MTU WA MPIRA: Wachezaji Simba wanacheza kama Messi?

KUNA wakati lazima ukweli usemwe. Haijalishi ni mchungu kiasi gani. Haijalishi unamuumiza nani, lakini ukisema unakuwa huru. Leo nitasema ukweli kuhusu hawa wachezaji wa Simba.

Ni kweli Simba imewekeza fedha nyingi msimu huu katika usajili. Imeshusha wachezaji wengi wa gharama kubwa. Hawa kina Che Fondoh Makone, Willy Onana, Fabrice Ngoma na Luis Miquissone wameikamua Simba mamilioni ya fedha.

Usisahau kuhusu Clatous Chama ambaye ameongeza mkataba mpya. Usisahau kuhusu kina Aishi Manula, Shomary Kapombe, John Bocco na wengineo waliiongeza mikataba msimu uliopita. Simba imewekeza fedha nyingi sana katika usajili.

Mbali na kuwekeza fedha, Simba imekuwa ikitoa posho kubwa kwa kila mechi wanayocheza endapo watashinda. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again alisema wakati anazungumza na Azam TV kuwa waliahidi kutoa Sh500 milioni endapo Simba ingeifunga Al Ahly kwa Mkapa kwenye mchezo wa ufunguzi wa African Fooball League (AFL).

Ni fedha nyingi sana hata kwa kuzitamka. Ni fnyingi hata kwa kuziandika. Ni Watanzania wachache wamewahi kushika. Hata hivyo bado Simba haikupata ushindi. Inashangaza sana.

Ukitazama kikosi kina mastaa wengi kuliko hata watani wao Yanga. Ila ndani ya uwanja, Yanga inacheza vizuri kuliko Simba. Kwanini? Subiri nitakueleza.

Wachezaji wengi wa Simba wanacheza kama hawajielewi. Wanacheza kama kikundi fulani cha watu wenye shughuli zao nyingine wanaokutana kila jioni kufanya mazoezi kujiweka sawa. Ni kama wanavyofanya ndugu zangu kina Swedi Nkwabi pale Mango Garden, Kinondoni. Wachezaji wa Simba wanacheza kama vile wamewahi kushinda kila kitu katika maisha yao ya soka. Ni kama vile wamewahi kutwaa ubingwa wa Afrika. Huku mtaani tunasema wa -acheza ‘kifaza’ sana. Wa acheza kistaa.

Ni kama vile wanacheza mechi imalizike wakaendelee na shughuli zao nyingine. Ukitazama wanaojituma ni wachache. Unaweza kuwahesabu. Henock Inonga anacheza kama Sergio Ramos wa miaka 36. Che Malone anacheza kama Harry Maguire. Kapombe anacheza kama ameshinda Kombe la Dunia majuzi na Argentina. Wanacheza kama watoto wa Umisseta. Inashangaza sana. Chama anacheza kama Lionel Messi. Kama ametoka kushinda Ballon d’Or ya sita majuzi. Anacheza kifaza. Timu ikiwa haina mpira utadhani siyo yake. Hajisumbui kukaba. Hajisumbui kurudi. Ni kichekesho.

Saido Ntibazonkiza anacheza kama vile Kelvin De Bryune. Anataka kufanya vitu lukuki wakati hata vichache vinamshinda. Timu ikipoteza mpira anatembea kama bwana shamba anayekagua shamba. Ndio mchezaji tegemeo. Ngoma anacheza vizuri akiwa na mpira. Timu ikipoteza mpira anakuwa mzito kama a amembeba mtu mgongoni. Anakimbia kama ana mawe mfukoni.  Tazama bao la kwanza la Yanga dhidi ya Simba. Mpira ulipotea alipokuwa Ngoma. Yanga wakaondoka kushambulia. Ngoma akawa anakimbia taratibu kurudi nyuma kama bwana harusi wa miaka 40. Yanga ikafanya shambulizi la kwanza na Simba wakaokoa. Ngoma bado hajafika kwenye boksi. Yanga wakashambulia tena na kufunga mbele ya macho yake.

Unafikiria kweli huyu ndiye Ngoma aliyesajiliwa kuongeza nguvu kwenye kiungo? Sio kweli. Anacheza kawaida.  Yule Sadio Kanoute wa msimu uliopita sio huyu. Kanoute anamkaba Pacome Zouzoua kama kibaka wa Mombasa. Hana wasiwasi. Pacome anaondoka mbele yake na kwenda kusababisha bao. Huyu ndiye Kanoute tunayemfahamu? Sio kweli.

Kwenye kikosi cha Simba wachezaji wanaojituma hawazidi watatu. Kuna Kibu Denis na Mzamiru Yassin. Mwingine ni nani? Mtafute mwenyewe.

Halafu kuna wachezaji wengine wamesajiliwa wako tu benchi. Ni kama wamefika Kitambaa Cheupe, Sinza. Hawana wasiwasi hata kidogo. Hawapambanii nafasi zao. Ndio hawa kina Shaaban  Chilunda, Abdallah Hamis, Duchu na wengineo. Ni kama wako ‘vakesheni’ hivi. Mchezaji umesajiliwa Simba katika dirisha kubwa huonyeshi dalili ya kutaka kucheza. Inashangaza.

Ukweli ni kwamba hata aje kocha gani kama wachezaji wa Simba watakuwa wanacheza kawaida hivi timu itakuwa na wakati mgumu. Wachezaji lazima wajitume.

Hebu itazame Yanga. Wachezaji wake siyo wakubwa kivile, lakini ndani ya uwanja wanacheza kama hakuna kesho. Wanakimbia muda wote. Wanakaba kwa pamoja. Hakuna mchezaji wa Yanga anacheza kivivu.

Hii ndio sababu hadi sasa unashindwa kusema ni mchezaji gani wa Yanga anacheza vibaya. Wengi wanacheza vizuri. Utaona tu hawa kina Aziz Ki, Pacome, Maxi Nzengeli wanatajwa zaidi, lakini ukweli ni kwamba wote wanajituma.

Wale kina Dickson Job, Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto pale nyuma wanafanya kazi nyingi chafu. Wanacheza kibabe muda wote. Hawana urembo. Huyo Yao Kouassi anacheza kama ametumwa na kijiji. Anajituma hadi anaboa. Hao kina Mudathir Yahya na Khalid Aucho wanacheza kama hakuna kesho. Hivi ndivyo timu inapaswa kuwa. Wachezaji wanatakiwa kujituma muda wote. Kwa Simba bado. Wanacheza kama ndio mabingwa watetezi wa ligi. Wanacheza kama ndio wametoka kutwaa ubingwa wa African Football League (AFL). Yaani wanachekesha  kuliko Ndaro na Eliudi.