Hello

Your subscription is almost coming to an end. Donโ€™t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nini kimewakuta mastaa hawa Ligi Kuu Bara?

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Licha ya ligi hiyo kusimama kwa sasa, ila wapo baadhi ya washambuliaji ambao wanakabiliwa na ukame wa mabao katika timu zao mbalimbali wanazocheza kutokana na kukaa muda mrefu bila ya kufunga, kama Mwanaspoti linavyowaelezea miongoni mwao.

WAKATI Ligi Kuu Bara ikisimama hadi Aprili Mosi ili kupisha kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa zinazochuana kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026, ushindani nao unaendelea kupamba moto kwa kila kona.

Licha ya ligi hiyo kusimama kwa sasa, ila wapo baadhi ya washambuliaji ambao wanakabiliwa na ukame wa mabao katika timu zao mbalimbali wanazocheza kutokana na kukaa muda mrefu bila ya kufunga, kama Mwanaspoti linavyowaelezea miongoni mwao.


MEDDIE KAGERE 'MK14' (NAMUNGO FC)

Mmoja wa washambuliaji waliofanya vizuri zaidi na kujizoelea umaarufu katika Ligi Kuu Bara ni aliyekuwa mshambuliaji wa timu ya Simba, Meddie Kagere 'MK14', ambaye kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha 'Wauaji wa Kusini', Klabu ya Namungo.

Nyota huyo raia wa Rwanda wakati anaondoka Msimbazi aliweka rekodi tamu kwa mastaa wa kigeni katika Ligi Kuu Bara ambayo imeendelea kuishi hadi leo, kwani licha ya wachezaji wengi waliokuwa bora na wazoefu kucheza ila wameshindwa kuifikia.

Kagere alitua Simba akitokea Gor Mahia ya Kenya msimu wa 2018-2019 na kufunga mabao 23 na kuipiku rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe ya wachezaji wa kigeni kufunga mabao mengi msimu mmoja alipofunga 21 msimu wa 2015-2016.

Msimu wa pili kwa staa huyo akiwa na Simba pia, alifunga mabao 22 na kutetea tuzo ya mfungaji bora ikiwa pia ni rekodi kwani, haikuwahi kutokea kwa mchezaji yeyote iwe mzawa au wa kigeni kutwaa tuzo ya ufungaji bora mara mbili mfululizo.

Baada ya hapo 'MK14' akaachana na kikosi cha Simba na kujiunga na Singida Big Stars msimu wa 2022-2023 na aliendelea kuonyesha kiwango bora kwa kufunga mabao manane, kisha msimu uliopita akaichezea Namungo na kufunga mabao mawili.

Licha ya rekodi hizo tamu ila Kwa sasa nyota huyo anaandamwa na ukame wa mabao kwani mchezo wa mwisho kufunga bao ni ule wa Februari 24, 2024, dhidi ya KMC FC, ambao kikosi hicho cha 'Wauaji wa Kusini' kikiwa ugenini kilitoka sare ya 2-2.

RELIANTS LUSAJO (DODOMA JIJI)

Lusajo ameanza vibaya maisha yake ndani ya kikosi hicho cha Dodoma Jiji kwani tangu ajiunge nacho msimu huu hajafunga bao lolote, huku mara ya mwisho kwake kufunga Ligi Kuu Bara ilikuwa wakati akiichezea Mashujaa FC msimu uliopita.

Mshambuliaji huyo aliyezichezea timu mbili tofauti msimu uliopita akianzia na Namungo FC kisha dirisha dogo kujiunga na Mashujaa, mara ya mwisho kufunga ilikuwa Mei 28, 2024, wakati kikosi hicho cha Kigoma kikiifunga Dodoma Jiji mabao 3-0.

Akiwa na Namungo FC aliyoitumikia tangu imepanda Ligi Kuu Bara msimu wa 2019-2020, huku akiwa ndiye kinara wao wa mabao, msimu uliopita aliifungia mabao mawili, japo Mashujaa aliifungia sita na kuhitimisha msimu wa 2023-2024 na mabao manane.


MOUBARACK AMZA (NAMUNGO FC/ KAGERA SUGAR)

Nyota huyu wa Cameroon kwa sasa amerejea tena Kagera Sugar katika dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Namungo FC, ambayo hadi sasa hajafunga bao lolote la Ligi Kuu Bara zaidi ya kufunga tu kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (FA).

Amza msimu bora kwake hapa nchini ambao hata yeye anakiri ulikuwa wa 2022-2023, wakati akikichezea kikosi cha 'Wagosi wa Kaya' Coastal Union ambapo alimaliza msimu kwa kufunga mabao saba, ingawa kuanzia hapo amekuwa na wakati mgumu kikosini.

Mshambuliaji huyo aliyerejea Kagera Sugar kwa mara ya pili, mara ya mwisho kufunga ilikuwa pia akiwa na timu hiyo wakati ilipoifunga Tabora United mabao 3-0, mechi iliyopigwa Aprili 17, 2024, kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.


SAMSON MBANGULA (TZ PRISONS)

Nyota huyu kwa sasa amefanyiwa upasuaji wa goti, katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), jijini Dar es Salaam, japo ana ukame wa mabao tangu mara ya mwisho alipoonekana uwanjani Oktoba 26, 2024, wakati Prisons ilipofungwa na KMC mabao 2-1.

Mbangula aliyemaliza na mabao manane msimu uliopita huku akiwa katika kiwango bora ndani ya kikosi hicho cha maafande, mara ya mwisho kufunga bao katika Ligi Kuu Bara ilikuwa sare ya timu hiyo ya 1-1, dhidi ya JKT Tanzania Machi 13, 2024.


MATHEO ANTHONY (JKT TZ)

Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo ya maafande wa JKT Tanzania msimu huu akitokea Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja, licha ya kuandamwa na majeraha, ila hata nafasi ya kucheza pia kwenye kikosi cha kwanza imekuwa ni finyu tangu msimu umeanza.

Akiwa na Mtibwa Sugar msimu uliopita, Matheo aliifungia mabao manne ya Ligi Kuu, huku mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1, dhidi ya Mashujaa, kwenye Uwanja wa Manungu Complex mjini Morogoro Desemba 19, 2023.


ADAM ADAM (AZAM FC/ TZ PRISONS)

Kwa sasa mshambuliaji huyo anaichezea Tanzania Prisons kwa mkopo akitokea kwa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Mashujaa FC aliyoonyesha kiwango bora, ingawa hadi wakati huu mambo yameenda kombo.

Msimu uliopita alifunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara na kuwavutia mabosi wa Azam FC waliomsajili japo hadi sasa hajafunga bao lolote, huku mara ya mwisho kufunga ilikuwa ushindi wa Mashujaa FC wa 1-0, nyumbani dhidi ya Namungo Machi 2, 2024.


HABIB KYOMBO (SINGIDA BS/ PAMBA FC)

Kyombo aliyeichezea Simba, amejiunga na Pamba Jiji katika dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Singida Black Stars huku akiandamwa na ukame wa mabao, baada ya kushindwa kutupia bao lolote la Ligi Kuu Bara akiwa na timu hizo zote mbili.

Mara ya mwisho kwa nyota huyo kufunga bao, ilikuwa ni katika ushindi wa Singida Fountain Gate iliyojigawa baadaye kisha kuitwa Fountain Gate wakati kikosi hicho kiliposhinda 2-0, dhidi ya Dodoma Jiji Mei 4, 2024, huku akitupia yote kambani.


CHARLES ILANFYA (JKT TZ)

Mshambuliaji huyo alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya goti ingawa mbali na changamoto hizo zinazomkabili ila hata nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya timu hiyo ya maafande aliyojiunga nayo msimu huu akitokea Mtibwa Sugar imekuwa ngumu.

New Content Item (1)

Mara ya mwisho kwa nyota huyo kufunga ilikuwa ni kichapo cha Mtibwa Sugar ilichokipata dhidi ya Yanga cha mabao 3-1, Mei 13, 2024, ukiwa mchezo ambao kikosi hicho cha Jangwani kilitangaza rasmi ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya 30, tangu mwaka 1965.


EDGAR WILLIAM (FOUNTAIN GATE)

Edgar ni ingizo jipya Fountain Gate ambapo amefunga mabao matano ya Ligi Kuu, ingawa anakabiliwa na ukame wa muda mrefu, kwa sababu mara yake ya mwisho alifunga katika ushindi wa kikosi hicho wa 3-2, dhidi ya Coastal Unon, Desemba 13, 2024.

Nyota huyo msimu uliopita akiwa na KenGold aliibuka mfungaji bora wa Ligi ya Championship baada ya kufunga mabao 21 kwa msimu mzima, ikiwa ni rekodi mpya kwani kabla ya hapo haijawahi kutokea mshambuliaji aliyefunga idadi kubwa kiasi hicho.

New Content Item (1)

Tangu msimu wa 2017-2018, rekodi kubwa ya kufunga mabao ilikuwa ikishikiliwa na mshambuliaji wa JKT Tanzania, Edward Songo aliyefunga mabao 18 msimu wa 2022-2023, japo idadi hiyo ilivunjwa na Edgar na kujitengenezea ufalme wake binafsi.

Mbali na ufungaji bora wa Championship, Edgar alishinda pia Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi ya Championship msimu uliopita baada ya kuwashinda Casto Mhagama aliyecheza naye KenGold na Boban Zirintusa wa Biashara United aliyejiunga na Tusker ya Kenya.

Mshambuliaji huyo anashikilia rekodi nzuri katika Ligi ya Championship kwani licha ya kuibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia amezipandisha timu mbili kwenda Ligi Kuu Bara akianza na KenGold msimu huu na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022.


JOHN BOCCO (JKT TZ)

Nyota huyu tangu alipoifungia JKT Tanzania mabao mawili katika ushindi wa 4-2, dhidi ya Tabora United kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Oktoba 18, 2024, hajafunga tena, japo anashikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote Ligi Kuu.

New Content Item (1)

Mshambuliaji huyo amefunga jumla ya mabao 156, ya Ligi Kuu Bara ambapo alianza kuifungia Azam FC aliyoitumia kwa misimu tisa kuanzia 2008 hadi 2017, mabao 84, huku Simba akiifungia 70, wakati kikosi hicho cha Maafande amekifungia mawili tu.

Bocco ndiye aliyevunja rekodi ya kutupia mabao mengi iliyokuwa inashikiliwa na Mohamed Hussein 'Mmachinga' aliyetamba na timu za Bandari Mtwara, Yanga, Simba, Mmbanga na Twiga Sports katika Ligi Kuu kwani alikuwa amefunga jumla ya mabao 153.


YASSIN MGAZA (DODOMA JIJI)

Mshambuliaji huyu anaandamwa na ukame pia wa mabao kwani mara yake ya mwisho kufunga ilikuwa ni kichapo cha kikosi hicho cha 2-1, dhidi ya Singida Black Stars, katika mchezo wa Ligi Kuu, uliopigwa Uwanja wa CCM Liti Singida Desemba 12, 2024.

New Content Item (1)

Nyota huyu anayeichezea Dodoma Jiji, msimu wake wa kwanza wa 2023-2024, alimaliza na mabao matatu ya Ligi Kuu Bara japo safari hii hadi sasa mambo yamekuwa ni magumu, licha ya kutabiriwa makubwa kutokana na kiwango alichoonyesha Zanzibar.

Mgaza alijiunga na Dodoma Jiji akitoka kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Ligi ya Zanzibar (ZPL) akiwa na kikosi cha KMKM msimu wa 2022-2023, ambapo alihusika na mabao 25, katika michezo 25 kati ya 30, baada ya kufunga 17 na kuasisti manane.