NYUMA YA PAZIA: Enzo pekee alivyowakausha La Liga na majirani zao
JINSI dunia inavyoshangaza. Jinsi maisha yanavyokwenda kasi. Unaweza kuamini? Kuanzia mwaka 1984 mpaka 1992 wanasoka ghali zaidi duniani walikuwa wameuzwa kwenda Italia. Katika kipindi hicho wanasoka sita walikuwa wamehamia timu za Italia na kuwa wanasoka ghali zaidi duniani.
Kuna ambao walikuwa wametokea nje ya Italia, na kuna ambao walitokea ndani ya Italia. Mwaka 1984 Diego Maradona alitoka Barcelona kwenda PSV kwa dau la Pauni 5 milioni. Mwaka 1987 Ruud Gullit alitoka PSV kwenda AC Milan kwa dau la Pauni 6 milioni. Mwaka 1990 Roberto Baggio alihama kutoka Fiorentina kwenda Juventus kwa dau la Pauni 8 milioni.
Jean Pierre Papin alitoka Marseille kwenda AC Milan kwa Pauni 10 milioni akavunja rekodi ya uhamisho wa dunia mwaka 1992. Mwaka huohuo, Marehemu Gianluca Vialli alikuwa ametoka Sampdoria kwenda Juventus kwa dau la Pauni 12 milioni. Akavunja rekodi ya uhamisho ya dunia. Mwaka huohuo Gianluigi Lentini akatoka Torino kwenda AC Milan kwa Pauni 13 milioni.
Hizi zote zilikuwa rekodi za uhamisho za dunia. Walikuwa wameiweka dunia mkononi. Baadaye mbele ya safari Ronaldo de Lima, Christian Vieri na Hernan Crespo wakarudi tena kuvunja rekodi za uhamisho wa dunia wakiwa Italia. Ilikuwa mwishoni mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Kuanzia hapo hapo wakaja Wahispaniola. Alikuwa ni Fiorentino Perez na genge lake la wahuni ambao walituletea sera za Galacticoz. Kuanzia mwaka 2000 mpaka mwaka 2013 kulikuwa na wachezaji watano waliovunja rekodi ya uhamisho wa dunia huku wote wakielekea Santiago Bernabeu.
Luis Figo, Zinedine Zidane, Kaka, Cristiano Ronaldo na Gareth Bale wote walielekea zao Real Madrid kwa kishindo kikuu. Wakati wote huo Waingereza walikuwa hoi. Mara ya mwisho kwao kuvunja rekodi ya uhamisho wa dunia kabla ya nguvu hizi za Waitaliano na Wahispaniola ilikuwa mwaka 1996 wakati Alan Shearer alipohama kutoka Blackburn Rovers kwenda Newcastle United.
Maisha yamekwenda na dunia imegeuka. Tunaendelea kushuhudia unyonge wa wengineo dhidi ya Waingereza kwa sasa. Majuzi nilisikia rafiki zangu wa La Liga wakilalamika kwamba Waingereza wamekuwa na matumizi yasiyo ya kawaida katika soka.
La Liga huwa wanajiona ni wapinzani wakubwa kwa Waingereza ndani na nje ya uwanja. Lakini hapana shaka katika miaka ya karibuni wamekuwa wakipigwa na kitu kizito na Waingereza. Upepo umegeuka na sasa hivi wamekuwa wakilialia.
Kwa mfano, dili la kiungo wa kimataifa wa Argentina, Enzo Fernandez limekaribia kulingana na gharama za uhamisho za wachezaji wote walionunuliwa katika Ligi za La Liga, Bundesliga na Serie A. Enzo ameigharimu Chelsea Pauni 110 milioni ambacho kimevunja rekodi ya uhamisho wa wachezaji ndani ya England.
Wakati huohuo La Liga imetumia Pauni 25 milioni, Serie A imetumia Pauni 25 milioni na Bundesliga imetumia Pauni 60 milioni. Hii ina maana hizi ligi tatu kwa ujumla zimetumia kiasi cha Pauni 120 milioni wakati Enzo pekee ameigharimu Chelsea kiasi cha Pauni 110 milioni.
Hapa ndipo La Liga inapojihisi imezidi kuachwa mbali na Waingereza. Kwa ujumla katika dirisha hili tu la Januari ambalo timu haziwi bize kununua mastaa Waingereza kwa ujumla wao wamenunua wachezaji kwa dau la Pauni 810 milioni wakati La Liga imetumia Pauni 25 milioni tu.
Zaidi kumbuka kwamba timu nyingi kubwa hazikuamua kuingia sokoni kwa nguvu. Manchester United iliamua kuchukua wachezaji wa mkopo wakati Arsenal haikutaka kwenda mbali zaidi kwa Moises Caicedo. Nadhani Waingereza wangeweza kutumia dola bilioni moja kwa dirisha la Januari tu.
Hapa La Liga imepata hofu. Kikubwa zaidi ni kwamba mastaa wa enzi zile hawaendi tena kwao. Kylian Mbappe aliigomea Real Madrid katika dakika za majeruhi kabisa na kuamua kubakia PSG. Hii ilitokana na nguvu ya pesa.
Lakini hapohapo kumbuka mshambuliaji, Erling Haaland aliamua kutua katika Ligi Kuu ya England kuichezea Manchester City. Zamani ingekuwa rahisi kwenda Hispania. Kwa sasa dunia inawatazamia mastaa wawili tu wakubwa ambao walipaswa kucheza Hispania kwa ulazima mkubwa kama tungekuwa tunaishi zama zile. Haaland na Mbappe.
Kuna mambo mawili hapa. Kwanza kuna pesa za Waarabu ambazo zimesababisha hali kama hiyo. Waarabu wa Paris wamebaki na Mbappe wakati Waarabu wa Jiji la Manchester wamebakia na Haaland. Lakini vilevile Waingereza wanapata pesa nyingi kutoka katika haki za mauzo ya televisheni.
Kuna wachezaji wa timu kubwa kutoka ligi mbalimbali wamekuwa wakitiririka katika timu za kawaida tu za England. Kwa mfano, pale Italia mmoja kati ya wachezaji ambao wamekuwa wakisifika katika soka lao ni staa wa Roma, Nicolo Zaniolo.
Wakati ukitazamiaa Zaniolo angeweza kutakiwa na klabu kubwa za England kama vile Manchester United, Manchester City, Chelsea, Liverpool au Arsenal kumbe ndio kwanza alikuwa anahusishwa kutua zake Bournemouth.
Hatujui mpaka lini lakini kwa sasa Waingereza wamepindua meza vibaya. Rafiki zangu Waitaliano ambao walitamba kwa matanuzi ya pesa miaka ya 1990 sasa wapo hoi. Wachezaji wanaowapata ni wale ambao hawatakiwi katika soka la Kiingereza. Hawa ndio kina Romelu Lukaku, Tammy Abraham, Chris Smalling na wengineo. Muda si mrefu wanaweza wakawa na Harry Maguire pia.
Ukiona mchezaji anakwenda Italia kwa sasa ujue hajagombaniwa na timu za England wala Hispania. Vinginevyo Italia linakuwa chaguo la tatu. Kuna mambo mawili yanaweza kutokea. Nadhani nguvu ya ndani ya uwanja katika soka la Kiingereza itazidi kwenda juu.
Na hii itasababisha Ligi yenyewe iendelee kuwa na mvuto na hivyo kuendelea kuvutia wawekezaji huku pia ikiendelea kupata masoko katika masuala ya haki za televisheni.
Nadhani haya ndio mambo ambayo Wahispania yamewafanya watokwe na povu. Bado tegemea dirisha gumu kwa Wahispaniola mwishoni mwa msimu huu.