MTU WA MPIRA: Tuwaambie Simba SC ukweli au tuwaache wapambane na hali yao

UKWELI ni kwamba Simba ya msimu huu ni dhaifu. Ni dhaifu kuliko Simba nyingine yoyote iliyocheza Ligi Kuu ndani ya miaka mitano iliyopita. Huo ndio ukweli mchungu.

Simba ya msimu huu haina uhakika wa kupata ushindi nyumbani ama ugenini. Haina uhakika wa kupata ushindi kwenye mechi kubwa ama ndogo. Kwa kifupi ni Simba ya mchongo.

Imekuwaje Simba iliyokuwa tishio msimu uliopita kuwa dhaifu ghafla hivi? Hilo ndilo swali linalohitaji majibu kwa sasa. Kama swali hili halitajibiwa, Simba itaendelea kuwa dhaifu kwa msimu ujao na mingine mingi.

Sababu ya kwanza Simba kuwa timu ya kawaida msimu huu ni kufeli katika usajili wa dirisha kubwa na dogo. Simba haikufanya usajili mkubwa msimu huu.

Ilikwenda kukusanya lundo kubwa la wachezaji wa kawaida. Matokeo yake nini kimetokea? Hakuna kitu cha maana wanafanya kwenye ligi.

Ukiachana na Sadio Kanoute ambaye amekuwa chaguo la kwanza mara zote msimu huu nani mwingine ni mchezaji wa daraja la Simba? Hakuna!

Yule Pape Sakho ni mchezaji mzuri wa kawaida. Yule Peter Banda ni mchezaji wa kawaida. Achilia mbali hao kina Jimmyson Mwanuke, Yusuph Mhilu na wengineo.

Wengi watabisha kuhusu Sakho, watadai kuwa ni mchezaji wa maana. Vipi amefunga mabao mangapi kwenye Ligi Kuu msimu huu? Ana asisti ngapi? Ametengeneza nafasi ngapi za mashambulizi ya Simba? Hapa ndipo kwenye kichekesho chenyewe.

Hadi kufikia mbili ya tatu ya msimu Sakho ana mabao mawili na asisti moja tu. Yaani kwa kifupi amehusika katika mabao matatu tu ya Simba. Banda ana bao moja na asisti moja. Mhilu ana bao moja wakati Mwanuke hana kitu.

Kibu Denis pamoja na kupewa uraia wa Tanzania amefunga mabao manne na asisti mbili tu. Amefunga bao moja tu tangu ndani ya 2022. Huyu ni mshambuliaji kweli? Ni kichekesho.

Hilo ndilo lundo la wachezaji wa kawaida waliosajiliwa Simba msimu huu. Unawezaje kufanya vizuri na wachezaji hao?

Pili, Simba iliwauza Luis Miquissone na Clatous Chama mwanzoni mwa msimu. Hawa ndio walikuwa roho ya timu. Miquissone na Chama waliibeba Simba kwenye ligi na kimataifa. Kuna wakati timu ilikuwa kawaida, lakini wao waliibeba mabegani mwao.

Chama amerudi, lakini ukweli ni kwamba bado hajawa fiti vilivyo. Chama huyu sio yule. Huyu amepoa kidogo. Hajachanganya kama alivyokuwa hapo kabla.

Msimu uliopita Chama alifunga mabao manane na kutoa pasi 15 za mabao.

Achilia mbali mashambulizi lukuki aliyoanzisha ambayo yalizaa mabao kwenye Ligi Kuu. Msimu huu tangu arudi ana matatu na hana asisti. Je Chama huyu ndio yule? Hapana.

Tatu, mastraika wa Simba msimu huu wamekwama kabisa. John Bocco na Chris Mugalu hawana bao lolote kwenye Ligi Kuu hadi sasa. Nini kimewakuta? Sijui ila ni wazi wameshuka viwango.

Ni Meddie Kagere tu mwenye mabao saba. Kichekesho ni kwamba Kagere huyu mwenye mabao hayo bado sio chaguo la kwanza pale Simba.

Yaani hao Bocco na Mugalu ambao hawana bao ndio wenye nafasi kikosi cha kwanza. Inachekesha sana.

Niliwahi kuandika hapa kuwa Simba imejaa wachezaji wengi wazee na ndicho kilichotokea kwa mastraika wake msimu huu. Akili inataka, mwili hautaki. Wamechoka mno.

Simba inatakiwa kufanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake kama inataka kufanya vizuri msimu ujao.

Vinginevyo wataiona Yanga ikitwaa ubingwa tena na tena.