MTU WA MPIRA: Azam FC inahitaji mtu mwenye roho ‘katili’

TUNAFUNGA msimu mwingine wa Ligi Kuu Bara hivi karibuni. Ulikuwa msimu mzuri na wenye ushindani mkubwa. Inavutia sana.

Hata hivyo ni mwaka wa 10 sasa tangu Azam FC ilipotwaa taji lake la kwanza na la mwisho la Ligi Kuu. Ni miaka mingi sana hata kwa kuitamka.

Mtoto aliyezaliwa mwaka ule Azam FC inatwaa ubingwa kwa sasa yupo darasa ya tatu au la nne. Yaani mtoto amezaliwa mpaka amekuwa na akili ya kutambua mema na mabaya, lakini bado Azam FC haijaweza kutwaa ubingwa mwingine. Inashangaza sana.

Tena bahati nzuri kwa Azam FC wakati ule ilitwaa ubingwa kwa rekodi nzuri ya kutopoteza mchezo hata mmoja. Waliwezaje? Subiri nitakwambia.

Hebu fikiria imeichukua Yanga SC miaka 57 kuweza kuweka rekodi kama hiyo ya kutwaa ubingwa bila kupoteza mchezo. Walifanya hivyo msimu uliopita.

Iliwachukua Simba SC miaka 45 kuweka rekodi kama hiyo ya Azam FC walipotwaa ubingwa bila kupoteza mchezo mwaka 2010. Lakini, Azam FC iliweka rekodi hiyo ndani ya miaka sita tu tangu ilipoanza kushiriki Ligi Kuu Bara. Azam FC waliwezaje?

Ni katika nyakati hizi Azam FC ilikuwa imekamilika katika kila idara. Ilikuwa imara katika uongozi, benchi la ufundi na wachezaji.

Mtendaji Mkuu kwa wakati huo alikuwa Nassoro Idrissa ‘Father’. Mtu mmoja makini sana na mwenye utashi wa juu. Alikuwa anaifanya kazi yake vyema. Hakuwa na longo longo wala siasa.

Ni katika nyakati hizo za utendaji wake Azam FC ilikuwa imara. Nidhamu ilikuwa juua katika utendaji. Kila kilichopaswa kufanyika kilikwenda kwa wakati. Huyu sasa ndiye mtendaji mkuu siyo kama hawa waliomfuatia.

Kwenye uongozi wa shuguli za timu kila siku alikuwepo Jemedari Said. Mtu mmoja shupavu. Hana konakona. Alikuwa meneja wa timu.

Aliwanyoosha sana wachezaji. Akaweka sheria zake kambini. Ukichelewa kuripoti kambini ulikuwa unakatwa mshahara. Hakuwa anatazama sura ya mtu. Kuna wakati aliwahi kumkata mshahara hadi staa wa timu, Kipre Tchetche. Wewe unaweza?

Huyo sasa ndiye alikuwa meneja wa timu ya ubingwa, siyo dhaifu kama hawa waliomfuatia.

Jemedari aliondoka baada ya kushindwana na aliyekuwa mtendaji mkuu mpya, Saad Kawemba. Walipishana misimamo akaamua kuondoka zake.

Upande wa tatu lilikuwapo benchi la ufundi. Azam FC ilianza msimu na kocha raia wa England, Sterwart Hall. Huyu alimaliza mechi 13 za mzunguko wa kwanza bila kupoteza. Alikuwa nafasi ya pili nyuma ya Yanga akizidiwa alama moja tu. Ilikuwa rekodi nzuri.

Kocha huyo akapata ofa nyingine nzuri kwingineko na kuamua kuondoka zake. Ilikuwa pigo kubwa kwa matajiri hawa wa ligi yetu. Lakini wakatuliza akili.

Wakaenda kumchukua raia wa Cameroon, Joseph Omog. Kocha huyu alikuwa ametoka kushinda Kombe la Shirikisho Afrika mwaka mmoja nyuma akiwa na AC Leopard ya Kongo Brazzaville.

Alikuwa kocha bora sana Afrika wakati ule na jina lake liliimbwa kila mahali. Hata hivyo Azam FC walivunja benki na kumchukua. Akaja na kuwapa ubingwa.

Kwa upande wa wachezaji Azam FC ilikuwa imewekeza kwelikweli. Hebu fikiria safu  ya ushambuliaji ilikuwa na John Bocco, Gaudence Mwaikimba na Kipre Tchetche.

Halafu kulikuwa na chipukizi kama Joseph Kimwaga na Farid Musa ambao walikuwa wakicheza kwa dakika chake.

Huyu Tchetche alikuwa kama Mayele. Mshambuliaji wa kweli. Anatisha kama pori la Kibiti. Ana kasi, ana uwezo wa kupiga chenga na kufunga. Baada ya kutwaa ubingwa alitangazwa kuwa mchezaji bora wa msimu. Hakuna aliyebisha.

Hii ndio ilikuwa Azam FC iliyoshiba. Ilikamilika kila idara kama nilivyokueleza hapo awali. Baada ya hapo nini kilitokea? Usiwe na haraka nitakwambia hapahapa.

Azam FC iliimarisha kikosi zaidi kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ikawachukua kina Didier Kavumbagu na Frank Domayo pale Yanga. Ikamsajili Shomari Kapombe. Ikashusha na vifaa vingine vya maana.

Bahati mbaya hawakuweza kufanya vizuri katika mashindano hayo, lakini kwenye Ligi Kuu waliendelea kuwa washindani. Wakamaliza nafasi ya pili nyuma ya Yanga.

Msimu uliofuata wakachukua wachezaji wa maana zaidi kama Sergie Wawa na wengineo. Wakatwaa ubingwa wa Kagame Cecafa Cup bila kupoteza mchezo wala kuruhusu bao. Walikuwa imara sana.

Msimu huu pia wakapoteza ubingwa dakika za mwisho kwa Yanga iliyokuwa imara zaidi. Yanga ile ya kina Donald Ngoma, Amissi Tambwe, Saimon Msuva na wengineo. Ungewalaumu nini Azam FC? Hakuna.

Nini kilitokea baada ya hapo? Azam FC ikaanza kusambaratika. Wakaanza kuja watendaji wakuu wa ajabu. Ni kama yule aliyekuja na kushusha mishahara ya wachezaji, ada ya usajili na kufuta posho.

Matokeo yake wachezaji kama Bocco, Kapombe, Aishi Manula na wengineo wakatimka klabuni hapo. Timu ikawa dhaifu kuliko udhaifu wenyewe. Ikaanza kusajili wachezaji wa ajabu. Wachezaji wa viwango vya Ihefu na Ruvu Shooting wakatua Chamazi kwa kigezo cha kubana matumizi.

Miaka ikaenda na vitu vikazidi kubadilika. Azam ikazidi kuwa dhaifu zaidi.

Hebu fikiria timu yenye kila kitu. Ina pesa. Ina uwanja wa kisasa. Ina hosteli nzuri na basi la kisasa, lakini ni msimu wa sita sasa haijaweza hata kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu. Inachekesha.

Miaka yake ya mwanzo Azam FC hata isingetwaa ubingwa, basi ingemaliza katika nafasi ya pili. Ilikuwa ni wababe wa kuwatenganisha Simba na Yanga pale kileleni. Ilikaa katikati yao. Nini kimebadilika?

Cha kwanza ni hawa watendaji wa kila siku wa timu. Azam FC kwa sasa ina watendaji dhaifu pengine kuliko nyakati zote. Hakuna kazi ya maana wanayofanya pale Chamazi.

Wanafanya kazi kwa mazoea. Kwa miaka mingi wameshindwa kusajili wachezaji wa maana. Wanasafiri na timu kila mahali kama ufahari tu.

Hawana mipango bora ya muda mfupi wala mrefu. Kwa kifupi wanaiangusha timu.

Upande wa benchi la ufundi wameshindwa kuwa na makocha wa maana. Na hata wakileta kocha mzuri hawezi kudumu kwa sababu wanashindwa kumpa mazingira mazuri ya kazi.

Mwisho wa siku kitu kizuri pale Azam FC imebaki kuwa basi na ule uwanja. Ila kwa upande wa timu bado bado.

Msimu huu wanashindana na Singida Big Stars kumaliza nafasi ya tatu. Msimu uliopita walishindana na Geita Gold. Yaani Azam FC imekuwa timu ya kushindania nafasi ya tatu? Siyo kweli, kuna kitu hakipo sawa.

Acha tuone msimu ujao watakuja na jipya gani. Lakini ukweli ni kwamba Azam FC inahitaji mtu mmoja mwenye roho mbaya. Mtu anayeweza kuwanyoosha wachezaji, benchi la ufundi na watendaji wengine. Mtu ambaye atawafanya watu wote watambue majukumu yao na kufanya kwa wakati. Huyu ndiye mtu wanayemkosa kwa sasa.