NYUMA YA PAZIA: Ghafla tuna Newcastle United ya Mbappe na Halands

Sunday October 17 2021
HALAND PIC
By Edo Kumwembe

MARA ya mwisho kwao kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya England Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa na miaka mitano mnamo mwaka 1927. Mara yao ya mwisho kuchukua ubingwa wa England ilikuwa ni miaka tisa tu tangu kumalizika kwa vita ya kwanza ya dunia.

Nawazungumzia Newcastle United. Wametwaa mataji manne tu ya Ligi Kuu ya England, wametwaa mataji sita ya FA. Hata taji lao la mwisho la FA walitwaa zamani. Walitwaa miaka sita kabla Tanzania haijapata uhuru wake. ilikuwa mwaka 1955.

Kila kitu kinaweza kubadilika muda wowote kuanzia sasa. Matajiri kutoka Saudi Arabia wamefanikiwa kununua asilimia 80 ya hisa za Newcastle United. Tajiri wa Newcastle, Mike Ashley amekunja pauni 300 milioni ameweka katika akaunti yake moja Uswisi na nyingine Cyprus. Timu imeuzwa.

Na sasa kila kitu kitabadilika Newcastle. Kwanza kabisa nisiwe mnafiki. Niliombea hili litokee. Newcastle United walistahili mambo mengi. Timu ambayo imedumaa tu lakini wakati fulani walikuwa wanatoa changamoto kwa wakubwa.

Enzi hizo waliwahi kuwa na akina Alan Shearer, Rob Lee, David Ginola, Gary Speed, Nobert Solano na wengineo. Lakini zaidi nilipenda mambo mengine mawili kutoka kwao. Mashabiki majeuri na wanaoipenda timu yao maarufu kama Geordies.

Lakini pia uwanja wao wa St James Park. Kabla ya kujengwa kwa uwanja wa Emirates na kutanuliwa kwa viwanja kama Etihad, uwanja wa St James Park ulikuwa ni wa pili kwa ukubwa miongoni mwa viwanja vya Ligi kuu ya England ukiwa unachukua mashabiki 52,305. Wa kwanza ulikuwa Old Trafford na unabakia kuwa hivyo mpaka sasa na idadi yake ya mashabiki 76,962.

Advertisement

Na sasa kila kitu kinaenda kubadilika Newcastle. Wakubwa wengine wana hofu na wamepinga kweli kweli Newcastle kwenda kwa Waarabu. Hakuna cha kuwasaidia kwa sababu wanajua kwamba Newcastle inakwenda kuwa Manchester City nyingine.

Kuna timu zina matajiri kutoka Marekani kama Arsenal, Manchester United na Liverpool. Wanajua kwamba hawawezi matanuzi ya matajiri kutoka katika pesa za mafuta za Waarabu au Warusi. Tayari Roman Abramovich aliwahenyesha alipoichukua Chelsea mwaka 2003. Mpaka leo wanahenya kwa Roman.

Wanajua jinsi gani ambavyo City wanawahenyesha tangu walipopata pesa za mafuta. Na tunapozungumza ni wazi kwamba City ni mabingwa wa Ligi Kuu ya England huku Chelsea wakiwa ni mabingwa wa Ulaya. Huwa haiji hivi hivi.

Kinachofuata kwa sasa unaweza kusikia Kylian Mbappe anabadilisha upepo na kutakiwa na Newcastle United. Unaweza kusikia Erling Haaland anabadilisha upepo na kutaka kwenda zake Newcastle United. Kipi bora kuliko pesa? Aliwahi kuuliza James Hadley Chase.

Newcastle itaanza kuajiri watu wajanja waliokubuhu katika nafasi mbalimbali za kiutendaji. Ni watu hao hao ndio wana namba za akina Mino Raiola, Kia Joorabchian, Jorge Mendes na wengineo. Hawa ndio wanaomiliki wachezaji wa maana katika sayari ya sasa.

Baada ya hapo nini kinafuata? Kununua mastaa kwa bei mbaya na kulipa mishahara mikubwa mastaa. Tatizo pekee kwa sasa linaweza kuwa katika upande wa makocha. Chelsea walikuwa na bahati kumpata Jose Mourinho akiwa wa moto.

Manchester City walipata bahati kumpata Pep Guardiola akiwa wa moto na mpaka sasa ameendelea kuwa wa moto. Kocha gani mwingine wa moto yupo sokoni? Zinedine Zidane? Sijawahi kumkubali licha ya kuchukua mataji matatu ya Ulaya akiwa na Real Madrid.

Antonio Conte? Inawezekana wakamchukua kwa sababu Conte siku zote ni mshindi. Tatizo ni kwamba sijui kama watataka soka la aina gani. Conte ni mshindi lakini hajawahi kutoa soka la kuvutia sana kama ilivyo kwa Pep na Jurgen Klopp.

Hata hivyo kwa yeyote ambaye atachukua kiti hicho ajiandae kuondoka muda wowote ule pindi wakati timu haipati matokeo. Wenye pesa zao wanawekeza kwa wachezaji wa maana na wanataka matokeo ya moja kwa moja.

Kitu kingine ambacho kipo wazi ni kwamba matajiri wapya wa Newcastle lazima watatanua uwanja wa St James Park na kuongeza idadi kubwa ya watazamaji. Ni kitu ambacho tayari matajiri wa Manchester City walishakifanya walipoinunua City.

Awali uwanja wa Etihad ambao ulikuwa ukitambulika kama Maine Road ulikuwa unaingiza mashabiki 47,400 lakini sasa wameutanua na unaingiza mashabiki 53,400. City pia wamejenga eneo la kisasa zaidi la mazoezi (complex) ambayo haina mfano wake barani Ulaya.

Vyovyote ilivyo hii sio habari nzuri kwa baadhi ya timu kubwa na ndogo barani Ulaya. Kuna wale wakubwa ambao lazima wajue wazi kwamba kuna wapinzani wakubwa wa kununua majina makubwa wameingia mjini.

Ni kama ambavyo kuna wachezaji wakubwa duniani wameishia kucheza timu kama Manchester City na PSG lakini ambao zamani wangeweza kuishia kucheza Barcelona, Real Madrid, Manchester United na AC Milan.

Mastaa kama Kelvin de Bruyne, David Silva, Sergio Kun Aguero, Marco Verrati na wengineo wengi wangeweza kuishia katika klabu kubwa kama hizi enzi zao lakini wamejikuta wameishia Manchester City na PSG.

Newcastle wanakuja kulivuruga soko zaidi na si tu kwamba itawapeleka wao juu lakini pia itaendelea kuwaacha rafiki zangu Arsenal na Manchester United wakiwa hoi pale katika Ligi Kuu ya England. Baada ya kuondoka kwa Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger sio tu kwamba wakubwa hawa wameyumba katika suala la mabenchi ya ufundi, lakini pia hawana jipya katika mvuto wa mastaa na pia ugomvi wa kununua mastaa. Wakati huu mastaa wakichagua kwenda City na Chelsea kwa sababu ya pesa na mafanikio, ndio kwanza Newcastle wanakuja hadharani kuongeza tatizo jingine la ndani na nje ya uwanja kwa timu hizi mbili ambazo wakati fulani zilibaki mbili tu zikitamba England.

Advertisement