MTU WA MASHABIKI: Yanga isijiamini sana, ubingwa Bara bado upo wazi

Saturday May 14 2022
Mastaa PIC
By Mwandishi Wetu

VITA ya ubingwa imeanza upya Ligi Kuu Bara. Sare tatu mfululizo ilizopata Yanga zimefufua matumaini kwa watetezi Simba. Pengo la pointi baina yao limepunguza badala ya kuongezeka. Hata zile kelele za mashabiki wa Yanga juu ya kubeba ubingwa mapema ni kama zimepungua.

Kuzitema pointi sita ghafla katika mechi walizoamini wangeshinda, zimewakata stimu. Kwa sasa ni zamu za mashabiki wa Simba kutamba.

Wanaamini lolote linaweza kutokea kwa timu yao kama watani wao wataendelea kudondosha pointi katika mechi zilizosalia.

Mechi tatu za ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, Biashara United na Mbeya City wanaamini ndizo zilizoshikilia hatma ya Yanga na kuwanufaisha Simba.

Simba wanaamini, Yanga ikichemsha katika mechi hizo nao wakapata matokeo mazuri, basi watakuwa na uhakika wa kutetea taji kwa msimu wa tano mfululizo.

Ingawa sio rahisi kuamini hilo, lakini katika soka lolote linaweza kutokea. Yanga ni kama ilishaona imemaliza kazi kwa kuongoza kwa muda mrefu msimamo wa ligi.

Advertisement

Pengo la pointi kufikia 14 liliwapa jeuri, lakini wakasahau kuwa msimu haujaisha na kila uchao timu pinzani zinapiga hesabu juu ya bonasi inayotolewa na Azam Media.

Huenda mmesahau, ngoja Mtu wa Mashabiki niwakumbushe, Bingwa wa msimu huu ukiacha kubeba ndoo, lakini atakomba Sh500 milioni, wakati mshindi wa pili atazoa Sh250 milioni na itakayomaliza nafasiya tatu itaondoka na Sh225 milioni.

Zawadi hizo haziishi hapo tu, timu itakayokamata nafasi ya nne itazoa Sh200 milioni, ilihali ile ya tano itaondoka na Sh65 milioni, wakati ya sita itazoa Sh60 Milioni na wa saba itachukua Sh55 milioni na itakayomaliza Nane Bora itaambulia Sh50 milioni.

Ofa hizo za mamilioni hayo ya fedha katika msimu wa kwanza wa udhamini wa Azam unazifanya karibu timu zote kuzipigia hesabu fedha hizo. Misimu kadhaa ya nyuma, zawadi za wadhamini katika ligi ziliishia kwa timu zilizokamata nafasi nne Bora.

Pia hata zawadi hizo za fedha za washindi hao wanne zilikuwa hazifikii hata zawadi anayopewa mshindi wa pili wa msimu huu ama timu inayomaliza ya tatu.

Hivyo, kila klabu ikizikumbuka fedha hizo na ligi kuwa lala salama, zinafanya kila moja kukaza buti na kucheza jihadi, ndio maana Yanga imekuwa ikibana.

Ndio maana Simba inataitiwa. Ndio maana Azam haijawa na uhakika wa kushinda mechi zake hata ikiwa nyumbani. Ndio inafanya Kagera Sugar, Mbeya City na hata Coastal Union kutokwa jasho viwanja vya nyumbani. Kila timu imekuwa ngumu.

Kwa hesabu za haraka Yanga, ilifanya vizuri duru la kwanza kuliko la sasa, licha ya kwamba imetema jumla ya pointi 12, sita zikiwa kila duru. Katika mechi za duru la kwanza ilitoka sare tatu na kuzitema alama sita katika mechi zao 15.

Kwa sasa ikiwa imesaliwa na mechi saba mkononi, tayari imezitema tena pointi sita katika sare tatu mfululizo dhidi ya Simba, Ruvu Shooting na Tanzania Prisons. Hakuna ajuaye yajayo katika mechi hizo saba zijazo.

Hata hivyo, nisiwakatishe tamaa mashabiki na wadau wa Yanga, bado timu ina nafasi ya kutwaa ubingwa wa 28, lakini sio kwa kujiaminisha moja kwa moja kama ilivyokuwa katika duru la kwanza.

Hata hao Simba nao wasijiamini sana kwamba wanaweza kupindua meza, kwa kuzingatia hata pointi ilizonazo sasa, imezipata kwa kuungaunga sana tofauti na ilivyokuwa ikitamba misimu minne iliyopita. Ukweli ndio huu.

Simba ya msimu huu haiaminiki. Mashabiki wanaona timu yao inashinda, lakini hawajui inashindaje kwa namna inavyocheza uwanjani. Haina makali na ule moto uliokuwa nao msimu uliopita. Wafungaji wake mahiri walioongoza msimu uliopita ni kama wamefungwa gavana. Hawafungi sana na hata wakifunga, sio kwa muendelezo kama ilivyokuwa msimu uliopita. Sitaki kuizungumzia Azam FC, kwani nayo ipo ipo tu. Haipo kwenye mbio za ubingwa, lakini haionyeshi inataka nini msimu huu. Namungo, KMC, Kagera Sugar, Polisi Tanzania kadhalika.

Hivyo kama kuna mtu alibeti ubingwa umeshajulikana hadi sasa na hata timu za kumaliza kwenye Nane Bora zimeshajulikana, ataliwa!

Ligi imeanza upya na lolote linaweza kutokea ndani ya raundi saba zilizosalia za kufungia msimu. Hii ni kutokana na ukweli mamilioni ya wadhamini na hali ilivyo katika msimamo wa ligi hiyo, bado unatoa nafasi ya maajabu kutokea. Kama Yanga haitagangamala, basi wajue Simba inaweza kutetea taji kwa msimu wa tano.

Kifupi ni kwa sasa kila timu lazima ishinde mechi zake ili kujiweka pazuri, vinginevyo ikifika Juni 29, yatazungumzwa mengine.

Advertisement