami. Spurs inafungwa kiurahisi kama timu nyingine yoyote ile. Na katika kushambulia inafunga katika mazingira magumu kama timu nyingine yoyote ile ya mitaa ya kati.
Kitu kibaya zaidi ni kwamba licha ya msimu wake wa mwisho kutokuwa mzuri na Tottenham, lakini Muargentina Mauricio Pochettino alifanikiwa kututengenezea Tottenham iliyokuwa kali enzi zake. Tottenham ambayo haikuchukua taji lolote lakini ilikwenda katika fainali za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
ule ukali wa watu wanne wa Pochettino, Harry Kane, Son, Dele Ali na Christian Eriksen umeondoka. Tottenham ya leo sio tishio tena licha ya kurudi kwa Gareth Bale ambaye anaonekana wazi kwamba hana furaha klabuni hapo.
Tunalazimika kuendelea kusubiri tena na tena kuona kam Jose amefika mwisho lakini viashiria ni vingi. Inaonekana mshale wake wa sekunde unakaribia kukata roho. Muda si mrefu tunaweza kusema ‘alikuwa mmoja kati ya makocha bora zaidi duniani’. Hata kwa Arsene Wenger iliwahi kuwa hivyo. Kuna nyakati ambazo alitisha lakini baadaye akageuka kuwa kichekesho katika kila kitu. Huwa inatokea. Hata hivyo nina hofu kwamba kwa Jose huenda inatokea mapema zaidi kwa sababu umri wake katika kazi hii sio mkubwa sana. Ana miaka 58 tu huku kukiwa na makocha wengi ambao waliendelea kuwa bora licha ya kuvuka umri huo.
Huenda soka la kisasa linampita Jose? Inawezekana. Ule mwaka aliokaa benchi kwa muda mrefu kabla ya kuibukia Tottenham tulikuwa tunatazamia kwamba labda alikuwa anautumia muda wake mwingi kujaribu kujua zaidi mbinu za makocha wa kisasa. Hata hivyo inaonekana aliambulia patupu. Baada ya kuchapwa na Zagreb juzi kuna mashabiki wakongwe wa Tottenham wameanza kupiga kelele Jose aondoke klabuni. Kama Spurs akichapwa na City katika fainali za kombe la Ligi, kama Spurs ikishindwa kuingia Top Four, basi hauwezi kujua. Huenda tukawa tumeuona mwisho wa Jose Tottenham.
Na kama Jose akifukuzwa Tottenham ina-maanisha atakuwa ame-fukuzwa na timu ndogo zaidi aliyowahi kufundisha maishani. Tottenham ipo chini ya Chelsea, Manchester United, Real Madrid na Inter Milan. Tusubiri.