Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nje ya soka fani zao zingine ni hizi!

Muktasari:

  • Hawa ni wanasoka mahiri wanaotingisha katika ulimwengu wa soka. Lakini, ulishawahi kujiuliza wachezaji hao wanapenda nini nje ya soka hususan katika michezo au burudani?

LONDON, ENGLAND: UNAWAJUA vyema uwanjani. Unaijua kazi yao wanaposakata soka wakiwa katika jezi za timu kubwa duniani Ulaya. Unawafahamu kwa majina na wakati mwingine unavaa jezi zenye majina na namba wanazovaa wawapo viwanjani.

Hawa ni wanasoka mahiri wanaotingisha katika ulimwengu wa soka. Lakini, ulishawahi kujiuliza wachezaji hao wanapenda nini nje ya soka hususan katika michezo au burudani?

Nyota wanaocheza katika timu kama Real Madrid, Manchester United, Barcelona, Liverpool, Manchester City na Chelsea mara nyingi huonekana wakionyesha vipaji vikubwa uwanjani. Hata hivyo, nyuma ya umaarufu wao, wachezaji hawa wana maisha mengine nje ya soka. Wengi hupenda michezo mingine, burudani au shughuli zinazowasaidia kupumzika na kuboresha afya ya miili na akili zao.

Sikia, nje ya soka wachezaji wote unaowajua wanayo michezo au burudani zingine ambazo wanazipenda ambazo ama hucheza au kushabikia. Hawa hapa ni baadhi yao na michezo au burudani wanazozipenda au kuzicheza nje ya soka.


Robert Lewandowski (Barcelona)

Supastaa huyo wa kimataifa wa Poland aliyetengenezea jina lake akiwa katika Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), ni shabiki wa mbio za baiskeli na pia anapenda kuendesha na kuchuana anapokuwa na muda. Mara zote staa huyo hupenda kufanya hivyo anapokuwa nchini kwao, Poland.

Vinicius Jr (Real Madrid)

Ukiachana na Kylian Mbappe pale Real Madrid, staa mwingine maarufu katika kikosi hicho ni ‘brazameni’ Vinicius Jr.

Vini kama anavyoitwa na mashabiki ni mpenzi wa muziki wa Kibrazili. Anajulikana kwa kasi na chenga zake kali, lakini awapo nje ya uwanja anapenda sana muziki huo unaokwenda sambamba na dansi. Mara nyingi huonekana akicheza muziki wa Brazil au hip hop katika mitandao ya kijamii. Pia hupenda kucheza michezo ya video wakati wa mapumziko.


Bruno Fernandes (Man United)

Nahodha wa Manchester United, Bruno Fernandes, ni shabiki mkubwa wa mchezo wa tenisi na anapopata muda wa mapumziko hupenda kucheza tenisi na marafiki au familia yake. Kwa mujibu wa maelezo yake tenisi humsaidia kuboresha umakini na wepesi wa mwili.


Aurelien Tchouameni (Real Madrid)

Kiungo wa Ufaransa wa Real Madrid, Aurelien Tchouameni anapenda mpira wa kikapu. Kama vijana wengi barani Ulaya anapenda kufuatilia Ligi ya Kikapu Marekani (NBA) na pia ana marafiki kadhaa ambao ni mastaa wa mchezo huo wanaocheza katika mashindano hayo. Pia Tchouameni hucheza mchezo huo wakati wa mapumziko yake.


Harry Kane (Bayern Munich)

Nyota wa Bayern Munich na nahodha wa timu ya taifa ya England, Harry Kane ni shabiki mkubwa wa mchezo wa gofu.

Mara nyingi hutumia muda wake wa mapumziko kwenye viwanja vya gofu, hususan anapokuwa England, ambako ni mmoja wa mastaa wa soka wasiokosekana katika mechi kubwa. Kane alivutiwa na mchezo huo enzi hizo wakicheza pamoja na staa wa zamani wa Wales, Gareth Bale katika kikosi cha Tottenham Hotspur.


Luis Diaz (Batern Munich)

Mshambuliaji wa kimataifa wa Colombia na Bayern Munich, Luis Diaz anapenda sana muziki wa Amerika Kusini na dansi. Ni jambo la kawaida kumuona akicheza dansi na hii ni hata baada ya kufunga bao uwanjani. Kwa kawaida anapokuwa likizo Diaz ni mtu anayependa kuhudhuria klabu za dansi kuliko viwanjani kuangalia mechi za soka au michezo mingine.


Erling Haaland (Man City)

Straika wa Manchester City na timu ya taifa ya Norway, Erling Haaland asipokuwa katika majukumu ya kisoka anajulikana kwa kupenda kutafakari (meditation), lakini pia ni mchezaji mzuri wa gofu. Haaland anaamini utulivu wa akili humsaidia kuimarisha umakini uwanjani na kwamba huupata anapocheza gofu kwa kuwa mchezo unaotumia akili na utulivu wa kimwili.


Enzo Fernandez (Chelsea)

Kiungo wa kimataifa wa Argentina na Chelsea, Enzo Fernandez hupenda kucheza michezo ya video wakati wa mapumziko. Ni mara chache huonekana katika mechi za kikapu ambao ni mchezo wake wa pili aupendao. Kwa kawaida asipocheza michezo ya video hucheza au kuangalia mechi za kikapu.


Matheus Cunha

Mshambuliaji wa Brazil anayekipiga Manchester United, Matheus Cunha anapenda sana muziki. Nyota huyo hapendi michezo mingine na ni nadra kuonekana viwanjani isipokuwa labda katika mechi za soka za timu zingine. Nje ya hapo eneo lake la kujidai ni kuserebuka ukumbini.

Seko Fofana (Rennes)

Kiungo wa Ivory Coast na Rennes, Seko Fofana ni shabiki mkubwa wa mpira wa kikapu na mara nyingi hupenda kuucheza wakati wa mapumziko. Asipokuwa uwanjani an timu yake utamkuta katika mechi za Ligi ya Kikapu Ufaransa akifuatilia michezo.


Bryan Mbeumo (Man United)

Mshambuliaji wa kimataifa wa Cameroon, Bryan Mbeumo hupenda kucheza tenisi ya mezani (table tennis), mchezo ambao alianza kuupenda tangu akiwa mdogo. Katika mazi yake ana viwanja viwili vya mchezo huo ambapo huwaalika rafiki zake kucheza nao. Ni nadra sana kumkuta katika mashindano ya mchezo huo akifuatilia, lakini awapo nyumbani hutumia muda mwingi kwenye runinga kuangalia.


Mason Greenwood (Marseille)

Kama isingekuwa ile kashfa yake ya shambulio la aibu na unyanyasaji dhidi ya mpenziwe kule England, mshambuliaji wa Marseille, Mason Greenwood angekuwa anakipiga katika kikosi cha Manchester United. Lakini, kwa ujumla nyota huyo anapenda sana michezo ya video wakati wa mapumziko na mara moja moja huhudhuria katika viwanja vya gofu kuangalia wanavyocheza.


Ivan Toney (Al Ahli)

Mshambuliaji wa England na Al Ahli ya Saudi Arabia, Ivan Toney hupenda mazoezi ya ndondi kama njia ya kuimarisha nguvu za mwili na ni mchezo ambao pia anaupenda kuufuatilia. Toney ni shabiki wa mabondia wakubwa karibu wote, na kabla ya kuhamia Saudia alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa bingwa wa zamani wa uzito wa juu duniani, Mwingereza Anthony Joshua.


Lamine Yamal (Barcelona)

Nyota chipukizi wa Barcelona na timu ya tifa ya Hispania, Lamine Yamal, ni miongoni mwa vijana wadogo wanaokuja juu katika soka mwenye mapenzi na michezo ya video tangu akiwa mdogo. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni amekuwa akipenda kuhudhuria mashindano ya kikapu na kuogelea.


Marcus Rashford  (Barcelona/Man United)

Katika makazi yake Manchester, Marcus Rashford, nyota wa Manchester United anayekipiga kwa mkopo Barca amejenga bwawa kubwa la kuongelea. Licha ya kuupenda mchezo huo pia anashabikia ngumi. 


Mohamed Salah (Liverpool)

Nyota wa Liverpool na timu ya taifa ya Misri, Mohamed Salah hupenda riadha. Hata hivyo ni mara chache kumshuhudia akikimbia, isipokuwa yanapokuwapo mashindano hasa ya kimataifa huhudhuria.

Ismail Sarr (Crystal Palace)

Mshambuliaji wa Senegal na timu ya Crystal Palace, Ismaila Sarr ni mpenzi wa kusikiliza muziki na kucheza dansi wakati wa mapumziko. Ndani ya kumbi nyingi zilizo jirani na makazi yake amekuwa maarufu kwani kila anapokuwa na nafasi huenda kuburudisha nafsi yake.


Harry Wilson (Fulham)

Kiungo wa Wales na Fulham, Harry Wilson anapenda mchezo wa gofu, na huwa hafichi kwamba anavutiwa zaidi na masupastaa wa mchezo huo kina Tiger Woods, Scottie Scheffler, Rory McIlroy na Tommy Fleetwood.


Rafael Leao (AC Milan)

Staa huyo wa kimataifa wa Ureno na AC Milan anapenda kuimba na tayari ameshatunga nyimbo zake kibao ambazo zinasubiri kuingizwa studio. Mbali na hilo pia ni mpenzi wa maonyesho ya mitindo ambayo mara kwa mara huhudhuria anapokuwa na nafasi. Lakini, mara nyingi awapo nyumbani hupenda kujiburudisha kwa nyimbo zake na  za wanamuziki wengine maarufu duniani.

Mastaa wengine ni Bukayo saka (Arsenal) huyu anapenda kuendesha baiskeli, Joao Neves (PSG) naye baiskeli, Raphina Dias (Barca) kuogelea, Joao Felix (Al Nassr) anapenda gofu na Eduardo Camavinga (Real Madrid (ngumi). Kwa ujumla, maisha ya wachezaji wa soka hayaishii uwanjani pekee. Michezo na burudani mingine huwasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuwafanya wawe na maisha yenye uwiano mzuri kati ya kazi na burudani.