NYUMA YA PAZIA: Arteta anawamezea mate nyota hawa

Muktasari:

  • Hata hivyo, kwa sasa Kocha Arteta bado anataka kushusha vyuma vingine ili kuifanya Arsenal kuwa tishio baada ya msimu uliopita kushindwa kubeba taji la Ligi Kuu England mbale ya wababe Manchester City.

LONDON, ENGLAND: Dirisha la usajili limeendelea kunoga Ulaya. Vita ya usajili ni kubwa na kila timu ina rada zake. Arsenal tayari imeshamsajili jumla kipa David Raya baada ya kuidakia kwa mkopo akitokea Brentford.

Hata hivyo, kwa sasa Kocha Arteta bado anataka kushusha vyuma vingine ili kuifanya Arsenal kuwa tishio baada ya msimu uliopita kushindwa kubeba taji la Ligi Kuu England mbale ya wababe Manchester City.

Hapa kuna haya majina matano ya nyota na maelezo ya kina juu ya viwango vyao na uwezekano wa kutua washika bunduki hao wa London.


Riccardo Calafiori

Alionyesha kiwango bora akiwa na Bologna ya Ligi Kuu England na kwenye fainali za Euro 2024 za Ujerumani akiwa na timu ya taifa ya Italia.

Ni mmoja wa mastraika wanaohusudiwa sana na Kocha Arteta na yuko kwenye hatua nzuri ya kutua kwenye kikosi hicho msimu ujao na tayari nyota huyo (22) ameshakubaliana na Arsenal mambo binafsi na anachosubiri ni klabu hiyo imalizane na Bologna.

Nyota huyu ambaye Arsenal itatakiwa kulipa Pauni 42 milioni ili kumnasa, pia alikuwa akihusishwa na Chelsea na Liverpool.

Msimu uliopita Bologna ilifuzu kucheza Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu 1964 baada ya kumaliza nafasi ya tano katika Serie A.


Nico Williams

Kiwango chake msimu uliopita akiwa na Athletic Bilbao na  moto anaoonyesha Ujerumani kwenye fainali za Euro 2024 akiwa na Hispania zimemfanya kuwindwa na timu kubwa za nchini kwake na England.

Arsenal ni moja ya timu hizo na staa huyu anapatikana kwa Pauni 46.5 milioni, kiasi kilichowekwa katika mkataba wake kwa timu itakayomhitaji.

Mwenyewe alizungumzia kuhusu tetesi za kutakiwa na timu vigogo na kusema kwa sasa anachofikiria ni Euro 2024 na baada ya hapo mengine yatafuata.


Victor Osimhen

Arsenal kwa sasa inatafuta straika kwani ni eneo ambalo Kocha Arteta alilibainisha lina mapungufu na lilichangia timu hiyo kupoteza ubingwa msimu uliopita.

Straika huyu wa Napoli kuna kila dalili akaondoka Italia na mwenyewe aliwahi kusema anataka kucheza Ligi Kuu England.

Mbali na Arsenal kumuwinda, Chelsea na Barcelona pia zinampigia hesabu nyota huyu aliyeisaidia Napoli kubeba taji la Ligi Kuu ya Italia msimu wa 2022/23 huku akiweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Afrika kuwa mfungaji bora kwenye Serie A.

Pia inaelezwa anataka kucheza michuano mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya Napoli kushindwa kufuzu.


Joan Garcia

Kipa huyu kutoka Espanyol amekuwa akitajwa anaweza kutua Arsenal kuchukua nafasi ya Aaron Ramsdale anayehitaji kuondoka kwa sababu hapati nafasi kubwa ya kucheza kikosi cha kwanza.

Garcia (23), alionyesha kiwango bora msimu uliopita na aliisaidia Espanyol kupanda Ligi Kuu kupitia mtoano.

Katika mkataba wake, kuna kipengele kinachoeleza timu inayohitaji kuuvunja itatakiwa kutoa Pauni 21.2 milioni.

Kipa huyu atakuwa sehemu ya kikosi cha Hispania kitakachokuwepo jijini Paris kwa ajili ya Olimpiki, hivyo kama makubaliano hayatafanywa haraka, basi mpango huo utalazimika kusitishwa hadi Agosti 11 na michuano hiyo itakuwa imemalizika.

Ikiwa Garcia atatua Arsenal washika mitutu hao watakuwa na makipa wawili kutoka Hispania baada ya kukamilisha dili ka David Raya.


Victor Gyokeres

Ni staa mwingine ambaye Arteta anatamani kuwa naye katika kikosi chake na ana uzoefu wa kutosha na soka la England.

Aliwahi kucheza nchini humo kuanzia mwaka 2018 alipojiunga na Brighton iliyomtoa mara kadhaa kwa mkopo, kabla ya kumuuza jumla kwenda Converty City ambayo mwaka 2023 aliisaidia kufuzu kucheza mechi ya mtoano ya kuwania kupanda Ligi Kuu.

Kiwango chake kilisababisha wababe wa Ureno, Sporting CP kulipa Euro 20 milioni ili kumsajili na kiasi hicho kililipa kwani ilibeba ubingwa wa Ligi Kuu Ureno msimu uliopita huku Viktor akifunga mabao 41 katika michuano yote.

Katika mkataba wake kuna kipengele kinachomwezesha kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Pauni 85 milioni, hivi karibuni alipoulizwa juu ya hatma yake alisema lolote linaweza kutokea.