NIONAVYO: Taifa Stars na Afcon, kuna somo kutoka Gambia

HISTORIA imeandikwa baada ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kufuzu kwa mara ya tatu kucheza Fainali za michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2023 itakayofanyika huko Ivory Coast mapema mwakani.

Stars ilipata nafasi hiyo baada ya kutoka suluhu na moja ya vigogo vya soka barani Afrika, Algeria na kuipiku Uganda ambayo ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya vibonde wa Kundi F, Niger.

Mara ya kwanza Tanzania kufuzu fainali hizo mwaka 1980 zilipofanyikia Nigeria baada ya kuifunga Zambia jumla ya mabao 2-1, ikishinda nyumbani 1-0 na kutoka sare 1-1 ugenini mjini Lusaka.

Naweza kusema hiyo ndio rekodi ya juu ya Tanzania kwani nafasi zilikuwa ni nane na tuliipata nafasi hiyo kwa mbinde. Katika fainali hizo za kwanza kwa Tanzania, timu yetu ilimaliza ikivuna pointi moja kundini baada ya sare ya 1-1 na Ivory Coast ambayo ndio rekodi ya juu ya ushiriki wa michuano hiyo.

Fainali za pili zilikuwa ni za mwaka 2019 zilipofanyikia Misri na Tanzania kutoka patupu kutokana na kupoteza mechi zote tatu mbele ya waliokuwa mabingwa Algeria na waliomaliza nafasi ya pili kwenye fainali hizo Senegal na majirani zetu wa Harambee Stars ya Kenya.

Safari hii tumekata tena tiketi za kwenda Ivory Coast katika fainali hizo za 2023 zitakazofanyika kati ya Januari na Februari mwakani, kutokana na idadi ya timu kuongezeka kutoka 16 hadi 24.

Hadi sasa tunajivunia kufuzu mara 3 tukiwa na pointi moja tu katika Afcon, kwani tumefuzu lakini hatujaweka alama ya kukumbukwa katika kufuzu kwetu na katika kushiriki kwetu Afcon.

Tunajivunia matokeo ya hivi karibuni lakini tunatakiwa kuwa wakweli wa nafsi zetu kama kweli tunataka kuwa bora zaidi.

Lazima tujiulize ingekuwaje mwaka 2019 kama tungecheza mchezo wa mwisho na Uganda akiwa bado hajafuzu au mchezo wa juzi na Algeria ungekuwaje kama Algeria isingekuwa imefuzu? Bila shaka majibu tunayajua.

Majibu hayo yanapaswa kutupa hamasa ya kufanya vizuri na kwenda hatua zaidi kwa kutafuta pointi na kufanya vizuri kule Ivory Coast mwakani.

Ni muhimu kujiona kuwa tuna timu ya kiwango cha kawaida ambayo kufuzu kwake kulihitaji kujitoa kwa machozi jasho na damu. Hamasa ya serikali hasa Rais wa nchi, Samia Suluhu Hassan ilikuwa ni kubwa na wachezaji waliweka juhudi zote zilizokuwa ndani ya uwezo wao.

Kwa kujikubali kuwa ni wadogo tutaweza kuweka juhudi na kusonga mbele ili kufikia walipo wakubwa. Tunatakiwa kukimbia wakati wenzetu wanatembea. Tunatakiwa kujifunza kutoka kwa mataifa ya kawaida kama Msumbiji, Gambia, Guinea ya Ikweta na wengine wanaofanya vizuri kwa miaka ya hivi karibuni.

Hivi karibuni nilikuwa na mazungumzo na kocha mkuu wa timu ya taifa ya Gambia, Mbelgiji Tom Saintfiet na baadhi ya viongozi wa Chama cha Soka cha Gambia kujua siri ya mafanikio yao ya karibuni na kufanya vizuri kwenye mashindano ya Afcon ambako walifika robo fainali.

Gambia ni taifa dogo la Afrika Magharibi lililozungukwa pande zote na taifa la Senegal isipokuwa upande wa magharibi iliko bahari ya Atlantiki.

Tofauti na majirani zao wanaozungumza Kifaransa, nchi hii ya Gambia iliyokuwa koloni la Mwingereza haikufaidika sana na watawala wa zamani linapokuja suala la maendeleo ya soka.

“Hadi Julai 2018 Gambia ilikuwa haijashinda mchezo wowote wa kimataifa tangu iifunge Tanzania mwaka 2013,”  anasema kocha Tom Saintfiet.

“Kila mmoja alikata tamaa na hakukuwa na imani tena kuwa Gambia inaweza kushinda mchezo wa kimataifa, achilia mbali kufuzu kwa fainali za Afcon.”

Hivyo kazi kubwa waliyofanya ni kuweka mkakati wa kufanya vizuri na kurudisha kujiamini. Kazi yao haikuwa ndogo ukitilia maanani kwamba Gambia ni nchi maskini, ligi maskini ukilinganisha na nchi kama Tanzania.

“Ligi ya Tanzania ni pana na ni tajiri ukilinganisha na Gambia. Tanzania wanalipa kama mara 5 ya mishahara ya Gambia,”  anabainisha kocha huyo.

Tangu mwaka wa 2018 wamekuwa wakifanya juhudi za kuwatafuta Wagambia na watu wenye asili ya nchi hiyo ya Gambia kuimarisha kikosi chao.

Timu imeanza kufanya vizuri na wadhamini wameanza kujitokeza.Wachezaji wa viwango vya wastani walioko Ulaya wanaiona timu ya taifa lao kama njia ya kujiweka sokoni na hata wanaocheza nje wanajua timu ya taifa inawafikisha pale ambako klabu zao maskini haziwezi kuwafikisha.

Mwaka 2021 Gambia ilifuzu kwa mara ya kwanza na kwenda hadi robo fainali. Gambia iliingia michuanoni ikiwa ni timu ya chini kabisa katika viwango vya Fifa kuwahi kushiriki fainali za Afcon.

Kufika robo fainali, njiani Gambia ilishinda dhidi ya mataifa makubwa kisoka kama Guinea na Tunisia na sasa kwa fainali za mwakani, Gambia imefuzu pamoja na Mali na kuziacha nje Jamhuri ya Congo na Sudan.

Kufuzu kwao ilibidi kusubiri hadi dakika ya 90 kuweza kusawazisha magoli mawili dhidi ya Congo iliyokuwa inaongoza 2-0, hivyo kupata pointi moja iliyohitajika. Gambia maarufu kama The Scorpions kama wanavyojulikana, wamefuzu mara mbili tu lakini ni timu ambayo, kwa rekodi yake, kila atakayekutana nayo ataiendea kwa tahadhari.

Tanzania tuna msingi mzuri wa kufanya vizuri kuliko mataifa kama Gambia. Ni mashirikisho machache duniani yenye kiwango cha uungwaji mkono wa serikali kama Tanzania.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.