NIONAVYO: Al Hilal na hatma ya Yanga SC kwenda robo fainali nyingine
Muktasari:
- Ilikuwa vigumu kubeti kutokana na namna kundi walilopangwa lilivyokuwa. Una TP Mazembe ya Lubumbashi ambao ni mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Mazembe kama si timu inayofuata kwa rekodi Afrika nyuma ya Al Ahly Cairo basi ni klabu nambari moja katika CAF kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
NI jambo ambalo halikutarajiwa sana wakati makundi ya Ligi ya Mabingwa yakitajwa. Hakuna aliyeamini Al- Hilal Omdurman ya Sudan, ingekuwa ya kwanza Afrika kufuzu kwa robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu huu 2024/25. Hili ni jambo ambalo hata wataalamu wa kucheza kamari wasingekuwa tayari kuwabetia.
Ilikuwa vigumu kubeti kutokana na namna kundi walilopangwa lilivyokuwa. Una TP Mazembe ya Lubumbashi ambao ni mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Mazembe kama si timu inayofuata kwa rekodi Afrika nyuma ya Al Ahly Cairo basi ni klabu nambari moja katika CAF kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Una Yanga ambao ni wana fainali ya Kombe la Shirikisho 2022/23 na pia robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita wa 2023/24 ambako walitolewa bila kupoteza mchezo katika dakika 90.
Bao la Aziz Ki Stephane lililokataliwa dhidi ya Mamelodi Sundowns ilikuwa ni uokozi pekee wa kuupeleka mchezo huo kuamuliwa na kipa Rowen Williams ambaye ustadi wake katika kudaka penalti zimempa umaarufu si katika Afrika bali duniani kote.
MC Alger wana rekodi nzuri kama zilivyo timu nyingi za Algeria na Afrika ya Kaskazini na haikushangaza kuwaona mashabiki wa Yanga wakishangilia kuwa katika hili kundi na hasa wakitamka wazi kwamba wapangaji wamewawezesha kupata nafasi ya kulipa kisasi kwa kocha Florent Ibenge na Al Hilal kwani katika msimu wa 2022/23 ndio waliiondosha Yanga katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa.
Kipigo hicho kikawa baraka kwani Yanga, kwa mujibu wa taratibu za wakati huo ilihamishiwa katika Kombe la Shirikisho ambako ilifanya vizuri hadi kufika fainali na kupoteza dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Mashabiki wa Yanga sio tu kwamba walifurahia nafasi ya kisasi, hapana; Yanga tayari waliona wanyonge wao hasa kwa Al Hilal na TP Mazembe ambayo walikuwa wameifunga ndani nje katika mitanange miwili ya mwisho kwenye Ligi ya Mabingwa.
Yanga waliona watakuwa juu ya Al Hilal na TP Mazembe kama si kuongoza kundi.
Sio tu kwamba Al Hilal sasa inaongoza kundi hilo na imeshafuzu kwenda robo fainali, bali pia imeshikilia hatma ya Yanga katika mashindano ya Afrika kwa msimu huu.
Tunaweza kusema 50% ya hatma ya Yanga iko mikononi mwa Al Hilal. Hatma yao inategemea kwa kiasi kikubwa matokeo yao dhidi ya Al Hilal wanayokutana nayo Jumapili huko Mauritania.
Kumbuka, Yanga walipoteza mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam dhidi ya ‘jeshi la samawati’.
Kubwa lililonishangaza na linaloweza kuwa linawashangaza wengi sio tu matokeo ya uwanjani bali namna Al Hilal inavyocheza katika ubora huu ikiwa ni msimu wa pili inaishi ukimbizini. Hakuna Ligi yoyote ya soka inayochezwa Sudan. Nchi iko vitani, klabu iko ukimbizini.
Msimu uliopita, Al Hilal waliweka kambi yao Dar es Salaam na michezo ya Ligi ya Mabingwa walicheza Kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Msimu huo hawakuweza kwenda zaidi ya hatua ya makundi.
Msimu huu Al Hilal wameweka kambi Mauritania ambako wanashiriki ligi ya huko na wanaongoza kwa sasa katika Lligi ya Mauritania ikicheza mechi 15 bila kupoteza hta moja.
Ni klabu ngapi zinaweza kufanya kazi katika mazingira kama haya na zikaendelea kufanya vizuri?
Ni klabu ngapi Afrika na duniani kote zinaweza kujikuta katika mazingira ya Al Hilal zikaendelea kuwa na kikosi chake na benchi la ufundi bila kutikiswa?
Ni namna gani klabu inaweza kuendelea kuwa na uongozi katika hali ya vita tena wakiwa nje ya mipaka?
Wapi wanapata rasilimali fedha za kuendesha timu?
Wataendelea kuwa imara kwa muda gani? Haya ni maswali tutakayoyajibu katika makala zijazo, lakini itoshe kusema kuwa Al Hilal ni timu iliyo vitani ndani ya uwanja na nje ya uwanja. Kuwa timu ya kwanza kufuzu kwa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ni jambo kubwa sana kwa Al Hilal na hali yao.
Yaani Al Hilal ambayo haikupewa nafasi ya kwenda zaidi ya hatua ya makundi.
Mwandishi wa makala hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF). Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.