MZEE WA UPUPU: Kauli ya Bumbuli na kumbukumbu ya msimu wa 1971

MKUU wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli, alinukuliwa juma lililopita akisema wao hawautambui mchezo wa marudiano dhidi ya watani wao, Simba, Julai 3 mwaka huu.

Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika Mei 8, 2021 lakini ukaahirishwa kutokana na sintofahamu iliyotokea siku hiyo.

Wakati wengi tukiamini pambano hilo litafanyika siku hiyo, ghafla tukamsikia Bumbuli akisema aliyoyasema na kutuacha vinywa wazi.

Japo baadaye kauli yake ilikanushwa na wakuu wake, lakini tayari ilitosha kutufanya wahenga tugonge kengele ya tahadhari kwenye vichwa vyetu tukirejea matukio ya nyuma ambayo mazingira yake yalikuwa kama haya.

Niliwahi kuandika hapa namna ambavyo Watani hawa wa Jadi wameshawahi kukimbiana, sasa leo nataka nielezee mkasa msimu wa 1971 ambao ulikuwa na sintofahamu kubwa ambayo haijawahi kutokea ikiwahusisha Yanga hawa hawa na mechi za marudiano hii ya Julai 3.


MKASA WENYEWE

Ligi ya Taifa mwaka 1971 ilihusisha timu za; Yanga - Dar Es Salaam (Pwani), Balimi - Bukoba (Ziwa Magharibi - sasa Kagera), Coop United (Mwanza), Spurs United (Morogoro), Mwadui (Shinyanga Young Boys (Tabora), Mwanga (Kigoma), Coastal Union (Tanga), CCP (Moshi), Kilimo (Mara) na Dundee United (Dodoma).

Wakati huo ligi ilichezwa kwa mtoano hadi fainali. Yanga wakatinga fainali kwa kuitoa Mwadui FC ya Shinyanga kwa bao 1-0 kwenye nusu fainali uliyojaa utata.

Wakiwa nyuma 1-0, Mwadui walitoka uwanjani (Taifa - sasa Uhuru) wakilalamika kwamba wachezaji wao walikuwa wakishambuliwa kwa mawe na mashabiki wa Yanga. Mwadui walitaka nusu fainali irudiwe, irudiwe, lakini FAT walikataa na kuwatambua Yanga kama washindi hivyo kutinga fainali.

Walikutana na Dundee United ya Dodoma na kushinda fainali hiyo na FAT iliwatambua Yanga kama mabingwa wa Tanzania 1971.

Lakini Baraza la Michezo, BMT, likaamuru nusu fainali na fainali Zirudiwe!

Ilianza nusu fainali ambapo siku ya marudiano, Mwadui walifika uwanjani lakini siyo Yanga wala waamuzi, wala viongozi wa FAT, wala mashabiki waliotokea uwanjani.

Mwadui walijipiga piga danadana uwanjani na kutoka wakijihesabia wameshinda na kutinga fainali.

Siku ya fainali walienda uwanjani na kuwakata Dundee wanawasubiri, walicheza nao na kushinda 2-1 na kujihesabia mabingwa wa Tanzania.

FAT ilikaa kimya bila kutoa ufafanuzi wowote huku Dundee United wakisema mchezo wao ulikuwa wa kirafiki, siyo fainali.

BMT iliibuka tena na kusema mechi hizo zirudiwe tena.

Siku ya marudiano ya nusu fainali, Mwadui nao hawakutokea uwanjani.

Cha ajabu, viongozi wa FAT, waamuzi na mashabiki waliotokea siku hiyo, kasoro Mwadui.

Yanga walipewa ushindi wa mezani na kutinga fainali.

Walikutana na Dundee United na kushinda 5-1 na kuwa mabingwa.


VIPI SIMBA

Kwenye timu zilizoshiriki ligi ya taifa 1971, Simba ambayo wakati huo ilikuwa Sunderland, haipo. Hebu angalia tena hapo!

Naam, Sunderland haikushiriki Ligi ya Taifa mwaka huo baada ya kususia.

Ni kwamba utaratibu wa mwaka huo ligi zilianzia ngazi ya wilaya, mkoa na baadaye ndiyo taifa, hakukuwa na madaraja.

Kwenye ngazi ya wilaya, timu zote za wilaya zilishiriki, halafu zinapatikana zitakazofuzu kuingia ngazi ya mkoa na baadaye ngazi ya taifa. Sasa kwenye ligi ya Mkoa wa Pwani kulikuwa na timu za Sunderland, Cosmopolitan, Tambaza na Yanga.

Sunderland waliigomea ligi hii na kujitoa kabisa kuwa sehemu ya msimu wa 1971. Hii ndiyo sababu huwaoni pale juu.

Kwa hiyo sisi wahenga tunapomsikia Bumbuli anasema hawaitambui mechi ya Julai 3, mawazo yetu yanatutuma kuamini kwamba Bumbuli anafikisha salamu za wenye Yanga yao ambao kiasili malumbano ni sehemu ya historia yao.

Mungu jalia pambano lifanyike lakini zaidi ya hapo, tutarejea matukio ya zamani na kusahau kwamba tuko kwenye zama mpya.