MTU WA PWANI : Usishangae anguko la Singida United hii ya sasa

Muktasari:

Walikuwa na timu hasa na kundi kubwa la watu waliamini kuwa ndio klabu ambayo ingeweza kuleta upinzani kwa vigogo vya soka nchini Simba, Yanga na Azam FC.

MIAKA miwili iliyopita, nyakati kama hizi, Singida United ilikuwa miongoni mwa timu zilizokuwa kwenye nafasi nne za juu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Baada ya kucheza michezo saba, ilikuwa imekusanya pointi 12 baada ya kuibuka na ushindi katika mechi tatu, kutoka sare michezo mitatu huku ikipoteza mechi moja tu.

Ndio kwanza Singida United ilikuwa imetoka kupanda daraja baada ya kusota kwa muda mrefu katika Ligi Daraja la Kwanza lakini ilianza Ligi Kuu ikiwa moto wa kuotea mbali.

Ubora huo wa Singida United haukuja kwa bahati mbaya kwani walikuwa na kikosi chenye kundi kubwa la nyota wa ndani na nje ya nchi ambao walikuwa chini ya usimamizi wa kocha mzoefu Hans van der Pluijm ambaye alitoka kuinoa Yanga.

Unapoitaja Singida United hiyo, unakumbushia kikosi kilichoundwa na wachezaji kama Mudathir Yahaya, Kenny Ally Mwambungu, Tafadzwa Kutinyu, Michel Rusheshangoga, Danny Usengimana, Ally Mustaf ‘Barthez’ na Simbarashe Nhivi.

Walikuwa na timu hasa na kundi kubwa la watu waliamini kuwa ndio klabu ambayo ingeweza kuleta upinzani kwa vigogo vya soka nchini Simba, Yanga na Azam FC.

Hata hivyo, ndani ya kipindi kifupi cha miaka miwili, maisha yameiendea kasi Singida United na sasa imeanza kuingia katika giza nene.

Tofauti na miaka miwili iliyopita, leo baada ya kucheza michezo saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara, wanashika mkia wakiwa na pointi zao tatu walizochuma baada ya kutoka sare kwenye michezo mitatu huku wakipoteza mingine minne.

Wakati kipindi kile wakifunga jumla ya mabao sita na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne tukatika mechi saba, kipindi hiki yenyewe imefunga mabao mawili tu huku yenyewe ikiwa imefungwa mabao saba.

Ni mapema mno kutabiri nafasi ambayo Singida United itamaliza kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu huu, lakini imeshaanza kuonyesha dalili ambazo sio nzuri na zenye kuleta hofu kwa wapenzi na washabiki wake na pengine wadau wa mpira wa miguu nchini.

Kuna sababu nyingi ambazo zinatoa ishara kuwa msimu huu unaweza kuwa wa anguko rasmi la Singida United mbali na hoja ya kutazama msimamo wa ligi ulivyo.

Kwanza imefanya usajili dhaifu kwa kujaza kundi kubwa la wachezaji ambao hawana uzoefu na ubora wa kucheza Ligi Kuu tofauti na timu nyingine, hivyo wanahitaji muda mrefu wa kukaa sawa jambo ambalo linaweza kuwafanya wajikute wakipoteza idadi kubwa ya pointi na kuwaweka kwenye nafasi mbaya katika msimamo wa ligi.

Sio jambo rahisi kupata wachezaji wazuri kwa kufanya usajili kwa mtindo wa kuitisha majaribio na kuwajaza pamoja kama vile shule au taasisi za elimu zinapofanya usaili wa wanafunzi.

Lakini kingine ambacho kinachangia kuwapa watu hofu juu ya kuanguka kwa Singida United ni hali mbaya ya kiuchumi ambayo imeisibu timu hiyo kwa msimu wa pili hivi sasa.

Tofauti na ilivyokuwa kwenye msimu wa kwanza, safari hii kundi kubwa la wadhamini limeikimbia Singida United na hivyo uongozi wa timu hiyo kujikuta upo kwenye wakati mgumu wa kuiendesha hali ambayo imekuwa ikizaa malalamiko ya mara kwa mara ya wachezaji kuhusu kutolipwa stahiki zao kwa wakati na kutopata huduma bora kama ilivyokuwa zamani.

Kinachoikuta Singida United hakijaja kwa bahati mbaya bali ni matokeo ya mbegu ambayo wao wenyewe waliipanda miaka miwili iliyopita.

Matumizi ya anasa na kulazimisha ushindani usio na sababu dhidi ya timu kubwa nchini uliifanya ijikute ikikosa nidhamu ya matumizi ya fedha na kuifanya ijiendeshe kwa hasara msimu uliofuata jambo ambalo lisingetokea kama ingekuwa na mipango sahihi.

Somo ambalo tunajifunza kupitia anguko linaloinyemelea Singida United linapaswa kutumika kubadili fikra na mitazamo ya viongozi wa klabu za soka nchini hasa kwenye masuala ya utawala na matumizi ya fedha katika kuziendesha timu zao.

Klabu zinatakiwa kuzingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na kujenga mifumo imara ya kujiendesha ili kuepuka kile ambacho kinaisibu Singida United kwa sasa vinginevyo hadithi itabakia kuwa ileile kila uchao.

Zisipojifunza kwa hiki kinachoikuta Singida United leo hii, tutegemee kuona kila kukicha zikipigania kutoshuka daraja na kushindwa kuleta ushindani kwenye ligi yetu.