NDINGA KALI: Kwenye magari Salah usimguse
Muktasari:
- Kwa upande wa magari mmoja kati ya wachezaji wenye starehe hizo ni Mohamed Salah ambaye ana magari mbalimbali ya kifahari ya aina mbalimbali kwenye maegesho yake.
LIVERPOOL, ENGLAND: WACHEZAJI wengi wa mpira wa miguu huwa na starehe ya kununua vitu mbalimbali vya thamani kama saa, boti, nyumba, vito na wengine magari.
Kwa upande wa magari mmoja kati ya wachezaji wenye starehe hizo ni Mohamed Salah ambaye ana magari mbalimbali ya kifahari ya aina mbalimbali kwenye maegesho yake.
Hapa tumekuletea ndinga zote anazomiliki staa huyu pamoja na thamani yake na uwezo wake kwa ujumla.
Bentley Continental GT
Salah anapenda gari za aina hii na kwa sasa anamiliki mbili. Inakadiriwa kuwa na thamani ya Pauni 160,000.
Ndani yake ina mandhari mazuri ikiwa ni pamoja na viti vya ngozi na ina kasi ya karibia kilomita 210 kwa saa pia ina injini ya V12.
Mashabiki wengi wanalijua gari hili na wanapoliona baadhi huwa wanalikimbilia kwa ajili ya kupata picha na staa huyo.
Bentley Bentayga
Moja ya magari ya kifahari zaidi lenye milango minne. Ilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015 na ikawa gari linalotakiwa sana na wachezaji wa soka wengi duniani kote.
Mbali ya Salah, Kyle Walker na Raheem Sterling pia wanalimiliki.
Mifano ya 2016 ilijivunia kuwa na injini kubwa ya twin-turbo W12. Wakati zinatoka zilikuwa zinauzwa kwa karibia Pauni 170,000.
Porsche 911 Turbo S
Gari hili la kifahari aina ya 911 Turbo S lina turbo mbili.
Kwa saa moja, gari hili linaweza kukimbia kwa kasi ya kilomita 205 kwa saa na ndio lenye kasi zaidi kuwahi kutengenezwa na kampuni ya Porsche, na hadi sasa Salah bado anamiliki gari hili. Bei yake inakaribia Pauni 100,000.
Lamborghini Aventador
Kama ilivyo kwa mastaa wengi wa soka, Salah pia ana Lamborghini Aventador katika maegesho yake.
Ndinga hii ina uwezo wa kufikia kasi ya juu ya kilomita 218 kwa saa na ndio lenye kasi zaidi analomiliki kwa sasa, kwa mujibu wa taarifa mbalimbali gari hili bei yake inaanzia Pauni 270,000 hadi 500,000.
Mercedes-Benz AMG GLE Coupe
Wachezaji wengi wanapoenda mazoezini hupendelea kuendesha gari lenye nafasi ya kutosha ndani.
Hii ndiyo sababu wengi wao huwa wanamiliki magari kama Range Rovers na Bentley Bentayga.
Kwa upande wa Salah anamiliki ndinga hii ambayo thamani yake dukani inafikia Dola 129,050.
Gari hili amekuwa akilitumia zaidi kwenda mazoezini ambapo ameonekana nalo mara kadhaa.
Mercedes-Benz SLS AMG Roadster
Huli ni moja kati ya magari ya bei ya juu ambayo Mercedes imewahi kuyaingiza sokoni, lakini hiyo haikumzuia Salah kulinunua mwaka 2022.
Ndinga hii ina uwezo wa kukimbia kwa kasi ya kilomita 197 kwa saa moja. Bei yake ni Pauni 175,000.
Audi Q7
Mastaa wengi wamekuwa wakitumia gari hizi zinazotengenezwa huko Ujerumani.
Salah aliinunua aliporejea England kujiunga na Liverpool akitokea Roma mwaka 2017.
Wachezaji wengi maarufu wa Barcelona walitumia Q7 kwenda na kurudi mazoezini hadi mkataba wa udhamini wa kampuni inayoyatengeneza na timu yao ulipomalizika.
Bei ya gari hili inaanzia Pauni 67,000.