MTU WA PWANI: Elimu ya mikataba inahitajika Ligi Kuu

LEO Jumamosi kutachezwa mechi ya Ngao ya Jamii baina ya Yanga na Simba katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Uwepo wa mechi ya Ngao ya Jamii ni kiashirio cha kufunguliwa kwa msimu wa mashindano ya soka hapa nchini wa 2022/2023.

Siku mbili baada ya mechi hiyo ya watani wa jadi ya Ngao ya Jamii, Ligi Kuu ya NBC kwa msimu ujao itaanza rasmi ambapo jumla ya timu nne zitakuwa katika viwanja viwili tofauti kufungua pazia la ligi hiyo.

Katika Uwanja wa Kassim Majaliwa kule Lindi, Namungo FC itaikaribisha Mtibwa Sugar wakati huo, Ihefu ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Highland Estate kukabiliana na maafande wa Ruvu Shooting.

Wakati Ligi Kuu ikiwa mbioni kuanza, dirisha kubwa la usajili kwa timu za madaraja tofauti nchini linaendelea ingawa linakaribia kufika ukingoni kwani litafungwa rasmi Agosti 31 na baada ya hapo timu hazitokuwa na fursa ya kusajili hadi pale dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa mwezi Desemba.

Kabla hata ligi haijaanza, tayari kumekuwepo na taarifa za uwepo wa migogoro ya kiusajili baina ya wachezaji na klabu ama timu dhidi ya timu ambapo baadhi ya wachezaji wanatuhumiwa kusaini mikataba katika timu mbili tofauti na klabu nyingine zinatuhumiwa kuwa na mikataba ya uongo kwa baadhi ya wachezaji ili ziwang’ang’anie waendelee kubakia katika vikosi vyao.

Mfano wa kesi zilizoibuka ni ya aliyekuwa kipa wa Polisi Tanzania, Metacha Mnata ambaye kwa sasa ametangazwa kusajiliwa na timu ya Singida Big Stars ambayo ilipanda daraja msimu uliomalizika.

Kwa mujibu wa uongozi wa Polisi Tanzania, kipa huyo anayedakia pia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, bado ni mchezaji wao halali na ana mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia timu hiyo.

Mgogoro mwingine ni wa mshambuliaji Juma Liuzio ambaye ameilalamikia klabu ya Mbeya City kumzuia kuondoka kwa kudai bado ana mkataba wa kuitumikia wakati huo yeye akifahamu kuwa mkataba wake na klabu hiyo umeshamalizika mara baada ya msimu uliopita kufikia tamati.

Hao ni baadhi tu ya wachezaji ambao mashauri yao yamejulikana hadharani lakini kiuhalisia wapo wengine ambao migogoro yao ya kimkataba kwa sasa ipo katika kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kutafutiwa ufumbuzi kabla ya msimu kuanza.

Hili sio jambo geni na mara kwa mara limekuwa likijitokeza kila unapofika muda wa dirisha la usajili kama hivi sasa na kwa hali ilivyo, inaonekana wazi kuwa migogoro hii ya kimikataba itaendelea kuwepo kama hatua stahiki hazitachukuliwa.

Sababu kubwa ambayo inaweza kuwa inachangia muendelezo wa migogoro hiyo ya mikataba baina ya wachezaji na klabu ni watu kukosa elimu stahiki ya kufahamu haki na wajibu wao katika kutumikia mikataba ambayo wanasaini.

Wachezaji hawafahamu athari za kusaini mikataba katika timu mbili tofauti kwa wakati mmoja na hii pengine inachangiwa na busara ambayo huwa inatumika katika kusuluhisha migogoro pindi makosa kama hayo yanapotokea kwa kuzitaka klabu zimalizane kwa kile kinachosemwa kuwa ni kulinda kipaji cha mchezaji.

Lakini pia klabu nazo zimekuwa haziwajibishwi ipaswavyo pindi zinapofanya makosa ya kurefusha mikataba kisirisiri pasipo upande wa mchezaji kufahamu.

Klabu na wachezaji wetu mara kwa mara wanapumbazwa na busara hizo na kuendelea kufanya mambo kienyeji pindi msimu wa usajili unapofika jambo ambalo limekuwa likisababisha kesi za mara kwa mara zinazohusu usajili.

Elimu ya usajili itawafanya wachezaji wafahamu kuwa ni makosa kusaini mikataba ya timu mbili tofauti lakini pia watatambua kwamba wanahitajika kupata uthibitisho wa kumalizika kwa mikataba yao na timu moja kabla ya kusaini ya timu nyingine.

Kwa upande wa timu pia zitafahamu kwamba zinapaswa kujiridhisha juu ya uhalali wa mchezaji kabla hazijamsajili lakini pia kwa baadhi ya timu kufahamu kwamba ni kosa kisheria kughushi mkataba wa mchezaji.

Janjajanja ambazo klabu na wachezaji wamekuwa wakiendelea kuzifanyakatika usajili na kukwepa kufuata njia sahihi haziwezi kuwasaidia na badala yake zinaweza kuja kuwaingiza matatizoni iwapo mamlaka zikiamua kuwa kali na kuwachukulia hatua.