Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kefa kawaridhisha Mashujaa, wengine wanalalamika

Muktasari:

  • Ni msimu wenye mbwembwe nyingi. Wimbo wa Rose Muhando unaimbwa kila baada ya mchezo mmoja, lakini sauti ya wimbo wa Mwana FA na Jay Moe kwenye wimbo wao ambao uliteka sana kipindi cha nyuma ‘Ingekuwa Vipi’ imekuwa ikisikika kwa mbali sana kwenye kila mechi inayohusisha Simba au Yanga.

SIMBA wamefurahi, Mashujaa FC wamekiri kuwa walizidiwa, lakini wengine wanalalamika kuwa mechi haikuwa fea. Huu ni mwendelezo wa Ligi Kuu Bara ambayo kwa sasa imebakiza mechi tatu hadi nne ili kumalizika, lakini Simba bado mziki ni mzito.

Ni msimu wenye mbwembwe nyingi. Wimbo wa Rose Muhando unaimbwa kila baada ya mchezo mmoja, lakini sauti ya wimbo wa Mwana FA na Jay Moe kwenye wimbo wao ambao uliteka sana kipindi cha nyuma ‘Ingekuwa Vipi’ imekuwa ikisikika kwa mbali sana kwenye kila mechi inayohusisha Simba au Yanga.

Labda unaweza kusema kuwa ni msimu mgumu kwa timu mbili, tofauti na mingine kadhaa iliyopita huu unaweza kwenda hadi kwenye mchezo wa mwisho bila kufahamika nani anakuwa bingwa wa nchi, labda ndiyo kipimo cha ligi bora.

Kwenye Uwanja wa KMC Complex juzi ilipigwa mechi ya kiporo kati ya Simba ambao walikuwa wenyeji wakivaana na Mashujaa, kabla ya mchezo harufu kuwa kuna timu imeahidiwa milioni 100 ikishinda na 50 milioni ikitoa sare ilikuwa inafuka kila sehemu.

Hii ni hali ya kawaida kwenye soka letu kwa sasa, kuna watu wanakula fedha kutoka kwa waajiri feki na hii imekuwa ikiongeza hasira kwa wanaotarajia kula fedha, wanaotoa fedha na wale ambao wanatumika kama daraja la watu kupata fedha. Nafikiri unanielewa ukitulia.

Kwenye mchezo huo kila mmoja alitarajia kile ambacho kilifanywa na Simba, wakati wanawaza kuwa Mei 25 wanaweza kuwa na uhakika wa kuzoa 4 bilioni kutoka kwenye Shirikisho la Soka Afrika (Caf), endapo watafanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho, kikosi hicho chini ya Fadlu Davids kilibadilisha nyota wake kwa sehemu kubwa.

Wazo lilikuwa ni Mashujaa siyo bora kama Berkane, lakini kichwani pointi tatu za mchezo huo zilikuwa muhimu sana kuendelea kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara, siyo dhidi ya Mashujaa bali dhidi ya watani wao wa Jadi Yanga ambao wanaongoza ligi kwa sasa.

Kwa kawaida kila mmoja alitegemea kwa makali ambayo Simba imeonyesha kwenye Kombe la Shirikisho Afrika basi mashabiki wangekuwa wengi kwenye mchezo huu wa Mashujaa, lakini wapi, sidhani kama walifika elfu tatu, labda wamezoea kushinda.

Kibegi cha Uamuzi kinaanza na mwamuzi Kefa Kayombo na Neema Mwambasha. Kefa alikuwa ameshikilia filimbi katikati ya uwanja na Neema alikuwa kibendera pembeni.

Achana na picha zilizotembea baada ya mchezo huo. Hilo ni la kawaida kwenye soka hata Ulaya hiyo ipo na kuwasaidia tu ni kwamba kabla hujawa mwamuzi kwenye soka la Tanzania lazima uwe shabiki wa Simba au Yanga. Kama huamini kutana na watoto wa shule ya msingi leo halafu jaribu kuwauliza ni mashabiki wa timu gani? Watakujibu. Tuachane na hilo.

Kefa ana mazuri yake mengi, lakini kwenye mchezo huo alikuwa na makosa yake pia. Naomba nimuulize kwanini Seif Karihe ambaye alitoka kwenye benchi na kuingia uwanjani kuzozana na waamuzi alibaki kwenye mchezo hadi mwisho? Kwenye picha za marejeo zinaonyesha kuwa hakuwa mchezaji anayestahili kubaki alifanya kila vurugu kwenye mchezo huo achana na zile za baada ya mchezo kumalizika.

Lakini kama Kefa aliamua kutumia busara sawa. Nilimuona Abdulnassir Gamal ambaye baadaye alikaa langoni kwenye kikosi cha Mashujaa baada ya aliyekuwa kipa wa timu hiyo Patrick Munthari kupewa kadi nyekundu aliondoka uwanjani na kwenda vyumbani kufanya nini?

Nani alimruhusu kutoka kwenye eneo la kuchezea na mbona aliporudi hakukuwa na adhabu yoyote? Labda Kefa aliamua kutumia busara, lakini kikanuni alitakiwa kuadhibiwa.

Sina shaka na dakika 15 alizoongeza Kefa kwenye mchezo huo kwa kuwa Mashujaa waliamua kutumia muda mwingi kupoteza na kipindi cha kufanya mabadiliko ya kimpira tu zilitumika dakika saba, achana na zile nyingine za matukio mengine. Ila shaka yangu kwa Kefa na Neema ni penalti ya mwisho ya Simba ya dakika 90+19.

Neema aliona tukio lile na kunyoosha kibendera chake kuashiria kuwa ni faulo, lakini Kefa alipofika eneo la tukio aliamuru ni mkwaju wa penalti - macho yangu yanaonyesha kuwa hakukuwa na uhalali wa mkwaju ule wala faulo, labda kama Kefa atakwenda kujiridhisha akiwa nyumbani kwa kuwa uwanjani hakukuwa na VAR.

Hata hivyo, Simba walishangilia mwishoni, Mashujaa wakasema wameridhika na matokeo, lakini wasiohusika na mchezo walilalamika kuwa Mashujaa wameonewa. Ndivyo soka letu kwa sasa lilivyo, kesho itakuwa tofauti, wanaolia wana faida kuliko waliopigwa.