MTU WA MASHABIKI: Huyu Mkude anastahili kujengewa mnara

MAPEMA wiki hii Simba ilikuwa bize ikihitimisha wiki yao iliyonogeshwa na tamasha bab’kubwa la Simba Day.

Ni tamasha lililonoga na kuwapa mzuka mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kiasi cha kukurupukia mapema Uwanja wa Benjamin Mkapa katika kutotaka kupitwa na mambo.

Ni kama ilivyokuwa tu kwa watani wao, Yanga waliolifanya tamasha kama hilo Jumamosi likiwa na na jina la ‘Wiki ya Mwananchi.

Kifupi matamasha yote yalinoga kwa namna klabu hizo kubwa nchini zilivyoyaandaa, hata kama yalitofautiana kwa aina ya mashamshamu yake na hata yalivyohitimishwa kwa matokeo ya mechi za kirafiki za kimataifa ambazo timu zao zilizicheza.

Yanga ilihitimisha tamasha lake kwa kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Vipers ya Uganda, ilihali Simba ilishinda idadi kama hiyo dhidi ya St George ya Ethiopia.

Kwa Simba tamasha hilo la Simba Day lilikuwa ni la 14 kwao tangu lilipoasisiwa mwaka 2009 na uongozi wa kina Hassan Dalali na Mwina Kaduguda, wakati kwa Yanga lilikuwa la nne kwani wenyewe walianza mwaka 2019.

Mtu wa mashabiki naamini kila upande ulipata burudani waliyoitarajia na hizi kelele na kejeli baina yao ni mbwembwe tu za utani wa jadi, ila kwa kweli matamasha yote yalinoga na kuonyesha namna gani Watanzania walivyo vichaa wa soka.

Pitso Mosimane kutoka Afrika na nyota wa zamani wa Chelsea na Arsenal, Alexander Song na Solomon Kalou watakuwa mashahidi kwa kile walichokutana nacho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kuyahudhuria matamasha hayo.

Nyomi na vibe la mashabiki, huenda limewashangaza kwani mambo kama hayo yamezoeleka kuonekana barani Ulaya na sio kwenye soka la Afrika, lakini Simba na Yanga zimewaonyesha kuwa mashabiki wao wanazipenda klabu zao kindakindaki.

Ukiachana na yaliyojiri kwenye matamasha hayo na maandalizi ya sasa kwa klabu hizo kwa ajili ya pambano lao la Ngao ya Jamii ili kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara 2022-2023, kuna kitu ambacho sidhani hata kama wanasimba wanafikirikia.

Jonas Mkude. Kiungo fundi wa kukaba aliye mwandamizi katika klabu ya Simba. Hili ni tamasha lake la 12 kama mchezaji wa Simba. Ameyakosa matamasha mawili tu kama mchezaji, yaani la kwanza la 2009 na lile lililofuata la 2010.

Mengine yote yaliyofuata kuanzia 2011 hadi hilo la juzi, Mkude yumo. Ndiye mchezaji mwandamizi na ameweka rekodi ya kudumu ndani ya timu hiyo kwa muda mrefu.

Ndio, achana na misala yake inayotokana na suala la utovu wa nidhamu, Mkude ni mwamba kwelikweli. Uwanjani ni Nungunungu kweli dhidi ya wapinzani. Anajua kukaba. Anajua kutengeneza mashambulizi na anajua kuituliza timu na mara chache chache hufunga mabao kwa mashuti ya kushtukiza.

Tangu alipoanza kuitumikia timu hiyo mwaka 2011 na kuingizwa kwenye pambano la watani la Mei 6, 2012 lililoshuhudiwa Yanga ikicharazwa mabao 5-0, Mkude amejijengea heshima kubwa Msimbazi.

Hata kama kila dirisha la usajili huwa na taarifa kwamba huenda akatemwa, lakini mwamba yupo hadi leo. Miaka zaidi ya 10 kuitumikia timu moja tena kama Simba ni nadra sana. Yanga ndio yenye utamaduni wa kudumu kwa muda mrefu na wachezaji. Kwa Simba hutoka mara chache na Mkude ni miongoni mwa waliokaa na kikosi kwa muda mrefu.

Wapo wanaombeza. Wapo wanaomuona anabebwa na bahati kutokana na majanga yake ya mara kwa mara, lakini ukweli ni kwamba Mkude ni mchezaji aliyejiheshimisha Msimbazi. Kama ingekuwa kwa klabu za mataifa ya wenzetu, muda huu mabosi wangekuwa wakifikiria namna ya kumuenzi. Wangeweza hata kufikiria kumjengea mnara au sanamu yake kama heshima kwa mchango wako ndani ya klabu hiyo.

Wachezaji wa ndani na wa kigeni wanakuja na kuondoka, lakini Mkude yupo tu. Wenzake walioanza nao Simba B, wametawanyika kila sehemu kiasi kwa baadhi ya mashabiki walioanza kuijua Simba juzi juzi hawawajui kama walianzia soka lao Simba.

Walianza pamoja na Mkude hapo Msimbazi, kisha kutimka na kumuacha Mkude akiendelea kuwawapokea na kuwaaga wachezaji wanaosajiliwa Msimbazi kila msimu.

Mkude amewapokea na kuwaaga hadi makocha wanaoingia na kutoka Simba kwa kudumu kwa muda mrefu. Kwa hali kama hiyo kwa nini asipewe heshima yake?

Imani yangu siku atakapoamua kuondoka Msimbazi ama kustaafu soka atapewa heshima zaidi ya waliyopewa mastaa wengine wa klabu hiyo.

Kuna sababu ya kufanya hivyo. Mkude amewapita kwa mengi, hata kama kuna wakati huwa anazingua kiasi cha kuchukuliwa poa. Tusimhukumu kwa mambo yake nje ya uwanja. Tumheshimu kwa anachokifanya uwanjani na pia anachokifanyia Simba.

Anazeeka na utamu wake. Utamu zaidi Mkude ni yule yule wa juzi, jana na leo, hata kama inaelezwa akiwa viwanja vyake vya maraha huwa anaharibu sana, ila kwa kile anachokifanya uwanjani, kimembeba kuendelea kuaminika Msimbazi.

Tumpe heshima!