Mzengela: Bondia aliyenusurika kuchomwa moto kwa wizi

Muktasari:
- Katika mahojiano na Mwanaspoti, bondia huyo kazungumzia mambo mbalimbali ikiwamo ndoto yake ya kwanza kucheza soka nafasi ya beki namba tatu na kiungo, lakini baada ya kuona mzunguko wa pesa unakuwa mgumu akaanza kutumia njia za mkato.
UKIMTAZAMA mwonekano wake huwezi kuamini kwamba ni mtu aliyewahi kufanya matukio ya kutisha na kuogofya mtaani kipindi cha nyuma kabla mchezo wa ngumi kumbadilisha kitabia. Huyo ni bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Mwinyi Mzengela (39).
Katika mahojiano na Mwanaspoti, bondia huyo kazungumzia mambo mbalimbali ikiwamo ndoto yake ya kwanza kucheza soka nafasi ya beki namba tatu na kiungo, lakini baada ya kuona mzunguko wa pesa unakuwa mgumu akaanza kutumia njia za mkato.
Mzengela anawataja wachezaji aliokuwa anapenda kuwatazama kutokana na vipaji vyao kuwa ni pamoja na Athuman Idd 'Chuji' na Haruna Moshi 'Boban'.
"Nimecheza sana timu za mtaani, ila niliyopandishwa kutoka U-20 ilikuwa Polisi Dodoma ambako sikukaa kwa muda mrefu baada ya kukengeuka," anasema Mzengela, shabiki wa Yanga anayemkubali Aziz Ki kutokana na ubora wake, kiungo aliyeondoka katika timu hiyo.

ALICHOMWA MOTO
Mzengela anasema kuna matukio kibao ambayo amekutana nayo maishani mwake, lakini lile la kuchomwa moto lilikuwa la aina yake.
"Tukio lililosababisha nichomwe moto. Nilikuwa naishi Dar es Salaam nilifanya matukio ya uporaji simu, bajaji, bodaboda hivyo nikawa natafutwa sana ikabidi nitafute maficho. Kwa mara ya kwanza nilikimbilia Shinyanga kuna sehemu moja ilikuwa inaitwa Ndala ya Juu ambako nilikuwa nauza maji," anasema na kuongeza:
"Baada ya kuona mambo hayaendi nilikuwa mchezaji mzuri wa mpira wa miguu, nilikuwa nacheza namba tatu. Ikabidi nikajiunga na Polisi Dodoma nilianzia U-20 kisha nikapandishwa, ila kwa bahati mbaya nikakutana na marafiki potofu nikaachana na mpira, nikarudi tena kitaa kukaba."
Anasema aliona pesa za uporaji ni nyingi na anazipata kwa haraka, ingawa ilikuwa ni njia ngumu na hatarishi kwa maisha yake.

"Kuna siku tukiwa katika harakati ya kuvunja gari ya sabuni ili tuchukue tukaziuze likapita gari la polisi hatukujua hilo. Akashuka na kupiga risasi juu, tukakimbilia porini na kuanza kurusha mawe hadi tukavunja vioo, alikuwa amefiwa anasafiri kwenda Tabora, akaenda ofisi za kijiji kutoa taarifa za kukamatwa kwetu, mimi nikafanikiwa kukimbia na kurudi Dar es Salaam, ila wenzangu walikamatwa," anasema.
Anaongeza baada ya kupita muda alipoona mambo yamepoa akarudi tena Dodoma kipindi hicho kilikuwa kinajengwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), hivyo akaenda kufanya kazi kama kibarua, ila akajikuta anaishia kufanya tukio.
"Kuna siku niliona Wachina wanapoweka pesa, nikaenda kulibeba begi lilikuwa na Sh20 milioni kisha nikaiba bodaboda ya mtu na kukimbia," anasema.
"Nilipita njia ya pori kwa pori nikajikuta nimetokea kijiji kimoja cha Iringa ambako wanakijiji walikuwa hawajanielewa kwa sababu nilisuka na kuvaa hereni, jambo ambalo halikuwa la kawaida kwao kipindi hicho. Wakanikamata na kunipeleka polisi nikaishia kukaa jela miezi saba na pesa zikapigwa juu kwa juu. Jela nimekwenda mara nyingi kwa matukio tofauti."
Mzengela anasema baada ya hapo alirudi uraiani kuendelea na mishe zake za uporaji na kufanya starehe za kutumia pesa hovyo akiwa hakosi kati ya Sh3 milioni hadi milioni tano.
"Usiku mmoja sikujua kama nimewekewa mtego. Wakati nakwenda kudandia gari ili tuvunje nilikuwa na rafiki yangu alikuwa anaitwa Mbili," anasema na kuongeza:
"Baada ya Polisi kupiga risasi juu ikamfikia mkononi mimi nikashuka haraka na kukimbia kumbe nilikokuwa nakimbilia ambako walikuwepo wanakijiji ambao walikuwa wameshaandaa vitu vya kunichomea moto. Wakaniweka katikati ya tairi nikiwa nimefungwa kamba miguu na mikono. Nikamwagiwa mafuta ya taa kisha wakawasha kiberiti nikaanza kuungua, ila bahati nzuri polisi waliniwahi

"Polisi wakazima moto na kunifungua kamba wakawaambia wanakijiji ni vibaya kujichukulia sheria mkononi. Wakanipeleka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma ambako nilikaa miezi minne. Baada ya hapo washkaji zangu ambao nilikuwa naiba nao wakaja kuniiba, walihofia nikipelekwa vyombo vya sheria nitawataja.
"Nikapelekwa maskani, walijitahidi kuniuguza. Baada ya kupata nafuu nikarudi Dar es Salaam, nikawa nakaa ndani tu vidole vya mikononi na miguuni vilikuwa vimebanana nikawa napitisha wembe kati kukata viachane, nikakosa tumaini ya kuishi ila kadri muda ulivyokuwa unaenda nikaanza kupona na kurudi kucheza mpira mtaani. Changamoto ilikuwa nikikaa bila kutembea vitu vilikuwa vinatembea mwilini.
"Makovu unayoyaona yalitokana na moto, sina meno mawili moja lilitoka wakati naiba nikapigwa ngumi, lingine lilivunjika nikiwa ulingoni katika pambano."

VIFO VYA KUTISHA RAFIKI ZAKE
Mzengela ana mengi aisee! Hapa anasimulia namba alivyoshuhudia vifo vya kutisha vya rafiki zake enzi hizo akiwa kibaka.
"Kuna siku tulivamia gari kumbe kule nyuma kulikuwepo na jamaa wamejipanga. Wenzangu wawili wakawa wamebanwa, nilikuwa nimebeba sime na kisu kidogo. Nilipoona nachelewa kutoa sime nikachomoa kisu kidogo na kuanza kuwachoma bila kuangalia nawachoma wapi. Wakaniachia nikaruka chini," anasema.
"Wakamshika mshkaji wa kwanza walikuwa na mitungi ya gundi wakamwingiza hadi tumboni akawa anatoa chakula chote alichokula kisha ikaanza kutoka gundi sehemu zake zote za siri. Wakamshika wa pili wakamuweka katikati ya tairi kisha wakawasha gari. Yote hayo niliyashuhudia nikiwa porini. Nikarudi nyumbani, nikapiga goti na kumuomba Mungu anisaidie kuacha hizo tabia.
"Baada ya siku tatu kutoonekana wazazi wa wale wenzangu wakaanza kuuliza wenzangu walipokuwa, nikawaambia sijaonana nao siku ya nne, ila kama mnavyojua mishe zao ni barabarani. Wakaanza kuwatafuta wakawakuta barabarani wakiwa vibaya mno.. kifupi nimeshuhudia wenzangu wengi wanakatwa na panga hadi wanakufa."

NGUMI ZAMBADILI TABIA
Bondia huyo anasema historia mbaya ya maisha yake ni chanzo cha kuingia katika mchezo wa ngumu na bondia aliyemshawishi kwa mara ya kwanza ni Kanda Kabongo aliyemwambia matukio aliyoyafanya anaweza akafanya vizuri na maisha yake kubadilika.
"Kabongo alihamia mtaani kwetu akawa anaona utukutu niliokuwa naufanya, akanifuata akasema mchezo wa ngumi unahitaji uvumilivu kwa mambo uliyoyapitia unaweza kuwa bondia mzuri...gym ya kwanza kunipeleka ilikuwa ya Japhet Kaseba," anasema na kuongeza:
"Kabongo wakati huo alikuwa anajiandaa na mapambano ya kwenda nje. Baada ya kuondoka nikajihisi kupoteza matumaini ndipo nikakutana na Rashid Nassor, ni mwanajeshi akaniendeleza kimchezo na kujitoa kunisimamia.
"Alikuwa analala uani nyumbani nikitoka tu ananidaka mkono na kuniuliza unaenda wapi hadi nilikuwa naenda naye kazini kwake. Aliapa kunibadilisha na akafanikiwa ingawa baadaye akaenda katika majukumu ya kitaifa Dafur, nikahamia gym ya Big Light na Mkumbange ambako nikawa nafanya mazoezi na mabondia mbalimbali kisha nikaanza ngumi hadi sasa ni bondia wa kulipwa."
Mzengela anakiri kwamba ngumi zimemsaidia amekuwa mfano wa kuigwa kwa vijana, kwani nje na wizi alikuwa anatumia dawa za kulevya, bangi, sigara na kunywa pombe za kila aina ila kwa sasa anaswali na ni mjumbe msaidizi wa mtaa anakoishi Mwananyamala, Dar es Salaam.
"Kuacha dawa za kulevya inawezekana. Mimi nilikuwa nafanya sana mazoezi sikuwa na muda wa kuviwazia hivyo tena. Nikisikia hamu natafuna bigijii. Kwa sasa nakunywa maji na vinywaji vya sukari. Nachukia kila kitu nilichokuwa nafanya nyuma na nimekuwa mshauri mkubwa wa vijana na wengine wengi wamebadilika," anasema.
"Nimeoa, mwanamke wangu wa kwanza nilizaa naye watoto wawili mmoja yupo chuo na wa pili aliacha akiwa kidato cha kwanza ni mtukutu na anapenda mpira. Mwanamke wa pili nina watoto wawili naye. Ndege ambazo nilikuwa naziona angani kwa sasa nazipanda. Kiukweli nawaambiwa vijana waepuke pesa za haraka."
Kupitia ngumi anasema amejenga nyumba, anamiliki bodaboda, anasomesha watoto tofauti na pesa haramu ambazo alikuwa anazipata na kuzitumia kwa starehe.
"Nimecheza mapambano 32, nimepoteza mapambano 10, nimedroo mawili yaliyobaki nimeshinda. Nje ya nchi nimecheza Malawi dhidi ya Salum Chazama nikapoteza, Uganda Surei Segalla, Dubai jina lake nimesahau na pambano la Italia tulichelewa kufika tukakuta limepigwa. Pia nilikwenda Dubai," anasema Mzengela ambaye anawataja Mike Tyson, Francis Cheka na Kaseba kuwa mabondia aliokuwa anawakubali sana.
Akizungumzia maisha mengine enzi zake, bondia huyo anasema: "Kipindi ambacho nilikuwa mhalifu sikuwahi kumpa mwanamke vitu isipokuwa pesa, maana nilikuwa naogopa kuua, kwani unaweza ukamnunulia gauni halafu unakuta kasimama na mwanaume mwingine ama simu anaitumia kuwasiliana na mwanaume mwingine. Niliamini nikimpatia pesa akinunua vitu nitakuwa sivijui."