Prime
NYUMA YA PAZIA: Vitinha, mtoto wa 2000 anayesumbua starehe za watu

Muktasari:
- Dunia ilipogeuka kuingia milenia mpya huku tukiwa na hofu ya kuzimika kwa mitandao na kompyuta, wao ndio wakaanza kuzaliwa. Fikiria mtoto aliyezaliwa 2000 tayari sasa hivi ameshafikisha miaka 25. Nyakati zimekwenda wapi? Na sasa tunao watoto maarufu wa 2000 ambao wanasumbua kila mahala.
WAMEJAA kila mahala. Wamejaa katika kumbi za starehe kwa sasa. Wamejaa kila mahala. Mara ngapi umewahi kusikia namna tunavyowazungumzia watoto waliozaliwa mwaka 2000 kuja juu? Ni wasumbufu. Wana bughudha. Jeuri na hawaelewi lolote.
Dunia ilipogeuka kuingia milenia mpya huku tukiwa na hofu ya kuzimika kwa mitandao na kompyuta, wao ndio wakaanza kuzaliwa. Fikiria mtoto aliyezaliwa 2000 tayari sasa hivi ameshafikisha miaka 25. Nyakati zimekwenda wapi? Na sasa tunao watoto maarufu wa 2000 ambao wanasumbua kila mahala.
Uwanjani pale PSG watoto wa 2000 wana mwakilishi wao. Wana mtoto wa 2000 ambaye anasumbua starehe za watu, lakini yeye anasumbua uwanjani. Vitor Machado Ferreira. Utotoni huko kwao Ureno walimuita Vitinha. Alizaliwa siku moja kabla dunia haijaadhimisha siku ya wapendanao 2000. Februari 13, 2000.
Umemuona Vitinha uwanjani? Ujeuri wote wa PSG upo katika mapafu yake. Aliwateketeza Liverpool pale Parc des Princes katikati ya Jiji la Paris. Bahati mbaya PSG walilala kwa bao la 'kichawi' la dakika za mwisho la Liverpool. Akaona haitoshi. Akawateketeza tena Anfield. Ikawa siku nzuri kwao na wakapata tiketi ya kusogea Jiji la London kucheza na Arsenal.

Jumanne usiku Vitinha alikuwa London akisambaza upendo katika eneo la kiungo. Alipambana kwelikweli kuwafunika kina Martin Odegaard na alifanikiwa. Inasemwa labda aliweza kwa sababu Thomas Partey alikuwa nje. Hatujui. Tutaona Jumatano ijayo pale Paris.
Mpira wa kisasa unahitaji watu walio bora wakiwa na mpira na wasipokuwa na mpira. Uzuri kimo cha Vitinha kinakupa mnyumbuliko. Wachezaji kama yeye wanapoamua kujituma au wanapojengwa na hulka ya kujituma, basi mpira wa kisasa unawafaa kwelikweli. Anaingia hapa, anatokea pale, anatokea pale anaingia hapa. Ghafla anajikuta mchezaji aliyekimbia kilomita nyingi uwanjani kuliko yeyote yule.
Aina ya Vitinha ni mchezaji anayecheza kwa nafasi zaidi. Hagusani sana kwa sababu hata akigusana hana ubavu wa kupambana na Casemiro. Anahitaji kunyumbulika na kucheza kwa nafasi. Kuziba nafasi au kufungua nafasi kwa muda mrefu wa mchezo.
Inakukumbusha nani? Thierry Henry anadai kwamba Vitinha anamkumbusha Andres Iniesta na Xavi Hernandez. Hauwezi kumkatalia. Wao ndio walikuwa nguzo eneo la kiungo wakati dunia inaingia katika mpira wa kisasa. Mpira wa kina Pep Guardiola. Ukitaka kufanikiwa inabidi ucheze kama wao. Gusa achia, gusa achia. Usipokuwa nao unakaba kama kivuli.

Kuanzia hapo tulipoanza kumuelewa Pep na viungo wa namna hii ndipo ukawa mwisho wa viungo wa nakshi. Sio kwamba tuliwatamkia kwamba hatuwataki, hapana. Mpira wenyewe ndio uliwakataa. Mpira ukawa unachezwa kwa haraka unapokuwa nao na usipokuwa nao. Muda wa kanzu, tobo, chenga, ukatoweka. Labda ndio maana kuna watu wanalalamika kwamba mpira umeondoka katika ladha ya mchezaji mmoja mmoja.
Tunalalamika kwamba hatuwaoni tena viungo kama kina Ronaldinho, Zidane, Andrea Pirlo na wachezaji wengine wa aina hii. Ukweli ni kwamba muda wa kufanya mambo mengi uwanjani haupo tena. Inabidi tupasiane kwa haraka kwenda kwao. Inabidi wote tukabe kwa pamoja na sio kumuachia Javier Mascherano au Patrick Vieira akabe peke yake.
Na sasa kuna mtoto wa 2000 kama Vitinha. Wenzake wanafanya vurugu baa na klabu za usiku wakisumbua watu wazima. Yeye anafanya uwanjani. Vitinha ana ufundi mwingi na wa haraka akiwa na mpira. Kwa maana ya kuuchezea kwa haraka na kutoa pasi kabla ya kufungua nafasi nyingine. Anafanya timu yake ionekane ina wachezaji 12 uwanjani achilia mbali kipa.

Vitinha pia anakaba kama kivuli. Inamaanisha anakuwa bora pia akiwa hana mpira. Popote mpira ulipo uwe wa timu yake au wa adui yeye anakuwa mita chache kutoka mpira ulipo. Haya ndio mapafu ya mbwa yaliyowaua Liverpool pale Parc des Princes na Anfield. Ndio mapafu ambayo Arsenal pia walihangaika nayo.
Kitu ambacho kitakushangaza ni ukweli kwamba Vitinha alicheza Wolves kwa mkopo 2020 hadi 2021. Kwanini haukuona uhodari wake? Wakati mwingine inatokana na timu kutocheza kwa mfumo ambao unamfaa. Ndio maana Xavi na Iniesta walikuwepo katika Barcelona ya Frank Rijkaard, lakini hawakuwa mastaa wakubwa kama Ronaldinho, Samuel Etoo na Deco.
Alipokuja Pep ndio akawanyanyua kuwa mastaa wakubwa kwa sababu waliingia katika mfumo wake na kuumudu. Ni kama Vitinha alivyoingia katika mfumo wa Luis Enrique. Si ajabu akaenda timu nyingine akaonekana mchezaji wa kawaida kama alivyokuwa Wolves. Inabidi mcheze katika staili ambayo timu nzima inajua inachotaka ikiwa na mpira na isipokuwa na mpira.

Enrique ameliweza hili baada ya kuivunja PSG yenye mastaa kina Kylian Mbappe, Neymar na Lionel Messi. Amechukua wachezaji mahiri wa daraja la kati ambao wapo tayari kuutumikia mfumo na wanaongozwa na mapafu ya Vitinha. Mpira wa kisasa ndivyo unavyohitaji. Unahitaji zaidi wachezaji wenye mapafu ya kuutumikia mfumo kuliko kujitumikia wenyewe.
Ni kama ambavyo tuliona Real Madrid yenye mastaa kina Vinicius Junior, Mbappe, Jude Bellingham na wengineo walivyotolewa nishai na Arsenal iliyocheza kitimu zaidi chini ya Mhispaniola Mikel Arteta. Hata ile Madrid ya Galacticos ya kina David Beckham, Ronaldo de Lima, Luis Figo, Zinedine Zidane nayo ilikuwa inatolewa nishai hivihivi.
Siku ambayo Madrid inaweza kwenda katika mikono ya kocha kama Xabi Alonso ndipo tutakaposhangaa kwamba anaweza kuruhusu mauzo ya wachezaji wenye majina makubwa kwa sasa pale Santiago Bernabeu kwa ajili ya kupisha wachezaji wenye mapafu kama Vitinha. Tatizo Florentino Perez anapenda wachezaji wanaouza jezi kuliko wachezaji wa aina hii ya Vitinha.
Hatujui mpira huu wa kina Vitinha utaisha lini. Hatujui kama mpira wa kina Zidane utarudi tena. Kwa sasa tunaendelea kufurahia shoo za kina Vitinha kwanza katika mpira mpya. Wazungu huwa wanasema 'enjoy while it lasts'. Na uzuri wake ni kwamba walau kwa sasa tunapata nafasi ya kujifunza kuwajua wachezaji muhimu zaidi uwanjani hata kama hawafungi mabao.

Ni kama wakati ule tuliposhtuka kwamba licha ya ubora wa Messi, lakini timu ya Barcelona ilikuwa haiendi bila ya utatu wa Xavi, Iniesta na pweza wa Catalunya, Sergio Busquets. Ndivyo ambavyo leo PSG inaweza kusonga mbele bila ya Ousmane Dembele, lakini ikakwama kwa kucheza bila ya Vitinha na Joao Neves. Ukweli mchungu katika soka.