Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NYUMA YA PAZIA: Mauro Icardi na Wanda Nara mfano sahihi wa muosha huoshwa

Icardi Pict

Muktasari:

  • Wakati fulani Icardi na Lopez walicheza pamoja katika Klabu ya Sampdoria. Nadhani hapo ndipo Icardi alipoanza kumtamani mke wa mwenzake. Na Wanda ni mrembo kweli. Alichokitaka kilitimia. Wanda akamuasi Lopez huku akitimka na watoto wake watatu.

NITAKUSIMULIA kitu. Nitakusimulia stori maarufu ya mshambuliaji wa Galatasaray anayeitwa Mauro Icardi. Staa huyu wa Argentina ambaye hata hivyo timu ya Argentina ameichezea mechi nane tu, Icardi alijichomeka katikati ya penzi zito la staa mwenzake wa kimataifa wa Argentina, Maxi Lopez na mrembo mzuri wa Kiargentina, Wanda Nara. Nara alikuwa mke wa Lopez kwa miaka kadhaa na walifanikiwa kupata watoto watatu.

Wakati fulani Icardi na Lopez walicheza pamoja katika Klabu ya Sampdoria. Nadhani hapo ndipo Icardi alipoanza kumtamani mke wa mwenzake. Na Wanda ni mrembo kweli. Alichokitaka kilitimia. Wanda akamuasi Lopez huku akitimka na watoto wake watatu.

Talaka ilitolewa mwaka 2013, Icardi akamuoa Wanda mwaka 2014. Nchi nzima ya Argentina ilinuna. Diego Maradona alinuna. Lakini zaidi ikasemwa kwamba Lionel Messi ambaye alikuwa na ushawishi mkubwa katika kikosi cha Argentina naye kanuna.

Ilikuwa habari kubwa zaidi Argentina kwa sababu wote watatu walikuwa Waargentina. Icardi, Lopez na Wanda wote ni Waargentina. Zaidi ni kwamba Lopez alikuwa mkubwa kwa Icardi na ni kama alikuwa amempokea katika soka la Italia.

IC 01

Mara mbili katika mechi za Inter Milan dhidi ya Sampdoria ambazo Lopez na Icardi walikutana uwanjani, Lopez aligoma kumpa mkono Icardi kitu ambacho kilibeba vichwa vya habari katika habari za michezo Italia na Argentina.

Inaelezwa kwamba kuanzia hapo Icardi hakuitwa tena katika kikosi cha timu ya taifa ya Argentina kwa sababu Messi alikuwa amechukia. Messi, mkubwa kama alivyo, ndiye ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa na ushawishi wa wachezaji wanaoweza kuitwa au kuachwa katika kikosi cha Argentina.

Hakumtaka tena Icardi huku akiamini kwamba kwa kufanya hivyo angemkera Lopez ambaye alikuwa ni rafiki wa karibu pia. Waargentina hawakuwa na haja na msaliti Icardi kwa sababu wakati huo walikuwa na kikosi ambacho kilikuwa kimesheheni mastaa.

IC 01 (1)

Pale mbele kulikuwa na kina Angel Di Maria, Gonzalo Higuain, Sergio ‘Kun’ Aguero, Carlos Tevez, Gabriel Millito, Martin Palermo na wengineo wengi. Habari ya Icardi ambaye alikuwa ameliudhi taifa ikafa kifo cha mende.

Katikati ya hili penzi la Icardi na Wanda ghafla Icardi akamfanya Wanda kuwa meneja wake. Pesa ikaendelea kubakia katika penzi. Wanda ndiye aliyesimamia dili la Icardi kwenda Inter Milan, kisha akasimamia dili la Icardi kwenda PSG na mwishowe kabisa akasimamia dili la kwenda Galatasaray ambako Icardi amekuwa akitamba sasa hivi. Walifanikiwa kupata watoto wawili huku penzi lao likiwa maarufu zaidi kutokana na umaarufu wa wote wawili. Achilia mbali kwamba Wanda alikuwa mzuri kwa sura na umbile lakini pia alikuwa mwandaaji maarufu wa vipindi vya televisheni.

Mapaparazi pia walikwenda nao kila mahala kwa sababu lilikuwa penzi maarufu pale Italia ambalo waandishi wa habari liliwakumbusha penzi la staa maarufu wa zamani wa timu ya taifa ya Italia, Francesco Totti na mrembo mwanamitindo, Hillary Blasi.

IC 03

Yapo mapenzi machache ya wanasoka yaliyowahi kupata umaarufu kama hivi. Ni kama vile pale England ilivyokuwa pia kwa David Beckham na Victoria Adams ‘Posh spice’. Au pale Hispania kulikuwa na penzi la Iker Casillas na Sara Carbonero.

Hapo katikati mahusiano ya Icardi na Wanda yakaanza kuyumba. Aliyeua kwa upanga naye anaweza kuuawa kwa upanda. Hatimaye kilekile ambacho Icardi alimfanyia Lopez ndicho ambacho na yeye amefanyiwa na staa wa kimataifa wa Senegal, Keita Balde. Icardi amejitokeza hadharani na kudai kwamba mke wake, Wanda Nara amemsaliti kwa kutoka kimapenzi na staa huyo wa Klabu ya Sivasspor ya Ligi Kuu ya Uturuki. Haishangazi sana kwa sababu wote wapo katika ligi moja ya Uturuki.

Lakini wala haishangazi zaidi kwa sababu kumbe na Balde naye alianza kumtamani Wanda zamani. Balde na Icardi wamewahi kucheza pamoja katika Klabu ya Inter Milan. Kama ambavyo Icardi alimtamani Wanda wakati akiwa anacheza pamoja na Lopez, basi ndivyo vivyo hivyo ambavyo Balde naye alianza kumtamani Wanda tangu wakati wakicheza pamoja Italia katika Klabu ya Inter Milan.

Na sasa talaka ipo mahakamani. Muda wowote kuanzia sasa talaka itatolewa. Nadhani Diego Maradona atatabasamu katika kaburi lake pale Buenos Aires. Nadhani Lionel Messi atakuwa anatabasamu katika Jiji la Miami pale Marekani. Nadhani itakuwa kicheko kikubwa kwa Waargentina walio wengi kwa sababu furaha yao kubwa ni kuona muosha ameoshwa.

IC 04

Lakini kama kuna mtu ambaye atakuwa na furaha zaidi katika hili basi ni Maxi Lopez mwenyewe. Anaweza kunywa kwa furaha iliyopitiliza baada ya kusikia kwamba Icardi naye amesalitiwa na mwanasoka mwingine. Kumbe Wanda ndivyo alivyo.

Afadhali kama Icardi angekuwa amesalitiwa na Wanda kupitia kwa mtu wa kada nyingine, lakini Mungu amemrudishia kulekule kwa mwanasoka mwenzake. Hivi ndivyo usaliti unavyoweza kufanya kazi. Wazungu huwa wanaita ‘karma’.

Badala la Wanda kuibuka na mwanasheria au mfanyabiashara, au muigizaji au msanii, yeye ameamua kuibuka na Balde. Hivi ndivyo ambavyo muosha huwa anaosha katika kipimo kilekile ambacho aliwahi kukipima awali.

Aliyeumia zaidi ni Icardi mwenyewe ambaye amepeleka mahakamani ushahidi wa namna ambavyo Wanda ametoka kimapenzi na Balde. Lakini na Wanda naye hajarudi nyuma ameonyesha namna ambavyo Icardi alikuwa analia warudiane. Ameonyesha meseji za Icardi akililia penzi lake na kutaka warudiane. Sijui atawatazamaje Waaregntina? Kweli muosha huoshwa. Tangu lini kunguru alifugika?