MTU WA PWANI: DTB isirudie makosa ya wenzao Ligi Kuu

Saturday May 14 2022
DTB pic
By Charles Abel

LIGI ya Championship (Ligi Daraja la Kwanza) msimu huu imebakiza raundi mbili kabla ya kufikia tamati huku ayari timu moja ikiwa imeshajihakikishia kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Timu ambayo imekuwa ya kwanza kupanda Ligi Kuu ni DTB ambayo ilikata rasmi tiketi ya kupanda daraja baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Pamba, Jumapili iliyopita katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Ushindi huo uliifanya DTB FC kufikisha jumla ya pointi 65 ambazo zinaweza kufikiwa na timu moja tu kwenye Ligi hiyo ambayo ni Ihefu jambo linaloipa uhakika wa kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi ya Championship ambazo kikanuni ndizo timu zinazopanda Ligi Kuu.

Kupanda Ligi Kuu kwa DTB FC ni jambo lililotegemewa na wengi kutokana na maandalizi na mipango mizuri ambayo timu hiyo ilifanya na kuweka kabla na hata ligi ilipoanza jambo lililopelekea ipate matokeo mazuri ambayo leo hii yamezaa matunda kwa timu hiyo kupanda Ligi Kuu.

Kwanza ilisajili kundi kubwa la wachezaji wenye uzoefu baadhi wakiwa ni wale waliotamba katika Ligi Kuu kwa nyakati tofauti na hata kucheza mechi za mashindano ya kimataifa kama vile Amissi Tambwe, Nicholas Gyan, David Mwantika, Juma Abdul, Yusuf Mlipili, Rajab Zahir, Yannick Tusilu, Tafadzwa Kutinyu na Owen Chaima.

Wachezaji hao ndio wamekuwa chachu ya timu hiyo kutamba katika Ligi hiyo na kujihakikishia kupanda mapema na kuthibitisha hilo, Tambwe aliyewahi kung’ara katika vikosi vya Simba na Yanga kwa nyakati tofauti ndiye mfungaji anayeongoza katika mashindano hayo na anayemfuatia ni pacha wake kwenye timu hiyo Nicholaus Gyna.

Advertisement

Ukiondoa usajili wa wachezaji wazoefu na wanaolifahamu vyema soka la Tanzania, kingine ambacho kimeibeba DTB FC ni huduma bora ambazo imekuwa ikizitoa kwa wakati kwa wachezaji wake kama vile mishahara, posho, malazi na nyinginezo jambo ambalo limekuwa likiwapa morali ya kufanya vyema.

Hata hivyo, DTB FC wanapaswa kukumbuka kwamba kupanda Ligi Kuu ni jambo moja na kuweza kuhimili ligi hiyo na kuweza kuleta ushindani ama kubakia katika misimu inayofuata ni jambo lingine.

Maisha ya Ligi ya Championship ni tofauti na yale ya Ligi Kuu hivyo wanapaswa kuhakikisha wanajiimarisha zaidi katika maeneo mbalimbali hasa ya kiutawala, usimamizi na kiufundi ili waweze kufanya vyema pindi watakapokuwa wakishiriki Ligi Kuu.

Kwanza wanahitajika kuimarisha kikosi chao kwa kuongeza wachezaji wenye ubora zaidi katika nafasi muhimu na zinazotengeneza uimara wa timu kama vile mshambuliaji wa kati, kiungo mshambuliaji, kiungo wa ulinzi, mlinzi mmoja au wawili wa kati pamoja na kipa.

Simaanishi waliopo kwenye nafasi hizo kwa sasa uwezo wao ni mdogo, bali wanapaswa kuongezewa ushindani na benchi la ufundi likapewa kikosi kipana ambacho kitawapa wigo mpana wa upangaji wa kikosi hasa inapotokea baadhi ya wachezaji ni majeruhi, wameonyesha kiwango dhaifu au wanatumikia adhabu.

Sio rahisi kwa timu kufanya vyema katika Ligi Kuu ikiwa ina kikosi kidogo kwani hupelekea wachezaji kuchoka na majeraha ya mara kwa mara ambayo hupelekea kutopata matokeo mazuri.

Lakini pia wanapaswa kuwa na matumizi mazuri ya fedha zile watakazopata kutokana na udhamini wa ligi, wadhamini binafsi, viingilio vya mashabiki pamoja na michango ya watu wenye mapenzi na timu hiyo.

Ubadhilifu wa fedha hupelekea hasara kwa timu na hivyo kufanya ishindwe kutoa huduma stahiki na bora kwa wachezaji jambo ambalo huwa mwanzo wa kufanya vibaya na kusababisha anguko la klabu husika.

Iko mifano ya timu nyingi ambazo zilifanya vizuri na zilikuwa na umoja, utawala na usimamizi mzuri pindi zilipokuwa madaraja ya chini lakini zilipofika Ligi Kuu, mambo yalibadilika na kujikuta zikikumbwa na migogoro na matumizi mabaya ya fedha, matatizo ambayo yalichangia kuzirudisha zilikotoka na nyingine kuporomoka zaidi.

Bahati nzuri kwao ni kwamba imezungukwa na watu ambao wanafahamu vyema soka la Tanzania na kumbukumbu ya timu zilizopanda kwa staili yao kisha zikaporomoka wanayo hivyo hilo litakuwa darasa tosha kwao kujipanga vyema kwa ajili ya ushiriki wao katika Ligi Kuu.

Hatutegemei kuona nao wakifuata mkumbo wa wenzao ambao hivi sasa wamesahaulika katika Ligi Kuu.

Advertisement