MZEE WA UPUPU: Kuna nini kwa Arajiga

JANA, Jumanne Septemba 20, 2022 ni siku ya 14 kamili tangu mwamuzi kutoka Manyara, Ahmed Arajiga kuvurunda kwenye pambano bora la Ligi Kuu Bara hadi sasa kwenye Ligi Kuu. Pambano hilo la sare ya mabao 2-2 lilikuwa kati ya Yanga na Azam lililofanyika Uwanja wa Mkapa, Septemba 6, 2022.

Katika mchezo huo Arajiga alionyesha udhaifu katika uwezo wa kutafsiri sheria za mchezo soka. Alishindwa kufanya uamuzi sahihi kwa Sospeter Bajana wa Azam ambaye alistahili kadi mbili za njano ambazo zingezaa nyekundu. Alishindwa kufanya uamuzi sahihi kwa Bernard Morrison ambaye alistahili kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumkanyaga tumboni makusudi Lusajo Mwaikenda wa Azam.

Pia alishindwa kufanya uamuzi sahihi kwa Bakar Mwamnyeto aliyestahili angalau kadi ya njano katika matukio manne, lakini hakuonyeshwa hata moja. Alishindwa kufanya uamuzi kwa shambulizi lililozaa bao la kwanza la Yanga ambalo mpira ulitoka kabla ya majaro ya Joyce Lomalisa.

Lakini pia alishindwa kufanya uamuzi sahihi kutoa penati isiyo sahihi kwa Yanga kufuatia kudanganywa na Bernard Morrison.


ONA HII

Agosti 30, mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitoa taarifa ya kufungiwa waamuzi wawili wa Ligi Kuu. Kwanza alikuwa Ahmada Simba aliyechezesha mechi kati ya Singida Big Stars na Mbeya City, Agosti 21 yaani siku tisa nyuma yake.

Mwamuzi huyo kutoka Kagera alifungiwa miezi mitatu baada ya kutenda kosa la kushindwa kutafsiri vyema sheria za mpira wa miguu hasa katika tukio la adhabu ya mkwaju wa penalti iliyowapatia Singida Big Stars bao la kwanza katika ushindi wao wa mabao 2-1.

Mwamuzi mwingine aliyekutana na adhabu siku hiyo alikuwa yule aliyechezesha mchezo kati ya Coastal Union dhidi ya Yanga uliofanyika Agosti 20, 2022 jijini Arusha. Mwamuzi huyo anayefahamika kwa jina la Raphael Ikambi kutoka mkoani Morogoro aliondolewa kwenye ratiba ya waamuzi kwa mizunguko mitatu baada ya kushindwa kufanya uamuzi sahihi kwa mujibu wa sheria za mpira wa miguu katika tukio ambalo mchezaji wa Coastal Union, Mteje Albano alimchezea mchezo hatarishi na usio wa kiungwana mchezaji wa Yanga, Yanick Bangala.RUDI KWA ARAJIGA

Makosa haya yaliyowafanya waamuzi hawa wawili waadhibiwe ndani ya siku 10 tangu wayafanye yalifanywa na Arajiga peke yake kwenye mchezo mmoja, lakini leo ni siku 14 hajachukuliwa hatua yoyote.

Nani anamlinda Arajiga? Arajiga huyohuyo alivurunda tena kwenye mchezo wa Tanzania Prisons na Simba, Septemba 14, kwenye uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Alishindwa kufanya uamuzi sahihi kwa Simba pale mshambuliaji Moses Phiri alipofanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na kipa wa Tanzania Prisons, Hussein Abel Thomas.

Simba walistahili penalti kwenye tukio hilo, lakini Arajiga alishindwa kufanya uamuzi sahihi. Mtu unabaki unajiuliza huyu Arajiga ana mjomba wake pale TFF? Au ana kiongozi mmoja mkuu hivyo kiongozi huyo anamlinda kuogopa kuaibika?

Msimu uliopita Arajiga alivurunda kwenye mchezo wa Coastal Union dhidi ya Mbeya City na kufungiwa mizunguko mitatu Ligi Kuu Bara. Lakini cha ajabu mwisho wa msimu akawa mwamuzi bora.

Mtu unajiuliza, huyu Arajiga analindwa na nani pale TFF? Anawezaje kuwa mwamuzi bora ilhali alivurunda kiasi cha kufungiwa? Siyo bure, lazima Arajiga kuna kinachomlinda pale Karume. Inafikia kipindi mtu unaangalia mchezo wa Ligi Kuu ukimuona Arajiga katikati basi jiandae kuona matukio ya ajabu.

Wakati Ligi Kuu ikiwa katika mzunguko wa nne tayari Arajiga ameshavurunda katika mechi mbili. Kwa makosa ambayo ameyafanya waamuzi wenzake wangekuwa wameshafungiwa, lakini yeye anadunda tu. Hapa tunapoongea ameshapangwa mechi nyingine.


YATAKUJA YA KENYA

Nchini Kenya, mashabiki wa soka walichoshwa na mambo kama haya. Waamuzi wanaharibu mchezo, mamlaka hazichukui hatua, basi wakaanza kuchukua hatua wenyewe. Mwamuzi akiharibu mchezo watu watamtafuta hata kwenye daladala (kule wanaita matatuu), halafu mtu anamsogelea na kumtegua hata mguu.

Akimkanyaga tu, basi jamaa anamjia juu na kumletea zogo wanakuja wenzake kumsaidia mwamuzi anapigwa na watu wanadhani ni ugomvi wa kawaida wa abiria kumbe ni kisasi cha uwanjani. Kocha wa Kagera Sugar, Francis Baraza na yule wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo wanajua zaidi mkasa huu kwa sababu ulitokea wakati wakiwa makocha kule.

Waamuzi walipigwa mitaani kwa mtindo huu hadi kuja kushtuka kwamba hivi ni visasi vya uwanjani. Hawa kina Arajiga kama wanalindwa na mamlaka, ni vyema waachwe hatua za kisheria zichukue mkondo wake. Arajiga ni vyema aachane na hiyo tabia inayomsababishia kulalamikiwa mara kwa mara. Huu mpira ni mkubwa kuliko kawaida.