Ni muda wa Yanga

KAMA ilivyo kwenye maisha ya kawaida kila jambo na muda wake, kuna muda wa kupata na muda wa kukosa lakini kuna muda wa kushinda na muda wa kushindwa hivyo hivyo kwenye kuanguka na kuinuka, hivyo ndivyo maisha yameiendea timu ya Yanga katika miaka yake 88, tangu kuanzishwa kwake 1935.

Huenda msimu huu ukawa ndio muda bora zaidi na wa mafanikio makubwa kwa Yanga tangu kuanzishwa kwake kutokana na rekodi kadhaa ilizoziweka na kufanya yale yasiyowezekana kuonekana yanawezekana.

Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika pia ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kuwa na walau mchezaji mmoja aliyetwaa tuzo kwenye kila hatua ya michuano hiyo.

Tuzo hizo ni zile za mabao ya kila hatua ambapo Fiston Mayele alianza kwa kuchukua bao bora la wiki katika michuano hiyo, akafuatia Mudathiri Yahya aliyeshinda tuzo ya bao bora la hatua ya makundi.

Baada ya hapo, Mayele alishinda tena bao bora la robo fainali ya michuano hiyo, baadae nusu fainali ya kwanza Stephane Aziz Kii akashinda bao bora na ile ya pili tuzo hiyo ikaenda kwa Kennedy Musonda.

Sahau kuhusu kuingia fainali hiyo, Yanga msimu huu pia imeendelea kuonyesha kuwa ni muda wake baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo ikiwa ni mara ya 29 kutwaa taji hilo na kuendelea kuifanya kuwa klabu iliyolibeba mara nyingi zaidi.

Pia Yanga imeingia fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), kwa mara ya pili ikiwa ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo baada ya kuifunga Coastal Union mchezo wa fainali na raundi hii itakutana na Azam FC uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Pamoja na yote hayo, maendeleo ya Yanga imechagizwa na maandalizi bora iliyoyafanya katika kila idara kuanzia zile muhimu kama zitakavyoorodheshwa hapa.


UONGOZI

Uongozi ni moja ya sehemu muhimu zaidi kwenye taasisi yeyote hususani soka ambayo inahitaji maarifa na utendaji uliotukuka.

Mwishoni mwa msimu uliopita, Yanga ilifanya uchaguzi wa viongozi na kumchagua Injinia Hersi Said kuwa Rais wa klabu hiyo huku Arafat Haji akiwa Makamu wake na kuunda bodi ya viongozi wengine katika kuiongoza na kuiendeleza Yanga.

Baada ya hapo kila mmoja katika nafasi yake alitimiza wajibu wake na kuongeza ushawishi kwa wadhamini, na kupata pesa iliyotumika katika kusajili wachezaji, na kuongoza timu kiujumla na hapo katikati aliongezwa Andre Mtine akiwa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo aliyeongeza ufanisi zaidi.


UDHAMINI

Kwasasa mpira ni pesa, na unahitaji pesa ili kuwa bora zaidi. Msimu huu Yanga imeongeza ushawishi wa kutosha kwa wadhamini na kufanya wengi wajihusishe na timu hiyo.

Ukiachana na Wadhamini kama Sportpesa, Azam TV, Jembe Energy Drink, Max na Unicef lakini kumekuwa na mfadhili wa timu hiyo GSM ambaye kwa nafasi ya kipekee anaimbwa zaidi kama moja ya kampuni na mtu aliyetoa mchango mkubwa katika mafanikio ya Yanga na anastahili maua yake.


BENCHI LA UFUNDI

Siri nyingine nyuma ya mafanikio ya Yanga kwa msimu huu ni benchi la ufundi lililoimarika kila idara kuanzia kwa Kocha mkuu, Nassredine Nabi, msaidizi wake Cedric Kaze, mtathimini michezo na kusoma wapinzani Khalil Ben Youssef, kocha wa viungo Helmy Gueldich, kocha wa makipa Milton Nienov, mchua misuli Youssef Ammar na wengine wote wanafanya kazi kuhakikisha kikosi kinafanya vizuri.

Wote hao kwa pamona na umoja wamekuwa wakifanya kazi kubwa kuhakikisha kikosi cha Yanga kinakuwa katika afya, umoja na ubora wa hali ya juu na kupambana uwanjani kwa lengho la kufikia malengo.


WACHEZAJI

Hapa ni eneo lingine ambalo Yanga imejitofautisha na timu nyingine nyingi za Ligi Kuu kutokana na aina ya wachezaji iliyonao.

Yanga ina zaidi ya wachezaji 25 na asilimia zaidi ya 75 ya wachezaji hao wamekuwa na viwango bora vinavyoshabihiana kwa karibu sana.

Uwepo wa wachezaji hao ambao ubora wao ni wa hali ya juu na haupishani sana kumefanya Yanga kutawala na kujenga mizizi ya kibabe kwenye kila michuano inayoshiriki.

Kuanzia makipa wakiongozwa na Djigui Diarra, mabeki chini ya Bakari Mwamnyeto, viungo wakiongozwa na Kharid Aucho na washambuliaji wakiongozwa na Fiston Mayele, Yanga kwenye kila eneo ina watu wawili au zaidi ambao ubora wao ni wa hali ya juu sana.


MASHABIKI

Huenda ukiwachukulia poa lakini mashabiki wa Yanga msimu huu wamechangia zaidi mafanikio iliyoyapata timu hiyo.

Mara zote mashabiki ni wachezaji wa 12, hivyo kushangilia kwao inakuwa kama wanawaongezea nguvu wachezaji na hali ya kujituma zaidi.

Mashabiki wa Yanga wamekuwa wakifanya hivyo kwa ubora sana msimu huu pia hata pale timu ilipopitia changamoto walitulia na kuwapa moyo wachezaji wao na hadi sasa ni kila kitu kwao ni 'Kivumbi na Jasho'.


WASIKIE WENYEWE

Rais wa Yanga, Injinia Hersi alisema mipango yake ni kuifikisha Yanga kwenye ubora wa kushindana na kushinda dhidi ya timu nyingine vigogo wa Afrika.

"Lengo kuu la kuiongoza Yanga ni kuifanya iwe timu bora Afrika itakayoshindana na kushinda mbele ya timu nyingine bora Afrika," anasema Hersi.

Nahodha wa timu hiyo, Mwamnyeto kwa niaba ya wachezaji alisema wapo Yanga kujituma kuhakikisha wanafikia malengo na kuwafurahisha mashabiki wao.

"Kila mmoja wetu (wachezaji), anatambua ukubwa wa timu hii, tupo hapa ili kuifanya kuendelea kuwa bora na kufikia malengo," anasema Mwamnyeto.