Nikimkumbuka Kizota, naikumbuka Boxing Day
Muktasari:
Wakati tunapasha misuli tulipigwa na butwaa kuona kile kikosi kilichompiga mnyama ndio kinaanza, jasho jembamba lilitutoka lakini wanaume tukasema liwalo na liwe, shughuli wataipata.
LEO Alhamisi ni siku maalumu, inaitwa Boxing Day, siku ya kufungua zawadi, siku moja baada ya Wakristo duniani kuadhimisha siku maalumu ya kuzaliwa mkombozi wao Yesu Kristo katika Bethelehemu ya Uyahudi takribani miaka 2000 iliyopita.
Neno kufungua zawadi limenikumbusha mbali, miaka takribani 23 iliyopita wakati nikielekea ukingoni katika kucheza soka la ushindani, ilikuwa kwenye Uwanja wa Karume, wakati mabingwa wa mkoa wa Dar es Salaam wakati huo, Cargo au Bandari Dar es Salaam walipocheza mechi ya kujipima nguvu na Yanga.
Wiki moja kabla ya mechi hiyo, Yanga walikuwa wamewafunga mahasimu wao, Simba mabao 3-1 yaliyofungwa na Sanifu Lazaro ‘Tingisha’, Makumbi Juma na Thomas Kipese.
Cargo pamoja na kuondokewa na baadhi ya wachezaji wetu nyota kama Ally Yusufu Chabala, Method Andrew, Samwel Owu na Anthony Kifaro waliokwenda Bandari Mtwara kuimarisha kikosi cha Kocha Zakaria Kinanda (marehemu), bado ilikuwa na wachezaji muhimu wakati huo.
Wachezaji hao ni Issa Manofu, Juma Dalo Upara, Mambo Mohamed, Mwamini Siso, Hamis Mponda, Ibrahimu Ramadhani na safu yao ya ushambuliaji ikiongozwa na mkongwe Hatibu Rajabu Bibo na mwandishi wa makala hii Kennedy Patrick enzi hizo jina Mwaisabula halitumiki. Cargo hiyo si haba, nayo ilikuwa moto, ukitufunga lazima uende kulala na viatu.
Pamoja na kujiamini kwetu tulitegemea kikosi cha Yanga hakitapangwa kamili kwa kuwa bado wale mastaa walikuwa wanashangilia ushindi, hivyo tungepata mteremko zaidi na kushinda.
Wakati tunapasha misuli tulipigwa na butwaa kuona kile kikosi kilichompiga mnyama ndio kinaanza, jasho jembamba lilitutoka lakini wanaume tukasema liwalo na liwe, shughuli wataipata. Kikosi kile cha Yanga kilikuwa hivi; Sahau Kambi (marehemu), Fredy Minziro, Kenneth Mkapa, Godwin Aswile, Salum Kabunda (marehemu), Issa Athuman (marehemu), Justin Mtekele (marehemu), Athumani China, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’, Said Mwamba ‘Kizota’ (marehemu) na Thomas Kipese.
Soka lilianza kwa taratibu huku kila timu na hasa Yanga wakisoma mchezo na kumtafuta nani mzuri wa kumkaba maana sisi timu yao nzima tulikuwa tunaiogopa na tunawafahamu.
Ni mara chache mno huwa napenda kuongea nilivyokuwa wakati nacheza lakini nami nilikuwa kati ya wachezaji wenye kipaji cha kuweka mpira kwenye nyavu za timu pinzani. Wakati Yanga bado wanatusoma, winga wetu machachari Mbaraka Zame aliambaa na mpira upande wa kulia na kumlamba chenga Mkapa kabla ya kupiga krosi iliyonikuta katikati ya msitu wa mabeki katili kupita kiasi Godwin Aswile na Salum Kabunda.
Niliwahadaa kwa chenga ya mwili na kuwaacha wakigongana na mimi kuwa uso kwa uso na Sahau Kambi na kwa kuwa nilikuwa katika eneo la kufunga niliuweka mpira nyavuni na kuiandikia Cargo bao la kuongoza lililodumu hadi wakati mapumziko.
Kipindi cha pili wakati tunatoka katika vyumba vya kubadilishia nguo Kizota ambaye nilikuwa naye utotoni pale Tabora alikuwa amejimwagia maji mwili mzima na mara akaniambia, Kenny sasa tunakwenda kufungua zawadi zenu.
Nilicheka tu nikabaki namshangaa tu fundi yule, maana Kizota alikuwa fundi kuliko fundi.
Mpira ulipoanza dakika zote 45 ulikuwa kwenye goli letu hadi unakwisha na tulikuwa tunafanya kazi moja ya kuokoa hadi tulichoka na mwisho wa siku tulipigwa mabao matatu yaliyofungwa na Issa Athuman, Kizota na Makumbi Juma kwa shuti kali mno ambalo kipa kijana wa wakati huo Issa Manofu alishindwa kulizuia.
Mpira ulipokwisha Kizota alinifuata na kuniambia Kenny nadhani umeiona Boxing Day yenu, tumewafungulia kipindi cha pili baada ya mtoto kuzaliwa kipindi cha kwanza, hiyo ilikuwa ni mwaka 1990.
Zawadi hiyo naikumbuka hadi leo basi, Said Mwamba ‘Kizota’ mtaalamu wangu pumzika salama, zawadi yako nimeifungua tena leo.