Nchi ina viwanja visivyosaidia kukidhi mahitaji ya soka
Muktasari:
Ni eneo muhimu ambalo wadau wa soka wamekuwa wakilichukulia kirahisi na kuona kana kwamba soka linaweza kujengwa toka ngazi ya chini kwa kuchezwa sehemu yoyote.
UWANJA wa kuchezea ni moja kati ya mahitaji muhimu na makubwa katika kujenga misingi ya uchezaji wa mpira wa miguu. Ni eneo muhimu ambalo wadau wa soka wamekuwa wakilichukulia kirahisi na kuona kana kwamba soka linaweza kujengwa toka ngazi ya chini kwa kuchezwa sehemu yoyote.
Sehemu ambayo ni ilimradi kuwe na eneo la kukimbiakimbia, lakini ukweli ni kwamba uwanja unatajwa kama Sheria Namba Moja ya Soka katika Sheria 17. Pamoja na kutajwa kwake haimaanishi liwe na eneo linaloitwa uwanja wa kuchezea tu, bali linatakiwa liwe ni kiwanja sahihi chenye vipimo sahihi na eneo lake la kuchezea liwe sawia ‘smooth’, likiwa na nyasi nzuri zinazowezesha mpira kutembea.
Kwa hapa nchini mambo ni tofauti sana kama ilivyo kawaida ya kila kitu kuchukuliwa kisiasa zaidi, wadau wa soka wanalia mno kusahauliwa kwa jambo hilo. Uwanja. Hata wanasiasa wenye mirengo yao ya kusaka uongozi ndani ya jamii hukimbilia kuanzisha mashindano hasa ya soka yakishirikisha vijana ambao ndio walengwa kwa kuamini kupitia mikusanyiko hiyo, ujumbe wa mwaandaji huyo itawafikia kwa urahisi vijana na hatimaye kutimiza malengo yao ya siasa. Lakini wanasiasa hao huwa hawaangalii mahitaji ya vijana kwenye michezo yanaanzia wapi, kwani hata viwanja vinavyotumika kuendesha mashindano hayo huwa havikidhi dhana ya michuano hiyo kuinua na kukuza vipaji.
Kwa sababu huwezi kuvumbua kipaji katika kiwanja chenye mchanga mtupu au katika kiwanja kilicho na mashimo kama kilichopigwa mabomu. Hii ni kwa sababu wachezaji hao wakitoka katika michuano hiyo baada ya kuibuliwa hawaendi kucheza kwenye viwanja vya mashimo. Pia ni wapi unaweza kukiona kipaji kwenye uwanja ambao mpira unachezwa na kupigwa juu kwa juu tu. Si rahisi. Bado wadau wengi wataendelea kulia na umaskini wa wachezaji wachache wenye vipaji kwa sababu ya tatizo la viwanja. Wadau wataendelea kuimba wimbo wa soka, lazima lianzie chini kuliko na watoto, hata viongozi wakiwamo Mawaziri wanapofungua mashindano kadhaa au mikutano ya TFF na imemtokea hata Rais Jakaya Kikwete kuzungumzia timu kuwa na vyanzo vya wachezaji.
Wote wanazungumzia kuwa ni lazima soka lianzie chini kwenye vipaji, lakini maajabu yake na swali la kujiuliza ni wapi watoto wanaweza kucheza vizuri kwa uhuru mkubwa? Viko wapi viwanja vya kuchezea na kujifunza mpira kila siku?
Ukiacha maeneo ya wazi yaliyokuwa na viwanja angalau kidogo vya kuchezea soka, kwa sasa karibu vyote yamekuwa ni makazi ya watu, hakuna ramani zinazofuatwa katika maeneo yanayojengwa kila siku zinazoonyesha eneo hili ni la viwanja.
Kuanzia ramani za vitongoji mpaka miji watu wanajijengea tu, hata shule za msingi na sekondari zilizojengwa miaka ya hivi karibuni hazina viwanja vya michezo! Unajiuliza ni vipi shule inaweza kuanzishwa bila viwanja vya kuchezea wanafunzi, haki ya kujumuika na kushiriki michezo iko wapi? Hivi hakuna vipengele vya Sheria za Ujenzi wa Shule zinazombana mtu au taasisi inayotaka kujenga shule au chuo kuwa na ulazima wa viwanja?
Maeneo mengi ya jijini Dar es Salaam yaliyokuwa wazi yakitumika kuendelezea vipaji vya soka yanakwisha si Jangwani, Biafra au kwingineko yote yanachukuliwa na mamlaka au watu ili kujenga nyumba ambazo zingeweza kujengwa nje ya mji na watu wakaishi. Kwa sasa yamesalia maeneo ya Kawe na Mwembeyanga, ambayo bila shaka yanamezewa mate na watu wengi sana ili kubebwa. Siyo Dar es Salaam pekee, jambo hilo lipo hata mikoani huwezi kuwakuta vijana wanacheza mpira kila siku kwani maeneo mengi yamechukuliwa na watu, ni aibu sana unapoliona eneo kubwa kama la Tegeta likiwa halina viwanja vya kutosha, nenda Ubungo, Ilala na kwingine uone. Sasa hawa vijana wanaanzia kucheza wapi? Viwanja viko wapi? Bila shaka wimbo huu utaendelea kuimbwa tu, lakini waimbaji wake hawajui wanaimba nini! Viwanja vimekuwa ni tatizo kubwa katika kufanikisha ligi mbalimbali ikiwamo kuzuia kumalizika mapema, lakini kikubwa vimekuwa ni kikwazo kikubwa katika kuongeza ladha ya soka Tanzania. Mapema wiki chache zilizopita tulisikia malalamiko mengi yakihusiana na Uwanja wa Mkwakwani Tanga ambao wadau wa soka wanasema haufai hata kidogo kuchezea Ligi Kuu, ni Uwanja unaonyima raha mchezaji kumiliki mpira kadri anavyotaka. Uwanja unawanyima wachezaji kucheza soka zuri linalotakiwa kuchezwa na pengine kushindwa kutoa matokeo ambayo yangekuwa sahihi. Hali ilikuwa ni mbaya hasa baada ya Mgambo JKT kuifunga Simba ndipo ubaya na uzuri wa uwanja ulipoanza kuonekana zaidi. Lakini siyo Uwanja wa Mkwakwani tu, ndiyo ulio katika hali hiyo mbaya, viwanja vingine kama cha Jamhuri, Morogoro ambacho wanachezea Polisi na Mtibwa Sugar siyo kiwanja rafiki kinachoweza kuwapa wachezaji nafasi nzuri ya kucheza soka maridadi na kwa uhuru. Ni uwanja ambao ukiuona kwa juu juu tu utadhani nyasi zake zipo vizuri, lakini ndani ya eneo la kuchezea (pitch) uwanjani hapo kuna miinuko na mashimo mengi madogo madogo yanaufanya mpira kushindwa kutambaa na unakuwa ukidundadunda bila mpangilio.
Uwanja wa Sokoine Mbeya, Nangwanda Sijaona Mtwara na vingine vinavyochezewa ligi mbalimbali nchini bado havipo kwenye ubora unaotakiwa hivyo kuharibu utamu wa soka unaotakiwa. Tatizo hilo ni moja ya pigo kubwa linauharibu mpira wa Tanzania. Ndiyo maana binafsi sikukilaumu sana kiwango kilichoonyeshwa na timu ya Taifa pale mjini Mwanza kwenye Uwanja wa Kirumba siku ilipocheza na timu ya Taifa ya Malawi na kutoka sare ya bao 1-1. Moja ya sababu kubwa zilizoufanya mchezo ule kukosa ufundi ni hali ya uwanja ilivyokuwa.
Kirumba ya sasa siyo ule wa miaka kumi au ishirini iliyopita, siyo uwanja wa kujivunia tena, uwanja una vijishimo vingi, vichuguu vidogo vidogo kwa ndani na kama tulivyouona siku ile mvua zinaponyesha ni tatizo. Kiutaalamu viwanja hivi vilitakiwa kila baada ya miaka kumi kuondolewa udongo wote pamoja na nyasi zote na kisha udongo na nyasi mpya zinapandwa, lakini hali haiko hivyo kwa viwanja vingi nchini. Pamoja na uzuri wote ilivyokuwa navyo baadhi ya viwanja leo hali haiko hivyo nenda hata katika Uwanja wa Nelson Mandela Sumbawanga, Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Jamhuri, Dodoma, Majimaji Songea na Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kwa sasa si mali kitu tena.Viwanja vilivyokuwa bora sana kwa sasa si bora tena zaidi ya kuwa majangwa au sehemu ya kulishia mifugo. Katika hili soka la Tanzania litaendelea kuwa bovu kila tutakapokuwa tukiziona timu zetu zikicheza, hatuwezi kuja kuliona soka zuri lilikuwa lichezwa na Ushirika Moshi, Pamba ya Mwanza, Mecco ya Mbeya au Majimaji Songea kwani viwanja ni tatizo kubwa.