Liverpool haijamaliza EPL 2024/25

Muktasari:
- Mechi zilizobaki, itakipiga na Chelsea, kisha Arsenal uwanjani Anfield, kabla ya kukipiga na Brighton na kumalizia na Crystal Palace. Hizo ni mechi ambazo zitakuwa kama mtoko kwa mashabiki wa Liverpool, kwa sababu hawatakwenda uwanjani na presha ya kupoteza.
LIVERPOOL, ENGLAND: MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu England zimeshafika kikomo na sasa ni kutafuta heshima tu. Liverpool imebakiza mechi nne kwenye Ligi Kuu England msimu huu na hakika hizo ni mechi ambazo zitakuwa na burudani kubwa kwa mashabiki.
Mechi zilizobaki, itakipiga na Chelsea, kisha Arsenal uwanjani Anfield, kabla ya kukipiga na Brighton na kumalizia na Crystal Palace. Hizo ni mechi ambazo zitakuwa kama mtoko kwa mashabiki wa Liverpool, kwa sababu hawatakwenda uwanjani na presha ya kupoteza.
Hata hivyo, kwa Kocha Arne Slot na wachezaji wa Liverpool bado kuna kitu wanakitafuta katika mechi hizo nne zilizobaki. Bado inahitaji ushindi kwenye mechi hizo, kwanza kuweka rekodi sawa na pointi watakazokuwa wamebeba mwisho wa msimu ili kutengeneza msingi wa kuanzia hapo kwa ajili ya msimu ujao.
Kitu kingine, kocha Slot atatumia mechi hizo kuwapa nafasi wachezaji wake wote kucheza ili kuwa na ufahamu wa mwisho nani abaki na nani afunguliwe mlango wa kutokea wakati dirisha la usajili litakapofunguliwa mwezi ujao.
Ukiweka kando mpango huo wa kocha Slot kwenye matumizi ya mechi hizo kumpa taswira ya mchezaji gani wa kubaki au kuondoka na mchezaji gani wakupewa nafasi kubwa kwenye kikosi kwa msimu ujao sambamba na wengine kuwasaidia kuweka rekodi zao kwenye ubora mkubwa msimu huu, haya hapa ni mambo mengine Liverpool inayasaka kwenye mechi hizo zilizobaki licha ya kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu England kwa msimu huu.
1. Kusaka rekodi ya pointi
Hiki ni kitu muhimu zaidi kwenye mpango wa Slot na wachezaji wa Liverpool. Miamba hiyo ya Anfield ilifikisha pointi 82 wakati ilipoichapa Tottenham Hotspur, Jumapili iliyopita na kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa msimu huu na bado ina mechi nne muhimu za kufukuzia pointi 12.
Hiyo ni nafasi muhimu kwao kuvuka pointi 90 kwa msimu wa nne kati ya saba (97 msimu wa 2018-19, 99 msimu wa 2019-20, na 92 msimu wa 2021-22), kitu ambacho kitatengeneza desturi ya wachezaji wa kikosi hicho kukipambania.

2. Kumsaidia Mo Salah kuweka rekodi zaidi
Wachezaji wote kwenye kikosi cha Liverpool hawatahitaji kuelezwa hili kwa sababu Mohamed Salah atawafanya wafahamu zaidi. Staa huyo wa Misri kwa sasa ndiye mchezaji wa kigeni aliyefunga mabao mengi kwenye historia ya Ligi Kuu England, huku akishikilia pia rekodi ya kuhusika kwenye mabao mengi (kufunga + kuasisti) katika msimu wa mechi 38 na ameshahusika na mabao 46, ambayo bado ana nafasi ya kuongeza zaidi. Hiyo ni kwa sababu mabao 47 yalifikiwa na Andy Cole msimu wa 1993-94 na Alan Shearer msimu wa 1994-95, huku misimu hiyo yote ilikuwa ya mechi 42.
3. Kuweka msingi wa kuanzia msimu ujao
Kuna kipindi ndani ya msimu huu ilidhaniwa mechi ya Liverpool na Arsenal ndiyo ingetoa taswira ya ubingwa, lakini miamba hiyo ya Anfield ilitumia faida ya wapinzani wao hao kuteleza na kuweka pengo kubwa la pointi lililowafanya kutangaza ubingwa mapema.
Sasa Arsenal itakuwa na kibarua cha kukabiliana na PSG, Jumatano ijayo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kabla ya kwenda Anfield kucheza na Liverpool, Mei 11, mechi ambayo wenyeji watacheza bila ya presha yoyote, kwa sababu ni mabingwa tayari.
Lakini, kwa heshima, Liverpool itahitaji kushinda mechi hiyo ili kuwaonyesha Arsenal wao wapo tayari hata kwa vita ya kuwania ubingwa wa msimu ujao.

4. Kufunga bao kwenye mechi zote za ugenini
Liverpool mpango wao ni kufanya kitu ambacho hakijawahi kufanywa na klabu yoyote kwenye Ligi Kuu England huko nyuma na kikosi hicho cha Slot kipo kwenye nafasi nzuri ya kulitimiza hilo. Kama Mo Salah na wenzake watatikisa nyavu kwenye mechi za ugenini huko Chelsea na Brighton, hapo itakuwa imeweka rekodi ya kufunga bao katika mechi zote ilizocheza ugenini kwenye ligi hiyo msimu huu na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufanya hivyo kwenye historia ya Ligi Kuu England. Hivyo, mechi nne ilizobakiza Liverpool ili msimu huu kufika mwisho, hazitakuwa za bonanza tu kwao.
5. Kumpa Conor Bradley mechi za kumwongezea uzoefu
Ikifahamika Trent Alexander-Arnold anaelekea kwenye mlango wa kutokea kwenye klabu hiyo ya Anfield na kama hilo litatimia, basi Liverpool italazimika kutafuta beki mwingine wa kulia kwenye kikosi hicho kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Na kama hilo ni hivyo, basi beki mpya wa kulia, ambaye anaweza kuaminika kwenye eneo hilo ni Conor Bradley, ambaye alikosa mechi ya Spurs kutokana na kuwa majeruhi, lakini alirejea mazoezini, hivyo pengine atakuwa fiti kucheza mechi zilizobaki. Bradley anaweza kupewa nafasi kama kipimo cha kukutana na mawinga wasumbufu kutoka kwenye timu zote nne itakazokutana nazo Liverpool kwenye ligi kutoka sasa.

6. Kufunika mabao ya Klopp ya msimu wa 2019-20
Inafahamika wazi Liverpoool ubingwa wake wa 2019-20 ulikuja kwenye kipindi cha janga la Uviko 19, hivyo ligi iliporejea na kuchezwa ilishuhudia viwanja vikiwa havina mashabiki, lakini ilifanikiwa kufunga mabao 85 katika msimu huo ikiwa chini ya kocha Mjerumani, Jurgen Klopp. Lakini, Liverpool hii ya Slot inaelekea kufukia mabao hayo ambayo yalifungwa na fowadi matata kabisa ya Liverpool kwa wakati huo iliyokuwa na wakali Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino. Hadi sasa, Liverpool imefunga mabao 80 katika mechi 34, hivyo ina nafasi kubwa ya kupiku mabao hayo ya msimu ambao Klopp aliipa taji la Ligi Kuu Liverpool. Liverpool ile ya Klopp iliruhusu mabao 33, ikiwamo 12 katika mechi tisa ambazo zilichezwa bila ya mashabiki, wakati hii ya Klopp imesharuhusu mabao 32.
7. Kumsaidia Ryan Gravenberch kufunga bao
Agosti mwaka jana isingekuwa rahisi kufikiria kwamba Ryan Gravenberch atafika Mei akiwa ameanza kwenye kila mechi ya Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Liverpool, lakini ndiyo hivyo kilichotokea ni kama kwa mastaa Virgil van Dijk na Salah, ambao wamecheza kwenye kile mechi, 34 zilizochezwa hadi sasa. Mdachi huyo amekuwa akifanya vizuri sana kwenye kiungo Namba 6, akicheza mechi 46 katika michuano yote na kuwa msingi imara wa ubingwa wa timu hiyo kwa msimu huu. Lakini, kitu kimoja hakufanya, kufunga bao. Gravenberch amekuwa mvivu kupiga mashuti ya mbali na amekuwa hasogei sana kwenye lango la wapinzani, kitu ambacho kimemfanya ashindwe kufunga bao lolote kwenye ligi hadi sasa. Na sasa anaweza kutumia mechi nne zilizobaki, kutafuta bao walau moja.

8. Kuwafanya mastraika kwenda mapumziko wakijiamini
Gravenberch hajafunga bao na si Diogo Jota au Darwin Nunez waliofunga mabao kwa idadi kubwa kama ambavyo walihitaji kufanya hivyo msimu huu. Hakuna mshambuliaji aliyefikisha tarakimu mbili ya mabao ya kufunga msimu huu (Jota 9, Nunez 7), licha ya kwamba walikuwa wachezaji muhimu katika kuisaidia timu kubeba ubingwa na Jota alifunga bao muhimu la kusawazisha dhidi ya Nottingham Forest na la ushindi kwenye Merseyside derby, wakati Nunez alifunga mabao mawili ya dakika za mwisho dhidi ya Brentford. Na washambuliaji wengine, Luis Diaz na Cody Gakpo nao pia watahitaji mechi zilizobaki katika kumalizia msimu wanazitumia vyema ili kujiweka kwenye wakati mzuri kabla ya kwenda mapumziko ya mwisho wa msimu.
9. Kumpa Federico Chiesa hadhi ya kuwa bingwa kamili
Majeraha mfululizo yamemfanya Federico Chiesa kucheza dakika 33 tu kwenye Ligi Kuu England katika mechi nne alizopewa nafasi na sasa ndiyo hivyo, timu yake imechukua ubingwa wa ligi hiyo. Na kanuni za Ligi Kuu England, ili kuwa bingwa rasmi, mchezaji anahitaji kucheza mechi tano kwenye ligi ili afanikiwa kupata medali ya ubingwa huo na ili staa huyo Mtaliano afikie kigezo hicho, atahitaji kucheza kwenye mechi hizo zilizobaki ili kuwa mmoja wa mabingwa kamili waliosaidia Liverpool kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England kwa msimu huu. Bila shaka, Liverpool itampa nafasi Chiesa ya kutimiza ndoto hiyo.

10. Kulinda rekodi za Wataru Endo kwa nguvu zote
Alisherehekea sana Jumapili iliyopita na hakika alikuwa na sababu ya kufanya hivyo. Kiungo, Wataru Endo amehusika kwenye nusu ya mechi 34 ilizocheza Liverpool msimu huu. Katika mechi hizo 17 alizocheza zote alianzia kwenye benchi, ambako kocha Slot alikuwa akimtumia Mjapani huyo kama mtu wa kuja kuongeza nguvu na kuipa timu makali mapya mchezoni kitu ambacho kilileta matunda mazuri. Na jambo hilo lilimfanya Endo kuweka rekodi bora kabisa za wachezaji ambao hawakuhusika kwenye faulo nyingi. Na kwa kutokuwa muda mrefu ndani ya uwanja kumfanya mchezaji huyo pia asionyeshwe kadi ya njano hata mara moja, kitu ambacho Liverpool bila shaka watahitaji kukilinda ili kumtengenezea rekodi safi kiungo huyo wa Kijapani.