NYUMA YA PAZIA: Kobbie Mainoo alivyopanda lifti badala ya ngazi

ANAKUMBUKA Steven Gerrard wakati huo akiwa kinda. Namna alivyopewa funguo za gari na Paul Ince kwenda mjini kumnunulia kitu ambacho alikuwa amesahau. Alipigwa na butwaa kwa sababu alikuwa hajui kuendesha gari. Aliogopa hata namna ya kumwambia Ince alikuwa hajui kuendesha.

Wakati huo mpira ulikuwa umejaa wababe ndani na nje ya uwanja. Uwanjani wako bora, nje ya uwanja unalazimika kuwafutia viatu mastaa wa kikosi cha kwanza. Ulilazimika kuwa na kipaji cha ajabu kupenya katikati yao na kucheza nao pamoja.

Kuna vipaji maalumu ndivyo ambavyo vingeweza kupasua. Mfano? Pele. Miaka 17 tu alikuwa katika kikosi cha Brazil pale Stockholm, Sweden akitwaa Kombe la Dunia. Aliwezaje? Ni kwa sababu alikuwa na kipaji maalumu haswa.

Lakini siku hizi kuna watu wana bahati zao. Kuna makinda wanapenya kwa sababu ya timu zilizopo au makocha waliopo. Mikononi tunaye kinda wa Manchester United, Kobbie Mainoo. Miaka 18 tu yupo katika kikosi cha kwanza cha Manchester United.

Unajua kwa nini amepenya? Ni kweli ana kipaji maalumu, lakini ni kikosi gani cha kumzuia kupenya? Hakuna. Kama kinda ana kipaji maalumu kama Mainoo ni rahisi kwake kupenya Manchester United. Kwa basi hili la Man United ambalo safari moja shamba na nyingine gereji, kwa nini asipate nafasi yake?

Kama una wachezaji kama Antony katika kikosi chako kwa nini Mainoo asipenye? Maisha yangekuwa magumu kwake kama angekuwa katika kikosi cha Manchester City au Arsenal ya sasa. Kuna makinda wazuri katika timu hizi, lakini wanapata ugumu wa kuingia katika kikosi cha kwanza.

Cole Palmer alilazimika kuondoka zake Manchester City huku Pep Guardiola roho ikimuuma. Alimwambia wazi asingeweza kuwaweka nje Riyad Mahrez na Bernardo Silva. Palmer alilazimika kuondoka zake.

Kwa nini Mino Raiola alipata nafasi ya kumlaghai Paul Pogba aondoke Manchester United akiwa kinda? Kwa sababu alijua kwa wakati ule Sir Alex Ferguson asingeweza kumweka nje Paul Scholes ili ampatie nafasi Pogba.

Ni rahisi kumpa nafasi na kumkuza kinda katika timu ambayo inayumba. Kocha anapata kiburi kwa sababu wachezaji wanaoonekana kuwa wakubwa wanashindwa kumpa matokeo uwanjani. Wakati mwingine hata kocha halaumiwi na mashabiki kwa kumpa nafasi kinda.

Sawa, kuna makinda wanaopenya kwa sababu ya timu ya wakubwa kuwa na majeruhi wengi lakini kuna kama hawa kina Mainoo ambao wanapenya kwa sababu tu kuna wazembe wengi katika kikosi cha wakubwa ambao hawaonyeshi ubora wao kila wikiendi.

Mchezaji kama Bukayo Saka naye amenufaika na Arsenal iliyokuwa katika maisha magumu. Kama angekutana na Arsenal ile ya kina Robert Pires si ajabu angejikuta akiangukia katika timu nyingine au ingemchukua muda mrefu kuchukua nafasi yake.

Mtazame Phil Foden. Wote tulikuwa tunaona kipaji chake maridhawa lakini ilimchukua muda mrefu kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza cha Guardiola. Kwa nini? Kushoto kulikuwa na Raheem Sterling na Leroy Sane.

Alipoondoka Sane akaja Jack Grealish. Mpaka alipokomaa zaidi ndipo Guardiola akaruhusu Sterling aondoke na nafasi ikaenda kwa Foden ambaye bahati nzuri pia ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani kiasi kwamba alibahatika pia kwa kuondoka Mahrez. Kwa sasa ni mchezaji wa kutegemewa.

Nafahamu kwamba katika umri wa miaka 18 tu Foden alikuwa tayari kuingia katika vikosi vingi vya kwanza vya klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya. Ni rahisi kumkuza kinda katika klabu ambayo imesambaratika kama Manchester United.

Kina Mason Greenwood wamepitia humu humu. Marcus Rashford amepitia humu humu. Siku United ikisimama tena imara maisha yataanza kuwa magumu kwa makinda. Mainoo naye amepitia humu humu.Kwa hiki kipaji alichonacho kwa nini asicheze United hii? Ana ubora. Ana utulivu wa hali ya juu na ana uhakika na maamuzi yake. Bahati nzuri ameonyesha kitu zaidi kiasi cha kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya England. Amepata lifti nzuri kupitia ubovu wa United ya sasa.

Kama ingekuwa zamani ingemchukua muda mrefu kukifikia kikosi cha timu ya taifa ya England lakini United imempa lifti nzuri Mainoo ambaye angelazimika kupita barabara ndefu kama Manchester United ingekuwa kama Manchester City au Arsenal ya sasa.

Makinda kama yeye wapo katika vikosi vya timu kubwa lakini wanalazimika kupitia barabara ndefu kutokana na ukali wa vikosi vyao. Katika soka hili la kiushindani maisha yanakuwa magumu sana kwa kocha kumuamini kinda mdogo kama Mainoo wakati una kikosi kipana kilichojaza mastaa.

Nini kinafuata kwa Mainoo? United inalazimika kumfuata alipo. United inapaswa kusajili wachezaji bora lakini kuwa na kocha wa uhakika zaidi kuweza kutimiza malengo yake. Ni kama ambavyo Arsenal wamefanikiwa kwa Saka. Timu imeweza kumfuata alipo. Vinginevyo Saka angeweza kushawishika kiurahisi kwenda zake Manchester City au kwingineko ambako kuna timu zinazowania mataji.

Kwa suala la pesa Mainoo yupo sehemu salama. Haitapita muda mrefu United watamwongezea mshahara.Pia United ina uwezo mkubwa wa kupambana na timu ambazo zitamshawishi kipesa Mainoo. United ni matajiri.

Kilichobaki kwa sasa ni kupambana naye tu katika kuongezea wachezaji wa maana na kocha ambaye atamfanya ajisikie yupo katika timu sahihi kama Foden na Saka walivyofanywa kwa Guardiola na Mikel Arteta. Vinginevyo ni wazi Mainoo ni kipaji maalumu ambacho inabidi tushukuru kukiona kutokana na lifti nzuri aliyopanda wakati United ikiwa haieleweki.