NIONAVYO: Haya yafanyike Ligi Kuu Kenya iamke upya

SIKU ya kilele cha ligi kuu ya Kenya (FKF Premier League) ilikuwa ni siku njema hasa kwa mashabiki wa Gor Mahia au K’ogalo kama wanavyoitwa na wapenzi wao . Ilikuwa ni sherehe kubwa baada ya Gor Mahia kuifunga Nairobi City Stars mabao 4-1. Kila shabiki alipenda kuwa sehemu ya sherehe hizi kiasi kwamba maofisa wa ligi, wa chama cha mpira na wale wa usalama kulihamishia zoezi la kutoa tuzo na medali katika chumba cha wageni maalum (VVIP).

Pamoja na sherehe, nderemo na vifijo vya wapenzi wa Gor ambao kwao huu ni ubingwa wa 20, bado kuna jambo moja halikuwa sawa au tuseme halikuwa kawaida; waliondoka mfuko mtupu. Hakukuwa na hundi iliyotoka.
Hali hii ya bingwa kutoka bila kitita cha pesa si kwamba haikutarajiwa .Hasha. Mwezi Mei mwaka huu Rais wa FKF Bwana Nicky Mwendwa alitamka hadharani kuwa shirikisho lake lilikuwa mufilisi hivyo bingwa wa msimu uliokwisha angeondoka patupu katika suala la fedha isipokuwa taratibu za medali na kombe ambavyo vilitolewa siku hiyo.
Waswahili husema nyakati hubadilika. Kwa miaka mingi  Kenya imekuwa kinara wa soka la Afrika Mashariki na Kati. Kenya haikufikiwa na taifa moja la ukanda huu hasa linapokuja suala la udhamini wa mashindano mbalimbali ya soka.

Haishangazi kusoma kwamba mashindano mengi ya Afrika Mashariki na Kati yalifanyika Kenya kwani msuli wa pesa ulikuwepo kiasi cha hata kuokoa mashindano pale nchi nyingine ziliposhindwa kugharamia uenyeji.

Kenya ilikuwa kitovu cha makampuni mengi yaliyokuwa tayari kudhamini mashindano mbalimbali ya mpira.

Kusikia kwamba bingwa wa Kenya ametoka bila hundi ya senti moja ni jambo la kusikitisha sana.

Hata hivyo, akiongelea hali hiyo ya ukata mapema mwezi wa Mei,n Rais Nicky Mwendwa alisema hali hiyo haimtishi kamwe kwani anaiona kesho inayong’aa. Bila shaka bosi huyo na shirikisho lake wana silaha mbadala kupambana na hali hiyo.
Hapa tunaongelea ligi ambayo ni nyumbani kwa Gor Mahia FC ambao ni mabingwa wa Kombe la washindi la CAF mwaka 1987, wanafainali 1979, nusu fainali 1989 na robo fainali 1988.

Hii ni ligi ambayo ilionewa wivu na mataifa mengine hasa kupitia vigogo wao kama Gor Mahia, AFC Leopards na Tusker. Hapa ni nyumbani kwa Joe Kadenge, nyumbani kwa Peter Dawo, nyumbani kwa Wiberforce Mulamba, nyumbani kwa Sammy Onyango Jogoo, nyumbani kwa Mahmoud Abass, nyumbani kwa Mwalala, nyumbani kwa Joash Onyango. Taja kila jina kubwa la mpira katika ukanda huu. Hapa ni nyumbani kwa mpira.
Mpira wa sasa, hasa ligi zinahitaji fedha nyingi kuendesha .Bila shaka uongozi wa FKF unalitambua hilo. Zimekuwa zikitolewa sababu lukuki kwa hali hiyo huku Rais wa FKF akinyoosha kidole kwa serikali iliyopita kuingilia sana masuala ya uendeshaji wa mpira kiasi cha nchi hiyo tajiri ya Afrika Mashariki kufungiwa mlango na Shirikisho la soka la Kimataifa ,FIFA.
Huko nyuma, ligi ya FKF yenye vilabu 18 ilipata kandarasi ya miaka 7 ya udhamini toka Kampuni ya Star Times yenye thamani ya karibu Dola za Kimarekani milioni 110. Hii kwa kweli ilionekana ni pumzi ya kutosha katika kuendesha ligi ya Kenya. Ushirika huo wa mwaka 2020, haukwenda mbali kwani mwaka mmoja baadaye Star times ikasitisha mkataba kwa ilichodai kuwa ni uendeshaji tofauti na makubaliano. Ligi ikawa yatima tena.

Mwezi Desemba 2022, waziri wa masuala ya vijana na michezo Ababu Namwamba alikuja na habari njema ya kwamba amejadiliana na Kampuni kubwa ya televisheni ya Afrika  Kusini ambayo ingekuja kupulizia hewa ya uhai katika FKF Premier League. Bado mambo hayajakaa sawa.

Mwezi Mei mwaka huu FKF waliingia mkataba wa muda mfupi na Kampuni ya Azam Pay Television ambayo pia ina kandarasi ya kurusha kwenye runinga ligi kuu ya Tanzania Bara.
Chini ya kandarasi hiyo, inasemekana Azam walitoa fedha inayokaribia dola za kimarekani elfu 80 ambazo ziligawiwa kwa vilabu vyote 18 na kisha Azam kurusha michezo miwili ya ligi hiyo.  Rais Nicky Mwendwa ana matumaini kwamba mahusiano na Azam, japo ya muda mfupi, yanaweza kuzaa kitu kikubwa katika muda mrefu. Upande wa Azam unachukulia mahusiano hayo kama njia ya kupima kina cha maji kabla ya kuyaoga. Tusubiri na kuona.

Bila kujali wanafanya kazi na Azam Paytv, Super Sport, Star Times au wengineo, ligi ya Kenya inahitaji udhamini imara ili iweze kushindana na ligi za majirani kama Tanzania, Uganda, Ethiopia na Sudan. Mpira ni mchezo wa ushindani na ili ushindane lazima uwe vizuri mfukoni. Klabu zinahitaji fedha kusafiri kutoka sehemu moja ya Kenya kwenda sehemu nyingine. Wachezaji wanahitaji mshahara kwa ajili ya maisha yao na familia zao.

Vinahitajika vifaa kwa ajili ya timu. Makocha wazuri wanapatikana kwa fedha. Waamuzi na maafisa wengine wa siku ya mchezo wanahitaji kulipwa ili kuwa katika ubora wao kazini.  Maofisa wa ligi wanahitaji fedha ili kuweza kuisimamia ligi ipasavyo .Inahitajika pesa kuweka sawa miundombinu ya kuchezea mpira.

Mifano imeonekana bayana huko Afrika ya Kusini, Tanzania, Morocco, Tunisia, Misri na kwingineko. Ligi Kuu ya nchi husika inapopata udhamini wa kueleweka. Ligi ku inapoendeshwa kwa weledi mkubwa. Basi uwezekano wa vilabu kupata wadhamini binafsi nao unaongezeka. Hali hiyo italeta msisimko ambao utaleta fedha nyingi katika ligi hiyo. Mashabiki wa Kenya hawana tofauti na wale wa nchi nilizotaja hapo juu, wanaweza kuubeba mpira wao ikiwa mpira utawezeshwa.
Haiingii akilini kwamba Shabana FC na Murang’a wamepanda daraja kuja kuwania kombe na medali tu. Lazima kiwepo kitu cha kuwania.

Ni muhimu kutafuta kila rasilimali ili kuiwezesha ligi ya Kenya iwe katika ubora na hivyo kurudisha mapenzi ya wananchi kwa mchezo huu. Ligi bora ya Kenya siyo tu kwamba itatoa burudani, itatoa ajira pia. Ligi bora ya Kenya itazalisha wachezaji wazuri kwa timu ya taifa, Harambee Stars.
Kama kisingizio cha matatizo na serikali na pia FIFA kimeondoka, sasa wananchi wanakodoa macho kwa Rais Nicky Mwendwa, Makamu Petra na Mtendaji Mkuu Omondi waweze kutatua changamoto inayorudisha nyuma ligi ya FKF.Changamoto ya fedha.

Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF).Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.