MTU WA MPIRA: Hata Dunia hii ingemshangaa kiaina beki Joash Onyango

NILISIKIA beki Joash Onyango alitaka kuondoka Simba. Niliamini zaidi baada ya kusoma Mwanaspoti ilipoandika habari yake. Ilikuwa ni ukweli mtupu.
Lakini nilithibitisha baada ya Onyango kushindwa kusafiri na timu kwenda Misri. Ni ushahidi tosha kwamba alitaka kuondoka Simba.
Nikashangaa zaidi kusikia amekimbilia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kushtaki, akilazimisha kuondoka Msimbazi.
Inashangaza sana kusikia habari hizi. Onyango amesaini mkataba mpya Simba hivi karibuni. Alitaka pesa ndefu kwenye mkataba wake mpya.
Moja ya hoja za Onyango wakati anataka mkataba mpya ni madai kuwa Sergie Paschal Wawa (yupo Singida Big Stars kwa sasa) analipwa pesa nyingi, lakini kazi kubwa anafanya yeye pale Simba. Inachekesha sana.
Hivi ndivyo Onyango alivyopewa mkataba mpya Simba. Amepewa mkataba baada ya kuongea sana. Ni kweli Simba walitaka kumwongezea mkataba ila wa mwaka mmoja lakini Onyango alitaka wa miaka mitatu. Kwa umri ule hapana.
Yawezekana kweli Onyango ana miaka 29 kama vyanzo mbalimbali vinavyoonyesha. Ila ukweli ni kwamba Onyango kuna kasi ya mechi zinamshinda. Ipo wazi.
Kuna uzito ambao Onyango yupo nao ambao unamfanya washambuliaji wa timu pinzani wang'are mbele ya Simba. Hasa washambuliaji wepesi.
Ni wazi kuwa Simba iliona pengo anapocheza Wawa na Onyango. Kuna kitu kilikuwa kinapungua. Wakaamua kumsajili Mohamed Ouattara.
Nilishtushwa kusikia Onyango amegoma kusafiri na timu Afrika Kusini akidai kuwa hafurahishwi na hali ya mambo klabuni hapo.
Beki huyo aliyewahi kutwaa tuzo kadhaa Kenya hafurahishwi na kukaa benchi pale Simba. Inashangaza sana. Onyango anakereka kukaa benchi mechi tatu tu benchi pale Simba.
Alikaa benchi kwenye mechi moja ya Ngao ya Jamii na mbili za Ligi Kuu tu na kuanza kulalamika. Akiona hatendewi haki pale Simba. Akiona kama Simba inamwonea. Inashangaza sana.
Mchezaji mzuri siku zote anataka ushindani. Lakini kwa Onyango kusajiliwa kwa Ouattara tu tayari alitaka kukimbia. Hataki kushindana hata kidogo. Ilikuwa ni ajabu na kweli.
Hii ndio sababu Onyango alitaka kuondoka Simba. Alitaka kuondoka siku chache tu baada ya kuona watu wengine wanacheza namba yake pale Simba.
Hii ni ishara kuwa aliona kama mazoezini anafanya vizuri kuliko wote na mechi wanapangwa wengine. Aliona kama hatendewi haki. Inashangaza.
Onyango amekaa Simba miaka miwili. Na wakamwongeza mkataba mwingine. Hii ni ishara kwamba ni beki mzuri. Hakuna mtu mwenye mjadala kabisa.
Onyango ni aina ya beki ambaye kila timu kwenye Ligi Kuu imetamani kuwa naye. Hata Yanga kuna wakati imemtamani Onyango. Huo ndio ukweli mtupu.
Hakuna ubishi kwamba kukosekana kwake kwenye mechi ya watani wa jadi kumechangia Simba kufungwa mabao mawili. Simba haijawahi kuruhusu mabao hayo ikiwa na Onyango uwanjani.
Hata hivyo pamoja na yote bado sikufurahishwa na taarifa za Onyango kutaka kuondoka Simba. Ilikuwa ni mapema mno kwake.
Kwa beki wa kizazi kipya kama Onyango alipaswa kupambana kwanza. Sio kutaka kukimbia. Ni lazima tukubali kuwa Simba ni timu kubwa sana Afrika kwa sasa. Kubwa zaidi ya wakati ule anakuja Onyango.
Kama Simba ni timu kubwa Afrika lazima itajiimarisha kila siku. Ndio maana msimu huu imechukua wachezaji bora wa Al Hilal ya Sudan, Asante Kotoko ya Ghana na Rivers United ya Nigeria.
Hii ni ishara tosha ya timu kubwa. Inachukua wachezaji bora kwingine inawaleta kwake. Ndio walichofanya Simba msimu huu.
Sasa inashangaza kuona wachezaji waliokuwepo kama Onyango wanaanza kutaka kuondoka mapema yote hii. Hawataki kabisa watu wapya katika nafasi zao.
Mchezaji mzuri siku zote haogopi mtu kusajiliwa katika nafasi yake. Anaogopa changamoto uwanjani. Wengine wanaogopa hata kwenye uwanja wa mazoezi. Ni ajabu na kweli. Ila ndio soka letu.
Uzuri ni kwamba Onyango amesalia kikosi cha Simba baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili huku Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likimtaka beki huyo aendelee kuitumikia Simba kama mkataba unavyoeleza. Hivyo ataendelea kukipiga na amecheza mechi iliyopita ya Ligi Kuu dhidi ya Prisons na pengine leo akacheza katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi.